Dar es Salaam
NA ATHNATH MKIRAMWENI
WANAFUNZI 937,581 wakiwemo wasichana 508,477 na wavulana 429,104 wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwakani ambapo wanafunzi hao watajiunga masomo hayo kwa mkupuo mmoja.
Idadi hiyo sawa na asilimia 100 ya wanafunzi waliokuwa na sifa ya kujiunga na kidato cha kwanza ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio ya Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kwamba kila mtoto anayefanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, anaendelea na masomo ya sekondari.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe, alisema wanafunzi hao wamepangiwa shule za sekondari za serikali ambazo zimegawanywa katika makundi mawili ambayo ni shule za bweni na kutwa.
“Shule za bweni zimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni shule za wanafunzi wenye ufaulu wa juu, shule za amali na shule za kitaifa,” alisema.
Alisema shule hizo za bweni za kitaifa zimepangiwa wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali ya nchi, kulingana na mgawanyo wa nafasi ulioainishwa kwa mujibu wa vigezo vya kitaifa.
“Uchaguzi wa wanafunzi ulifanyika kwa kuzingatia mwongozo wa uchaguzi wa mwaka 2024 na mgawanyo wa nafasi ulizingatia mikoa na halmashauri,” alisisitiza.
Alisema shule za sekondari za bweni kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu zimejumuisha wanafunzi 815 wakiwemo wasichana 335 na wavulana 480.
Alizitaja shule hizo ni lboru, Msalato, Kibaha, Kilakala, Mzumbe, Tabora Boys na Tabora Girls.
Katika shule za amali, alisema wanafunzi 3,441 wamechaguliwa ambapo wasichana 1,279 na wavulana 2,162.
“Kwa shule za bweni za kitaifa, wanafunzi 7,360 wamechaguliwa ambapo wasichana 5,014 na wavulana 2,346. Pia, wanafunzi 925,965 wakiwemo wasichana 501,849 na wavulana 424,116 wamechaguliwa kujiunga na shule za kutwa zinazopokea wanafunzi kutoka maeneo karibu na shule za msingi walizohitimu,” alisisitiza.
Profesa Shemdoe alisema serikali imejizatiti kuhakikisha maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hayaendi kinyume cha ratiba.
“Wanafunzi wote waliosajiliwa wataripoti shuleni ifikapo Januari 12 mwakani kwa wanafunzi waliochaguliwa shule za bweni na Januari 13 mwakani kwa wanafunzi wa shule za kutwa.
“Maandalizi ya shule na mipango ya uhamasishaji kwa wazazi, shule na jamii imekamilika, kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayechelewa,” alisisitiza.
Alisema kwa kuzingatia mabadiliko ya mitaala iliyoboreshwa, serikali itaendelea kuhakikisha utekelezaji wake.
“Ni muhimu kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wao wameandaliwa ipasavyo ili waweze kuanza masomo yao kwa wakati. Jamii inatakiwa kushirikiana na serikali kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni na kuanza masomo bila vikwazo vyovyote,” alisema Profesa Shemdoe.
Alimpongeza Rais Dk. Samia kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya elimu nchini kupitia uwekezaji wa serikali katika elimu na kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya elimu.




