Na MWANDISHI WETU
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, katika kikao chake kilichofanyika jana Zanzibar, pamoja na mambo mengine, imepitia, kujadili na kufanya uteuzi wa wagombea uongozi wa CCM wanaotokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kutiwa saini na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, ilisema, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa wanaotokana na Bunge kutoka Tanzania Bara nafasi tatu ambao ni Paul Christian Makonda, Livingstone Joseph Lusinde na Asia Abdulkarim Halanga.
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa wanaotokana na Bunge kutoka Zanzibar, walioteuliwa ni Khamis Mussa Omar na Tauhida Cassian Galos.
Pia, katibu wa wabunge wote wa CCM, ameteuliwa Agnes Elias Hokororo.
Wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wameteuliwa watatu ambao ni Najma Murtaza Giga, Deodatus Philipo Mwanyika na Cecilia Daniel Pareso
Aidha, Kamati Kuu ya Halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, pia imefanya uteuzi wa wagombea uongozi wa CCM wanaotokana na Baraza la Wawakilishi ambao ni Said Ali Juma, Hamza Hassan Juma na Lela Muhamed Mussa.
Wawakilishi wa CCM watakaoingia bungeni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Bakar Hamad Bakar, Dk. Shaame Ali Ali, Simai Mohammed Said na Fatma Ramadhan Mandoba.
Katibu wa Wawakilishi wote wa CCM, ameteuliwa Machano Othman Said huku wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi ni Mahmoud Omar Hamad na Hudhaima Mbarak Tahir
UCHAGUZI MDOGO PERAMIHO
Kuhusu mchakato wa uchaguzi wa ubunge, Jimbo la Peramiho,
kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 105 (7)(f) ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 Toleo la Julai 2025, Kamati Kuu imefanya uteuzi wa Dk. Lazaro Killian Kombakuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho, lililopo Wilaya ya Songea Vijijini.




