MANCHESTER, England
MKONGWE Wayne Rooney, amesema yupo tayari kurejea kuongeza nguvu katika benchi la ufundi la klabu hiyo kama Michael Carrick atafanikiwa kuteuliwa kuwa kocha wa kikosi hicho.
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England, alishacheza pamoja na Rooney ambapo yupo katika rada za kukabidhiwa timu hadi mwishoni mwa msimu huu.
Uongozi wa Manchester United ulimfuta kazi hivi karibuni aliyekuwa kocha Ruben Amorim kutokana na mwenendo mbovu wa matokeo msimu huu.
Hivi sasa uongozi wa klabu hiyo unahaha kutafuta kocha mpya kwa ajili ya kuendelea alipoishia Amorim hadi mwishoni mwa msimu huu.
Vilevile, kiungo wa zamani raia wa Scotland, Darren Fletcher, aliyewahi kucheza pamoja na Rooney ndani ya United, hivi sasa amepewa timu kwa muda.
Taarifa kutoka katika mtandao wa klabu, zinasema huenda Carrick akaanza kukonoa kikosi hicho kitakaporejea mazoezini leo.
Rooney alisema kuwa yupo tayari kushirikiana na Carrick kama atatangazwa kuwa kocha wa kikosi hicho.
Alisema Carrick ni mmoja wa watu wanaofaa kuingoza United kwani alishacheza muda mrefu na kuipatia mafanikio makubwa.
Alisema hivi sasa wanatakiwa watu wanaoijua timu hiyo kiundani kuhakikisha wanaiongoza na kurejesha matumaini yaliyopotea kwa mashabiki na wadau wa United.
“Carrick ndiye mtu anayeweza kurejesha matumaini ndani ya kikosi cha Manchester United hivi sasa, nipo tayari kushirikiana naye kuhakikisha timu inarejea katika ubora wake.
“Wanaotakiwa kuiongoza United hivi sasa ni watu kama Darren Fletcher, John O’Shea, Carrick au mimi ambao tunaitambua timu kwa kiasi kikubwa na kuhakikisha inarejesha makali yake katika msimu huu.
“Timu imeshapoteza imani kwa mashabiki inatakiwa kufanyika kazi ya ziada kuhakikisha inarejesha matumaini kwa mashabiki na familia za mpira,” alisema.
Katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, hivi sasa Manchester United ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 21 msimu huu.
(BBC)




