Na SIMON NYALOBI
BAADHI ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani nchini, wamepongeza uamuzi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuelekeza fedha zilizotengwa kwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru za Desemba 9, 2025, zitumike kurekebisha miundombinu iliyoharibika kutokana na vurugu za Oktoba 29, mwaka huu.
Wakizungumza na Uhuru hili kwa nyakati tofauti, viongozi hao, walisema uamuzi huo, unapaswa kuungwa mkono kwa kuwa una tija kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Makini, Coaster Kibonde, alisema uamuzi huo ni busara na unapaswa kuungwa mkono na watu wenye mapenzi mema na nchi.
“Nampongeza Rais Dk. Samia kwa uamuzi sahihi, umelenga kumsaidia mwananchi wa kawaida ambaye kila siku, anaitumia miundombinu hiyo.
“Tukumbuke maadhimisho ya Sherehe za Uhuru yanapita, lakini miundombinu itatumika muda mrefu, ni mahitaji ya wananchi, tumpongeze Rais Samia kwa uamuzi huo,” alisema.
Alifafanua kwamba, kurekebishwa miundombinu ya mabasi ya mwendokasi, kutapunguza changamoto ya usafiri kwa wananchi wa kawaida, ambao hutumia kwenda katika shughuli za uzalishaji mali.
Katibu wa Chama cha Wakulima (AAFP), Rashid Rai, alisema uamuzi wake, umejali maslahi ya wananchi wengi.
“Uamuzi wake, umeonesha utumishi uliotukuka, fedha zinakwenda kutumika kutatua matatizo ya watu wengi, badala ya sherehe pekee,” alisema.
Alisema uamuzi wa Rais Samia, unathibitisha dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wengi waliompa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano.
Vilevile, aliyekuwa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Ukonga, jijini Dar es Salaam, Rashid Mweyo, alisema uamuzi huo, ni sahihi kwa kuwa, fedha hizo zitagusa maisha ya wananchi wa kawaida.
Mwanasiasa huyo, alisema uamuzi huo utaponya ‘majeraha’ ya baadhi ya wananchi katika maeneo tofauti, wanaokosa huduma baada ya ofisi za serikali za mitaa na vituo vya polisi, kuchomwa katika vurugu hizo.




