Na WAANDISHI WETU
WABUNGE wamewasihi Watanzania kulinda amani ya nchi kwa kuepuka uchochezi wa chuki miongoni mwao.
Mbungewa Kisarawe, Dk. Selemani Jafo amesema vijana hawana budi kutambua kwamba amani ni maisha, ajira, ustawi na uchumi; lazima itunzwe.
“Hakuna biashara bila amani, hakuna kufanya kazi bila amani, hakuna ajira bila amani, uchumi wa nchi na ustawi wa jamii vyote vinasababishwa na uwepo wa amani.
“Hivyo kijana wa kitanzania tambua amani yetu ndiyo maisha yetu, ajira zetu, ustawi wetu na uchumi wetu,” alisisitiza Dk. Jafo.
CHIKU ISSA
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Chiku Issa, alisema wanawake wa mkoa huo wanawajibu wa kulinda na kuimarisha amani ya nchi.
Alisema vurugu zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu, zimegharimu maisha ya watu na mali zao na kutia dosari kwa amani nchi, ziwe somo kwa kila mwananchi zisijirudie tena.
Chiku ambaye alikuwa akizungumza katika kikao cha baraza la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Arusha, alibainisha kuwa amani ya taifa huanzia katika familia.
“Mwanamke ni nguzo ya malezi na ustawi wa jamii, ninawakumbusha umuhimu wa kuwaandaa watoto kuwa na maadili, heshima na nidhamu,” alisema.
Chiku alisema kina mama wa zamani walikuwa wakimtazama mtoto mara moja tu, anaelewa na kujirekebisha makosa yake.
CECILIA PARESO
Cecilia Pareso ambaye ni mbunge wa viti maalumu mkoani Arusha, alisema wanawake wanatakiwa kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuimarisha amani ya nchi hatua itakayowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Niwaombe wanawake wenzangu tuungane kumsaidia Rais Dk. Samia kutimiza dhamira yake ya kutuachia Tanzania yenye tabasamu, kwa kuhubiri amani katika familia zetu,” alisema Cecilia.
JOSHUA NASSARI
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, alitoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo kulinda amani kwa nguvu zote.
Akizungumza na viongozi wa jadi, mila, dini, viongozi wa serikali na wananchi, chini ya mti aina ya mringaringa wa kabila la Wameru, Nassari alisema wamekutana katika eneo hilo kwa lengo la kuhubiri amani siyo vita.
“Hatutakubali mtu yeyote aturudishe tulikotoka. Sisi tutalinda amani ya eneo letu la Meru.Tumefika katika mti huu wa mila kutangaza amani, siyo vita dhidi ya mtu wala serikali,” alisema Nassari.
Nassari alikumbusha namna mgogoro wa kanisa uliowahi kutokea katika eneo lao na kusababisha mpasuko kiasi cha ndugu wa tumbo moja kushindwa kusalimiana hata kushirikiana katika shughuli za kifamilia.
“Mnakumbuka miongo mitatu iliyopita ilitokea vita na vurugu za kiimani ya kanisa moja. Hali hiyo ilitugawa, ilisababisha ndugu wa familia moja kushindwa kushirikiana, hata mtu akiwa na kipaimara cha mtoto wake anashindwa kumwambia ndugu yake, hali ile hatutakubali itokee tena Meru,”alisisitiza Nassari
Kwa mujibu Nassari, matukio ya vurugu za Oktoba 29 na 30, mwaka huu, zimeibua kumbukumbu chungu, na zimeonyesha umuhimu wa amani na umoja katika wilaya yao.
“Imetuchukua miongo mitatu kurudisha hali ya kukaa pamoja bila kujali dini, koo wala itikadi. Halafu wanakuja watu wanataka kuturudisha huko. Hapana, hatuwezi kukubali,” alisema Nassari.
YANIKI NDOINYO
Mbunge wa jimbo la Ngorongoro, Yaniki Ndoinyo alisema wilaya ya Ngongoro wamepitisha azimio la kulinda amani na kutojihusisha na maandamano yenye nia ovu ya kuvuruga amani ya nchi.
“Katika wilaya yetu tumeweka azimio la kudumu la kutoshiriki kwa namna yeyote ile mambo yatakayovuruga amani ya nchi yetu kwa sababu tunaamini maandamno siyo suluhisho la kushughulikia changamoto zinazotukabili,” alisema Ndoinyo
Kwa mujibu wa Ndoinyo, wananchi wa jimbo hilo wapo tayari kushirikiana na serikali kwa kuwa ndiyo yenye uwezo wa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.
“Sisi wananchi wa jimbo la Ngorongoro tumechagua amani na kukataa maandamano. Tunaamini changamoto zetu ikiwemo ya ukame ambayo tumeshaitolea taarifa, zinafanyiwa kazi kadri inavyowezekana awamu kwa awamu,” alisema Ndoinyo.
SARA MSAFIRI
Mbunge wa jimbo la Mvomero mkoani wa Morogoro, Sara Msafiri amewataka vijana kujiepusha na uvunjifu wa amani kwani kukosekana kwa amani kunarudisha nyuma maendeleo ya taifa.
Sarah alisema baadhi ya vijana wamekuwa na mihemko ambayo husababisha athari kwa taifa amewataka kuepuka na kulinda amani ya nchi.
ABUBAKAR ASENGA
Mbunge wa jimbo la Kilombero, Abubakar Asenga, amewataka wananchi kuiunga mkono serikali na kuacha kufuatilia mambo ya mitandaoni yanayochochea uvunjifu wa amani.
Asenga amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiwasikiliza watu ambao baadhi yao wako nje ya nchi wakihamasisha maandamano ambayo hayana tija kwa taifa.
Asenga alisema uvunjifu wa amani unarudisha nyuma maendeleo, ni vizuri kila mtu kuepuka viashiria vya uvunjifu wake.
RASHID SHANGAZI
Wabunge wa Mkoa wa Tanga, Twaha Mwakioja (Mkinga) na Rashid Shangazi (Mlalo), nao wametoa wito kwa vijana kuepuka vurugu na kutunza amani.
Wabunge hao wametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, walipozungumza kwa simu, wakisisitiza kuwa utulivu na subira ndiyo njia pekee ya kulinda uchumi na mustakabali wa nchi.
Mwakioja alibainisha kwamba amani ni urithi wa thamani, kitendo cha vijana kujihusisha na uvunjifu wake ni usaliti kwa jitihada za waasisi wa taifa.
Mwakioja aliwaonya vijana kuhusu athari za kupokea maelekezo ya kutoka kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa watu ambao yanapotokea machafuko hayawaathiri kwa kuwa hawapo nchini.
“Nawaasa vijana wenzangu epukeni kupokea maelekezo kutoka mitandaoni yanayoleta uchochezi na uharibifu wa taifa letu, mali zetu, biashara zetu na familia zetu,” alisema Mwakioja kwa msisitizo na kuongeza “Ili hali hao wanaotuchochea wapo nje ya nchi wakifurahia maisha mazuri ya amani na familia zao.”
Aliongeza kuwa vurugu inakimbiza uwekezaji na inawaumiza moja kwa moja vijana ambao wanahitaji ajira, huku akisisitiza wazingatie shughuli za uzalishaji mali badala ya vurugu.
Mbunge wa Mlalo Rashid Shangazi, alisisitiza umuhimu wa vijana kuzingatia mustakabali wa maisha yao, akitaja idadi yao kubwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022.
“Vijana mna kesho nyingi kuliko jamii nyingine,” alisema Shangazi na kuongeza, “ninawaasa kipindi hiki nchi ikiwa katika sitofahamu, ni vema mkazingatia tunu ya amani ambayo tumerithi kutoka kwa waasisi kupitia awamu mbalimbali.”
Shangazi alitaka Watanzania kuonesha ukomavu kwa kuipa nafasi tume iliyoundwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kufanya kazi yake ya uchunguzi wa kiini kilichosababisha matukio ya vurugu Oktoba 29, mwaka huu.
Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Katavi, Martha Maliki, alisema vijana wanapaswa kuendeleza tunu ya amani kwa kuhakikisha inakuwa msingi wa maisha bora.
“Msisitizo wa kutunza amani ni jambo linalopaswa kuzama katika mioyo, akili na mawazo ya kila raia wa Tanzania ,” alisema.
Mbunge wa Chemba (CCM), Kunti Majala aliwasisitiza Watanzania kulinda amani kwa kuwa ikitoweka madhara yake ni makubwa kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa jumla.
“Tuna Tanzania moja, hivyo ni muhimu kuilinda na kuitunza amani iliyopo kama mboni ya jicho. Amani ikitoweka itaathiri kila mtu,” alisema.
Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Jackson Kiswaga alisema kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha anakuwa mlinzi wa kwanza wa amani.
Kiswaga aliwasihi wananchi kutokubali kugawanyika kwa tofauti za kisasa, kidini na kikabila kwa lengo la kuligawa taifa.
“Mtaji wa kwanza wa maisha salama kwa kila Mtanzania ni amani, hivyo ni muhimu kuitunza na kuilinda,”alisisitiza Kiswaga.
Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini , Dickson Lutevele, aliwasihi vijana kutotumika vibaya na wasioitakia mema nchi. “Tuyasemee mema yanayofanywa na serikali na kuwalinda viongozi wetu,”alisema Lutevele.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Ritta Kabati, alisema kuna umuhimu kwa Watanzania kujivunia amani, kwa kuwa ikitoweka athari ni kubwa.




