Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ametaja sababu za kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri hususan kumbadilishia majukumu Waziri Profesa Palamagamba Kabudi amsaidie kipindi hiki kuendana na mabadiliko ya siasa za dunia zenye mtazamo chanya na hasi kwa Tanzania.
Pia, amewateua Makamu wa Rais Mstaafu Dk. Philip Mpango kuwa mshauri katika Uchumi na Miradi na Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa kuwa mshauri wake mambo ya jamii.
Rais Dk. Samia aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na wanamichezo mbalimbali wakiwemo wachezaji wa Taifa Stars kuwapongeza kwa kufanya vizuri katika mashindano ya AFCON yaliyofanyika nchini Morocco.
“Jambo lingine ambalo limeingia katika shughuli ya leo ni kumuaga Profesa Palamagamba Kabudi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuja kwangu Ikulu . Imekuwa mapema kubadilisha kwasababu ya kwendana na siasa za dunia zinavyokwenda zenye mtazamo chanya na hasi kwa Tanzania.
“Pale Ikulu, nahitaji akili iliyopevuka yenye maarifa mapana, uzoefu mkubwa na mtu ambaye yuko vizuri katika kujieleza na kueleza jambo likaeleweka. Nimepiga picha serikalini kwangu kote, nikasema Profesa Kabudi atanifaa, hivyo wale washauri wangu wengine wanahitaji mtu mtulivu atakayeweza kudili nao,”alisema.
Ameeleza kuwa, viongozi wengine ambao ni wa umri wa watoto wake wanaweza wasiwe na majibu mazuri lakini kwa uwezo wa Profesa Kabudi, anaweza kufanya vizuri katika nafasi hiyo. “Kwahiyo hizo ndiyo sababu zilizosababisha nimchague Profesa Kabudi aje ofisini kwangu Ikulu anisaidie kazi,”alieleza.
Vile vile Rais Dk. Samia amesisitiza umoja na mshikamano kwa Taifa kuendeleza uzalendo ambao ni msingi wa maendeleo nchini.
Pia, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya vizuri katika nyanja za kimataifa na kupata vikombe vitano huku akipokea vikombe vitatu kikiwemo cha Tanzania kuwa nchi bora kwa Utalii Afrika na Duniani na kingine cha hifadhi ya Serengeti, kingine ni Zanzibar kutambulika kuwa sehemu nzuri ya mikutano ya utalii na Hoteli bora ya Utalii Tanzania ikiwa ni sifa nzuri kwa Taifa.
Kuhusu amani, Rais Dk. Samia amesisitiza “Kwa wale wanaotaka kutuvurugia kuchafua sifa yetu washindwe na walegee, Tanzania itaendelea kuwa kitovu cha amani, haya tuliyoshinda tuendelee kushinda hata huko mbele,”alisisitiza.
Awali, Waziri Profesa Kabudi amesisitiza uzalendo wa kulipenda Taifa na kuimarisha maadili mema ya Kitanzania.
Amempongeza Rais Dk. Samia kwa kuongoza vyema na kuliunganisha taifa kupitia farsafa yake ya 4R ambayo imekuwa na tija kubwa kuwaunganisha watanzania na kuchochea maendeleo.
Amesema watanzania wazalendo wanasisitiza umoja wa kitanzania siyo mbadala wake, kuiheshimu Tanzania kama mama kwani hakuna nyingine.




