Na MWANDISHI WETU
KOCHA Amri Said ametaja mbinu tatu za kuhakikisha timu za Yanga na Simba zinashinda mechi zijazo za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza UHURU jijini Dar es Salaam, Said maarufu kwa jina la ‘Jap Stam ‘alisema Yanga na Simba zina wachezaji wazuri wenye uwezo wa kupindua meza.
“Timu zipo vizuri lakini kuna changamoto kadhaa ambazo zikifanyiwa kazi na makocha ushindi unapatikana,”alisema.
Amri Said ambaye aliwahi kuichezea Simba kwa mafanikio makubwa, alisema timu hizo zikiimarisha sehemu ya ulinzi na ushambuliaji mambo yatakauwa mazuri.
Alisema jambo jingine la pili ni kuhakikisha mashabiki wanawapa sapoti ya kutosha ili ziweze kushinda.
Sababu nyingi alisema ni vyema wachezaji wote wa timu hizo wakacheza kwa tahadhari kutokana na mbinu za timu za ukanda wa Kaskazini mwa Afrika kuwa wajanja wa kupoteza muda na kuwatafutia kadi wachezaji wa timu pinzani.
Yanga inatarajiwa kucheza na Al Ahly visiwani Zanzibar huku Simba nayo ikicheza na timu ya Esperance Tunis jijini Dar es Salaam.
YANGA
Akizungumzia kuhusu kikosi cha Yanga, Amri Saidi alisema timu hiyo ilicheza vizuri kulingana na mpango wa kocha , Pedro Goncalves.
“Unajua ule mchezo ulikuwa na hesabu mbili za kulinda na kushambulia kwa kushtukiza, walicheza vizuri,”alisema.
Beki huyo wa zamani wa Simba alisema kasoro ilikuwa kuna muda walinzi wa Yanga walijisahau kuwahi kurudi nyuma kuziba nafasi ambazo wachezaji wa Al Ahly walitumia vizuri kupata ushindi.
“Angalia bao la kwanza lilifungwa kutokana na beki mmoja wa Yanga kushindwa kuondoa mpira kwa kichwa ambapo mchezaji wa Al Ahly alitumia nafasi kufunga,” alisema.
Kocha huyo alisema bao la pili lilitokana na kosa la mchezaji moja kutoa mpira kwa mchezaji wa Al Ahly kitu ambacho kilisababisha timu hiyo ya Misri kupata bao la pili.
“Naamini makocha wa Yanga wameona kasoro hizo , najua watazifanyia kazi na kisha kusuka wembe wa pale mbele mipira ikija waitumie kuwaadhibu Al Ahly katika mchezo ujao, wanafungika wale,” alisema.
Hata hivyo, Amri Saidi alimsifu kocha wa Yanga kwa jinsi alivyopanga kikosi na kutengeneza nafasi nyingi kama washambuliaji wangekuwa makini timu hiyo ingerudi nchini na ushindi.
“Wachezaji wa Yanga walitengeneza nafasi kadhaa, lakini walikosa mabao, angalia Al Ahly ina wachezaji bora na wana uwezo wa kubadili matokeo muda wowote, walitumia makosa ya wachezaji wa Yanga kushinda mchezo huo,” alisema.
Alisema Yanga ina kazi kubwa kutokana na Al Ahly kuundwa na nyota wenye viwango vikubwa huku wengine wakitoka timu za Barani Ulaya.
“’Quality’ ya wachezaji wa Ahly ni kubwa, lakini wachezaji wa Yanga walipata nafasi nyingi wakashindwa kuzitumia, wenzao walipata nafasi chache wakapata ushindi,ni imani yangu Yanga wakitulia na kujipanga kuondoa kasoro hizo, watashinda mchezo ujao,” alisema Amri.
SIMBA
Kocha Amri Saidi alisema wachezaji wa Simba walicheza vizuri walikuwa na ubora, lakini shida ilikuwa sehemu ya kiungo, ilishindwa muda mwingine kuunganisha mipira kufika lango la Esperance.
“Washambuliaji wa Simba walipoteza nafasi kadhaa kupachika mabao, kuna wakati walipata nafasi wakapoteza,” alisema.
Hata hivyo, kocha huyo alishauri benchi la ufundi la Simba kufanya marekebisho upande wa ushambuliaji.
“Nasema bado Simb a inatakiwa kuwa na mshambuliji wa kupachika mabao, kwani nimejaribu kuangalia pale namba tisa na 10, hakuna mtu wa kusumbua sana, walinzi wa timu pinzani,”alisema.
Hata hivyo, kocha huyo aliusifu uongozi wa Simba kwa kuongeza nguvu katika kikosi chao.
“Nimeona baadhi ya wachezaji waliosajiliwa hivi karibuni wameonesha uwezo mkubwa,.Chama alifanya kazi nzuri yak ugawa mipira mbele lakini ilikuwa inapotea,” alisema Amri Said.
Pia, kocha huyo alipendekeza makocha wa Simba inabidi wafanyie kazi sehemu ya walinzi wa timu hiyo kuhakikisha wanacheza mipira ya krosi inayopigwa na timu pinzani ili lango liwe salama.




