Na MWANDISHI WETU
MSANII nyota wa singeli, Meja Kunta, amesema mwaka huu amejipanga kuhakikisha anawapa sapoti kubwa wasanii wachanga kutimiza ndoto zao.
Nyota huyo amewahi kuwika na nyimbo mbalimbali zikiwemo Mamu, Kidimbwi, Madanga ya Mke Wangu, Wafoo, Sina, Tabia Mbaya na Chura Superstar.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Meja Kunta alisema amefanya kazi kubwa ndani na nje ya nchi, lakini sasa amejipanga kuwaunga mkono wasanii chipukizi.
Meja Kunta alisema hatua hiyo imekuja ili kuhakikisha wasanii chipukizi wanatimiza ndoto za kuwa wasanii wakubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
“Nimebarikiwa kufanya kazi kubwa ndani na nje ya Tanzania.Lakini mwaka huu nimechagua kuwa sehemu ya safari ya wasanii wanaohitaji msaada, ili wakue na kusimama imara,” alisema.
Nyota huyo amewaomba Watanzania kuwaunga mkono wasanii chipukizi kuhakikisha muziki huo unasonga mbele.
Katika kulithibitisha hilo, mkali huyo wa miondoko ya singeli ladha, ameuanza mwaka kwa kushirikishwa katika wimbo unaoitwa Maumivu aliouimba na msanii chipukizi, Don Breeze.




