MUSSA YUSUPH
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, ameeleza kuwa, Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ustawi wa wananchi umeonekana.
Dk. Asha – Rose, aliyasema hayo alipohutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu katika Uwanja wa Sabasaba mjini Kibaha mkoani Pwani.
Alisema kuwa, Mkoa wa Pwani ni kituo cha biashara na utalii kupitia vivutio mbalimbali vilivyokuwa sehemu ya masimulizi kupitia filamu ya Tanzania Royal Tour.
Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu kumpigia kura Dk. Samia, wabunge na madiwani wa CCM, kwani kufanya hivyo ni kupigia kura maendeleo na utu wa Mtanzania.
Mratibu wa Kampeni Kanda ya Pwani, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Halima Mwamuya, alisema hadi sasa, ushindi mkubwa utapatikana katika mikoa hiyo.
Alieleza kuwa, wagombea ubunge na udiwani katika kanda hiyo yenye kujumuisha mikoa ya Pwani, Tanga na Morogoro wanakubalika.
Halima, alisema alikutana na kundi la wazee ambao nao wamemhakikishia kwamba, wanamuunga mkono Dk. Samia katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlawu, alisema wananchi wa mkoa huo, wanamshukuru Dk. Samia, kwani hakuna sekta yenye kumnufaisha mwanadamu ambayo haijaguswa.
Alisema upatikanaji pembejeo za mazao ya korosho na ufuta zimechangia kuongeza vipato vya wakulima.
Hata hivyo, aliomba barabara ya kwenda mikoa ya kusini eneo la Kokoto Mbagala kwani kipande hicho kimeendelea kuleta changamoto kwa wananchi.
Vilevile, aliomba ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoa ya kusini.




