Na HAPPINESS MTWEVE, Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Daniel Chongolo, ameitaka Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), kuhakikisha sheria inazozisimamia, zinasomana na taasisi nyingine kuimarisha utendaji kazi.
Taasisi hizo ambazo zimeagizwa mifumo yake isomane na TOSCI ni pamoja na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Alisema utekelezaji wa majukumu yao ni shirikishi, hiyo itaongeza wigo wa uzalishaji mbegu kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Chongolo alisema hayo jijini hapa, alipokutana na viongozi mbalimbali, wakiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),
Alisema katika kutekeleza malengo na mikakati iliyopangwa na Wizara na Taasisi zake, viongozi wana wajibu wa kuhakikisha kazi hizo, zinakuwa na manufaa kwa wakulima.
“TOSCI ninawaelekeza, sheria mnazosimamia kama mamlaka zinasomana na Taasisi za TARI na ASA kwa kuwa utekelezaji wake unashabihiana,”alisema.
Aidha, aliitaka ASA kuongeza wigo wa uzalishaji mbegu kwa kushirikiana na sekta binafsi, huku akiitaka TARI kuongeza utafiti zaidi katika zao kama kokoa.
Pia, Chongolo aliiagiza TARI kuwafikiria watafiti wa mbegu ili wanufaike na utafiti wao, kama kuongeza umri wa kustaafu kwa watafiti wabobezi.
Akizumgumzia miradi inayoendelea chini ya wizara hiyo na taasisi zake, Chongolo alitaka ikamilishwe kwa wakati kwa mujibu wa mikataba.




