Na ELIZABETH JOHN
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amewasihi wananchi kudumisha amani, kushirikiana na Jeshi la Polisi, kuhakikisha usalama wa taifa unaendelea kuimarika.
Simbachawene aliyasema hayo Dar es Salaam, katika ziara yake ya kutembelea baadhi ya vituo vya Jeshi la Polisi, vilivyochomwa moto jijini katika vurugu zilizotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Vituo alivyotembelea Waziri Simbachawene ni Mbezi Juu, Ubungo, Temboni na Salasala.
Alisema uharibifu wa miundombinu ya vituo hivyo, umekwamisha utendaji kazi wa baadhi ya vituo, jambo lililosababisha wananchi kushindwa kupata huduma.
Aliwaomba wananchi kuendeleza mshikamano na Jeshi la Polisi kwa kuwa, ndiyo msingi wa kudumisha amani na usalama wa Taifa.
Aidha, Simbachawene, alisema serikali imeanza hatua za haraka kuhakikisha miundombinu ya Jeshi la Polisi, inarejeshwa kwa ufanisi na wananchi waendelee kupata huduma.
Simbachewene aliwataka wananchi kudumisha mshikamano na Jeshi la Polisi na kushirikiana kwa karibu kuhakikisha upendo, amani na utulivu wa jamii vinaimarishwa.




