RABAT, Morocco
NYOTA Sadio Mane juzi aligeuka kuwa shujaa wa Senegal baada ya kuwaongoza Simba hao wa Teranga, kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Mane aliiongoza miamba hiyo juzi katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat, Morocco wakati Senegal ikishinda 1-0.
Licha ya bao la ushindi kufungwa na kiungo Pape Gueye, lakini kitendo cha Mane kuwaongoza wenzake kumaliza mchezo huo ni sababu tosha ya kuwa shujaa wa kweli wa miamba hiyo.
Mane alionyesha ukongwe, nidhamu na ustaarabu wake katika dakika za nyongeza kipindi cha pili wakati nyota wenzake walipogomea mechi na wengine kurejea vyumbani kufuatia kupinga uamuzi wa refa Jean-Jacques Ndala wa kuizawadia penalti Morocco.
Morocco ilipata penalti hiyo kufuatia staa wake, Brahim Diaz kuanguka baada ya kuvutwa na beki Malick Diouf ndani ya eneo la hatari wakati wa kona, ambapo Senegal walipinga kwa kudai haikupaswa kuwa penalti.
Baada ya dakika kadhaa za kubishana huku nyota wa Senegal wakiongozwa na kocha Pape Thiaw kugoma kuendelea na mchezo, Mane aliwaamuru wenzake warejee uwanjani hatua ambayo iliwafanya kumtii na kuiruhusu Morocco kupiga penalti.
Hata hivyo, Morocco ilikosa mkwaju huo kufuatia kipa Edouard Mendy penalti ya Diaz aliyepiga katikati mwa goli kipa huyo.
Baada ya mechi hiyo kwenda katika dakika 30 za nyongeza, Gueye aliiandikia bao Senegal dakika ya 94, akiweka mpira kimiani kwa shuti kali na kuipa ubingwa wa pili Senegal baada ya mwaka 2021 kufanya hivyo kwa mara ya kwanza.
Mane alisema michuano ya mwaka huu ndiyo itakuwa AFCON yake ya mwisho kukipiga Senegal.
“Mpira wa miguu ni kitu fulani cha kipekee sana, dunia ilikuwa inatazama, dunia inaupenda mpira na nafikiri mpira ni starehe hivyo tunapaswa kuonyesha taswira nzuri juu ya mpira.
Nafikiri kingekuwa kitendo cha ajabu kama tusingecheza hii mechi kwa sababu mwamuzi ametoa penalti. Nafikiri hiko kingekuwa kitendo cha ajabu sana hususan katika mpira wa Afrika, ni bora ningepoteza mechi kuliko kitendo kama hicho kitokee katika mpira wetu,” alisema Mane.
Mchezaji wa zamani wa Nigeria, Daniel Amokachi aliiambia BBC: “Mane alikwenda mbali zaidi kuirudisha timu mchezoni na imemlipa,”.
Mchezaji wa zamani wa Morocco, Hassan Kachloul alisema “Mpira wa Afrika na mpira wa dunia ulikuwa unapoteza hadi pale Mane alipoingilia. Kitu ambacho nilipenda zaidi ni kwamba, mchezaji pekeee kutoka Senegal (aliyewarudisha wenzie uwanjani) alikuwa Sadio Mane. Hii inaonyesha ubora wa mtu huyu,”.
MANE MCHEZAJI BORA AFCON
Baada ya mchezo huo, Mane alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Katika michuano hiyo, Mane anayekipiga klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia, ameifungia Senegal mabao mawili na kutoa pasi tatu za mabao katika mechi saba za kombe hilo msimu huu.
DIAZ, BONO
Pia, mshambuliaji wa Morocco, Diaz alitangazwa kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo baada ya kufunga mabao matano katika mechi saba.
Aidha, kipa wa Morocco, Yassine Bounou ameshinda tuzo ya kipa bora wa mashindano hayo baada ya kuonyesha kiwango bora kuanzia mechi ya kwanza hadi fainali.
CAF YALAANI
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limelaani vitendo visivyo vya kiungwana vilivyoonyeshwa na baadhi ya wachezaji na viongozi katika fainali hiyo.
“CAF inapitia upya vipande vyote vya picha mjongeo na itapeleka suala hilo katika bodi zake kuhakikisha uamuzi sahihi unachokuliwa kwa watakaokutwa na hatia,” ilisema taarifa ya CAF.
KOCHA SENEGAL AOMBA RADHI
Kocha wa Senegal, Thiaw, ameomba radhi kwa kitendo cha kuwaamuru wachezaji wake kugomea kuendelea na mechi wakati Morocco ilipozawadiwa penalti.
Kitendo hicho kilisababisha mechi hiyo kutoendelea kwa zaidi ya dakika 17.
“Hatukubali (uamuzi wa refa). Ninaomba radhi kwa ajili ya mpira wa miguu. Hatukupaswa kufanya vile lakini tulishafanya na sasa tunaomba radhi,” alisema Thiaw, 44 alipozungumza na BeIN Sport.




