Na MWANDISHI WETU
TIMU ya Azam FC, iliizamisha Simba baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mchezo huo, ulianza kwa kasi pande zote ambapo kila timu ikitaka bao la mapema kujiweka katika mazingira mazuri.
Katika dakika ya saba, mchezaji wa Simba, Joshua Mutale alishindwa kuitumia nafasi aliyoipata baada ya shuti lake kupaa juu nje ya lango, kabla ya Elie Mpanzu kufumua shuti kali lililogonga mwamba.
Azam FC walijibu shambulizi katika dakika ya 15, Iddy Selemani alipiga shuti kipa wa Simba, Yakoub Suleiman akapangua ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya 20, Simba walifanya shambulizi jingine lakini umakini mdogo wa Anthony Mligo alishindwa kukwamisha mpira wavuni akiwa eneo la hatari, mpira ukatoka nje ya lango.
Kipa wa Azam, Zubery Foba alionekana kufanya kazi ya ziada katika dakika ya 34, baada ya kuokoa shuti la Mpanzu.
Katika dakika ya 45, Simba nusura wapate bao la kuongoza ambapo Stephen Mukwala alipiga shuti likatoka sentimeta chache nje ya lango, hadi mapumziko ya kipindi cha kwanza timu hizo zilitoka zikiwa suluhu.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kulishambulia lango la Azam, dakika ya 46 Mpanzu alikosa utulivu ambapo shuti lake lilitoka nje kabla ya Selemani Mwalimu kurudia kosa dakika ya 70.
Azam ilionekana ikilishambulia lango la Simba kama nyuki, dakika ya 81, Japhet Kitambala alipachika bao la kuongoza baada ya kuunganisha krosi iliyochongwa na Nassor Saadun na kuujaza mpira wavuni.
Katika dakika ya 88, Azam ilipata bao la pili lililowekwa kimiani na Iddy Selemani kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Saadun na mpira kujaa kimiani moja kwa moja.
Simba alijibu shambulizi dakika ya 90 lakini Kibu Denis alishindwa kuitumia vyema nafasi hiyo baada ya kuingia na mpira eneo la hatari kipa wa Azam akaokoa hatari hiyo langoni mwake, hadi mchezo unamalizika, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kufuatia ushindi huo, katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam imepanda hadi nafasi ya tisa ikijikusanyia pointi tisa huku Simba ikibakia nafasi ya tano kwa pointi 12 kabla ya mechi ya jana kati ya Yanga na Coastal Union.
Simba: Yakoub Suleiman, Shomari Kapombe, Karabou Chamou/Jonathan Sowah, Steven Mukwala/Selemani Mwalimu, Anthony Mligo, Kante Alasane, Joshua Mutale/Kibu Denis, Morice Abraham, Yusuph Kagoma, Wilson Nagu na Elie Mpanzu.
Azam FC: Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Yoro Diaby, Landry Zouzou, Feisal Salum, Sadio Kanoute/ Nassor Saadun, Zidane Sereri/ James Akaminko, Idd Selemani. Pascal Msindo, Himid Mao na Japhet Kitambala.




