Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kilichotokea usiku wa tarehe 19 Februari, 2026, katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imesema “Rais Dk. Samia anamkumbuka Kardinali Pengo kama kiongozi wa kiroho na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani, maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa, kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki.
Ameongeza kuwa, Taifa limepoteza kiongozi aliyelitumikia kwa uadilifu na kujitolea, na kwamba mchango wake katika malezi ya kiroho na maadili utaendelea kukumbukwa, kuthaminiwa na kuenziwa.
Rais Dk. Samia ametuma salamu za rambirambi kwa Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, OFMCap – Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam; Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), viongozi wa dini, pamoja na waumini wote walioguswa na msiba huu mzito.
Aidha, Rais Dk. Samia ameungana na Kanisa, waumini na Watanzania wote kwa ujumla katika kipindi hiki cha majonzi, na anamuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.





