Na MWANDISHI WETU
UONGOZI wa klabu ya Yanga umefungua mazungumzo na klabu ya Cr Belouizdad kwa ajili ya kuinasa saini ya mshambuliaji, Khanyisa Mayo.
Taarifa iliyopatikana kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo, imeeleza kuwa mchezaji huyo huenda akasajiliwa muda wowote katika kipindi cha dirisha dogo la usajili.
Kanyisa Mayo kwa sasa anaichezea timu ya Kaizer Ciefs ya Afrika Kusini ambapo amepelekwa huko kwa mkopo akitokea CR Belouizdad.
Chanzo cha habari kimeeleza kwamba mchezaji huyo kama atakubali ofa ya Yanga muda wowote akikutana na viongozi wa klabu hiyo atasaini mkataba wa kuvaa uzi wa njano na kijani.
Katika hatua nyingine, klabu za Mbeya City na Pamba FC bado zinaendelea kuwafuatilia baadhi ya wachezaji wa Yanga ili kuwasajili.
Timu hizo, zimeonesha nia ya kutaka kunasa saini ya kiungo Farid Mussa ambapo kila moja kivyake imeonesha nia hiyo.
Pia, timu za TRA United na KMC nazo zimeonesha nia ya kutaka kumsajili Denis Nkane kwa mkopo.
UHURU imemtafuta Rais wa klabu ya Yanga lakini juhudi za kumpata zilishindikana.




