Na NASRA KITANA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania ( TFF), kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Wakala wa Usafirishaji (Blueberry Travels) wameandaa mchakato wa kurahisisha usafiri wa mashabiki ambao watakwenda nchini Morocco kuiunga mkono Taifa Stars, katika mashindano ya Kombe la ataifa ya Afrika (AFCON 2025).
Fainali hizo zinatarajiwa kuanza kufanyika Desemba 21 hadi Januari 18, mwaka huu nchini Morocco ambapo Taifa Stars imepangwa kundi C ikiwa na timu za Uganda, Nigeria na Tunisia.
Stars ambayo ipo nchini Misri kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya mashindano ya hayo, itaanza kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Nigeria, unatarajiwa kufanyika Desemba 23, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Michezo wa BMT, Benson Chacha alisema mchakato huo, umefanyika baada ya kupokea barua na simu nyingi kutoka kwa mashabiki wakitaka kufahamu jinsi ambavyo watasafiri ili kuisapoti timu yao.
“Sisi BMT pamoja na TFF tumekuwa tukipokea barua na simu nyingi kutoka kwa mashabiki wakitaka kufahamu jinsi ya kusafiri kwa pamoja, tumefanya mchakato na kutafuta kampuni ya Blueberry ambayo itarahisisha mashabiki wengi kwenda Morocco kuishangilia Stars,” alisema Chacha.
Kwa upande wake Ofisa Masoko Blueberry Travel, Kelvin Charles alisema kuwa anaishukuru BMT na TFF kuwapa nafasi ya kuwapeleka Watanzania nchini Morocco kwa ajili ya kuishangilia Taifa Stars.
Alisema wameandaa vifurushi rafiki kwa kuangalia vipato vya Watanzania ambapo vitawasaidia kwenda na kurudi ikiwemo malazi na usafiri wa ndani wakiwa nchini humo.
“Kifurushi cha mchezo wa kwanza kati ya Tanzania dhidi ya Nigeria kwa mtu mmoja atalipa dola 2,535, wakati kwa watu wawili watalipa dola 2,320, kifurushi kingine ni ule mchezo wa Desemba 27 utakaoikutanisha Tanzania na Uganda mtu mmoja atalipa dola 2,970 wakiwa wawili watalipa dola 2,700.
“Pia mchezo wa Desemba 30, mwaka huu wa Stars dhidi ya Tunisia, mtu mmoja atalipa dola 3,000 kwa wawili ni dola 2,780 huku kwa upande kifurushi cha wale ambao wanataka kuangalia michezo yote watalipa dola 4,400 mtu mmoja itakuwa dola 5,250,” alisema Charles.
Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo alisema kikosi hicho kinaendelea vizuri na maandalizi kuhakikisha kinafanya vizuri katika mashindano hayo.
Alisema kila mchezaji yupo vizuri huku wale waliokuwa nje ya nchi wakiendelea kuripoti kambini kujiunga na wenzao.
“Timu yetu inaendelea vizuri malengo kufanya vyema katika michuano ya AFCON msimu huu,” alisema Ndimbo.




