Na ATHNATH MKIRAMWENI
TANZANIA imeingia katika orodha ya nchi 10 bora zinazovutia zaidi kwa uwekezaji barani Afrika, ikishika nafasi ya tisa, yakiwa matokeo ya mageuzi makubwa ya kisera yaliyofanywa na serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, katika mkutano na wawekezaji wa kimkakati, jijini Dar es Salaam, jana.
TAKWIMU
Kupitia mkutano huo ulioratibiwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA), waziri huyo alitoa takwimu zinazoonesha kukua kwa kiwango cha uwekezaji nchini na kusema mwaka 2021 nchi ilisajili jumla ya miradi 256 pekee, wakati mwaka 2025 idadi ilipanda hadi kufikia miradi 915.
Profesa Mkumbo alisema thamani ya uwekezaji imepanda kutoka chini ya dola za Marekani bilioni tatu mwaka 2021, hadi dola bilioni 11 mwaka jana.
WAZAWA
Katika hatua nyingine, Waziri Mkumbo aliwataka Watanzania kuacha tabia ya ‘kukodisha majina yao’ kwa wawekezaji wa kigeni kwa malipo madogo kufanikisha uwekezaji.
Alisema kitendo hicho kinadhoofisha azma ya serikali ya kuhakikisha wazawa wanamiliki uchumi wa nchi yao.
Profesa Mkumbo alifichua mbinu inayotumiwa na baadhi ya wawekezaji wageni kukwepa sheria zinazowataka kushirikiana na wazawa na kusema, baadhi ya Watanzania wamekuwa wakikubali kuandikwa kama wamiliki wa hisa
kwa mfano wa asilimia 30 kwa kupewa kiasi kidogo cha fedha, wakati kiuhalisia hawana uamuzi wala umiliki wowote.
Profesa Mkumbo alibainisha kuwa, wazawa wengi wanashindwa kukua kibiashara kwa sababu hawajui fursa na vivutio vinavyotolewa na serikali, tofauti na wawekezaji wa kigeni ambao hufanya utafiti kabla ya kuingia nchini.
Kutokana na hali hiyo, Profesa Mkumbo aliiagiza TISEZA kuzunguka nchi nzima kutoa elimu kwa wazawa kuhusu fursa, mazingira ya biashara, na vivutio vinavyopatikana kuwajengea ujasiri wa kuwekeza na kutengeneza ajira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri alisema mamlaka hiyo imejiwekea lengo la kuvutia na kusajili miradi isiyopungua 1,500 katika kipindi kijacho.
Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero, Victor Byemelwa aliipongeza serikali kupitia TISEZA kwa kuendelea kushughulikia changamoto za wawekezaji na kuboresha mazingira ya biashara nchini.




