IRENE MWASOMOLA Na DUSTAN NDUNGURU
BAADHI ya wakuu wa mikoa, wameeleza utayari wa serikali mikoani mwao kuhakikisha wanafunzi wanaanza masomo Januari 13, huku wakionya kukosekana kwa sare kusiwe kikwazo kwa mwanafunzi kufika shule kwa wakati.
Aidha, wameonya kutofumbiwa macho kwa mtumishi yeyote atakayejaribu kugeuza mtaji na kujiingizia fedha kupitia changamoto za wanafunzi wanaotarajiwa kuanza masomo.
Akizungumza na UHURU, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, alisema hadi wiki iliyopita zaidi ya asilimia 45 ya wanafunzi walikuwa wameandikishwa kujiunga darasa la kwanza na awali.
Senyamule alisema mkoa huo unatarajia kuwa na wanafunzi zaidi ya 45,000, ambao watajiunga na kidato cha kwanza katika mwaka huu wa masomo.
“Kwa kidato cha kwanza zaidi ya watoto 45,000 hawa wote wanatakiwa kufika shule, tumetoa tahadhari kwa wazazi na walezi kwa watoto watakao chelewa tutachukua hatua za kisheria kwa mzazi au mlezi wake,” alisema.
Kwa mujibu wa Senyamule, hakuna sababu ya mtoto kutofika shule kwa kuwa serikali inatoa elimu bila malipo na kila mzazi alipata muda mzuri wa kujiandaa kwa kuwa taarifa za mtoto kujiunga kidato cha kwanza zilitolewa mapema.
Aidha, alisema serikali ya mkoa imechukua hatua ya kuziandikia barua taasisi binafsi na dini, kuendelea kuwakumbusha wazazi na walezi kuhakikisha wana wapeleka watoto shule.
Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa Dodoma inaendelea kutoa kipaumbele namba moja kwa sekta ya elimu hususan suala la ufaulu na kudhibiti utoro.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani, alisema maandalizi ya miundombinu na maeneo mengine yanayohusu kufanikisha wanafunzi wanasoma vizuri katika mkoa huo,yako tayari.
Hata hivyo, alionya baadhi ya shule kuacha kuweka ulazima kwa wazazi kununua sare shuleni.
Alisema wapo baadhi ya walimu wamefanya miradi hiyo kuwa ya kwao na kusababisha wafanya biashara wengine ambao wanalipa kodi kwa kazi hizo kukosa wateja.
“Kuna malalamiko kwa baadhi ya shule kuweka kipengele cha lazima wanafunzi kununua sare shuleni, tuhakikishe mzazi anapewa uhuru kwani kuna wafadhili pia wanatoa sare kwa watoto,” alielekeza.
Dk. Batilda aliwataka wazazi na walezi kutoacha kuwapeleka watoto shule kwa kigezo cha kukosa sare.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, aliwataka wazazi na walezi mkoani humo kuhakikisha wanawaandalia wanafunzi mahitaji muhimu shule zitakapofunguliwa wiki ijayo wafike kwa wakati bila vikwazo.
Kanali Abbas aliyasema hayo juzi, baada ya kufanya ziara ya kukagua ukamilishaji wa ujenzi na maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa shule ya sekondari Amali Ruvuma juu iliyopo katika Manispaa ya Songea.
Mkuu wa mkoa huyo alisema dhamira ya serikali kuanzisha shule za amali, ni kuwasaidia vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.
“Niwaombe sana hakikisheni mnakamilisha kazi za ujenzi zilizobakia kwa wakati kabla shule kufunguliwa nisingependa kuona wanafunzi wapo darasani mafundi nao wapo humo humo wanafanyakazi kwa kuwa huo utakuwa usumbufu kwa wanafunzi ambao wakifika hapa wanapaswa kujikita katika masomo bila shida,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, alisema mkoa huo unatarajia kuandikisha wanafunzi wa elimu ya msingi 65,670, kati yao wavulana ni 33,530 na wasichana 32,440.
Pia, alisema mkoa huo unatarajia kuwa na wanafunzi wa awali 68,162.
Vilevile Sendiga alisema maandalizi ya kupokea wanafunzi yamekamilika ikiwamo, uwepo wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, mabweni, maabara na miundombinu mingine ya kujinza na kujifunzia.
“Tunatarajia watoto hawa wataripoti hapa, tunaendelea na zoezi la kusajili kidijitali tutapata ‘data’ (takwimu) nyingine kamili baada ya watoto kufika shule,” alisema.
Aidha Sendiga alisema Mkoa huo umejipanga vyema na una walimu wa kutosha kufundisha masomo yote.




