Na SUPERIUS ERNEST
JANUARI 27, ndiyo siku maalumu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa kwa namna mbalimbali na wananchi wa Tanzania, wakijumuika na Rais Dk. Samia kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya.
Kwa miaka kadhaa sasa, Rais Dk. Samia amekuwa akiitumia siku yake ya kuzaliwa, kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaenddeleo ikiwemo uzinduzi wa miradi.
Katika kumbukizi ya mwaka huu, ambayo inafanyika leo, kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema Rais Dk. Samia ataadhimisha siku hiyo kwa upandaji wa miti ikiwa ni dhamira yake ya kuhamasisha utunzaji mazingira.
Ikumbukwe Rais Dk. Samia ni kinara wa nishati safi ya kupikia kimataifa, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha upandaji miti nchini kote na kuepusha kukata miti kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kauli mbiu ya upandaji miti ni: “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti. Tuna wajibu wa pamoja wa kulinda mazingira. Panda mti sasa, ni alama ya uzalendo.”
Pia, kampeni hiyo ya upandaji wa miti inasisitiza kuwa siku ya leo kila mwananchi aianza kwa upandaji miti, kwani utalinda vyanzo vya maji, utaimarisha uoto wa asili na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia kampeni hiyo, kila mwananchi aelewe hatua ya upandaji wa mti leo, inalinda maisha ya kesho.
Ni vyema wananchi wakamuunga mkono Rais Dk. Samia katika siku yake hiyo ya kuzaliwa kwa kutunza mazingira kwa upandaji miti.
Njia bora ya kumuunga mkono ni kwa kupanda mti sehemu uliyopo, kuupiga picha na kuchapisha mtandaoni, iwe hamasa kwa wengine kufanya hivyo hata baada ya siku hiyo.
Katika hotuba zake mbalimbali, Rais Dk. Samia, amekua akihamasisha utunzaji mazingira, kwani inasaida kuepuka athari mbalimbali ikiwemo mmomonyoko wa udongo.
Pia miti inasaidia kutoa kivuli kwa wananchi hata watoto wakiwemo wanafunzi wanapokuwa mashuleni au wanapocheza mitaani.
Kupitia kampeni hiyo, Rais Dk. Samia amekuwa akisisitiza kupanda miti ya matunda ambayo inakuwa na tija zaidi kuliko kupanda miti isiyo na faida.
Kwa mfano, upandaji wa miti ya miembe, mipeasi, mifenesi, parachichi na mingine kama hiyo yenye faida.
Kila mwananchi ana kila sababu ya kuunga mkono kampeni hiyo lenye tija, lengo la kuifanya nchi kuwa kijani.
Miti isipopadwa, mazingira yatakuwa ya ukavu na ukame, yasiyovutia, ni vyema kuhakikisha zoezi la upandaji wa miti linakuwa la jamii yote.
UVCCM WAMUUNGA MKONO
Akizungumzia kumuunga mkono Rais Dk. Samia, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohamed Kawaida, alimtakia heri Rais Dk. Samia katika siku yake ya kuzaliwa kwa niaba ya vijana wote nchini.
“Januari 27 ndiyo siku aliyozaliwa Rais Dk. Samia, tunamtakia heri, katika siku yake hii adhimu ya kumbukumbu ya kuzaliwa na tunampongeza sana sana katika siku yake ya kuongeza mwaka, tutaendelea kuwa pamoja naye wakati wote,” alisema.
Alisema vijana wako tayari kumuunga mkono katika kusherehekea siku hiyo adhimu ya kuzaliwa kwa upandaji wa miti wakiungana na taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF), kupanda miti na kuchangia damu.
Alieleza kuwa shughuli hizo muhimu zitafanyika visiwani Zanzibar Mwaisala, Bungi na Kizimkazi ambapo Januari 26 jana ilifanyika kazi ya uchangiaji damu na leo kupanda miti.
Kawaida alisema Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa kwa vijana kwa kuwateua katika nafasi mbalimbali za uongozi jambo ambalo limeendelea kuwapa imani kubwa juu ya serikali yao.
Alisema vijana wana imani kubwa kwa serikali yao, wanamhakikishia wataendelea kumuunga mkono Rais Dk. Samia kwa nguvu zote katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Rais wetu Dk. Samia afahamu kuwa vijana tuko mikono salama, tuna imani naye, tutaendelea kumuunga mkono wakati wote na kulijenga na kulitumikia Taifa usiku na mchana,”alisema.
Alieleza kuwa Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa ya kuchochea miradi ya maendeleo mikubwa na y a kimkakati, jambo ambalo limeendelea kuchochea ukuaji uchumi.
Aliwasisitiza vijana kujituma na kujitoa katika kulitimikia taifa, kwani mafanikio hayafikiwi kwa wepesi isipokuwa kwa kujitolea na kuvumilia maumivu.
Kawaida alisema Katiba ya CCM imeeleza umuhimu wa elimu na wajibu wa kijana katika kuipata elimu, huku akiwataka kuongeza juhudi zaidi.
Aliwahimiza kushirikiana kwa pamoja, kubadilishana mawazo na wengine, kuzingatia utiifu, uzalendo na nidhamu.
Alisema UVCCM, imeendelea kuhakikisha vijana wanapata na kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo na zinazojitokeza kutoka serikalini.
Aliwasisitiza vijana kujiunga na matawi ya UVCCM yaliyopo katika vyuo mbalimbali nchini.




