Na ELIZABETH JOHN
SERIKALI imesisitiza dhamira yake ya kuifanya sekta ya madini kuwa injini kuu ya ukuaji uchumi wa taifa, kwa kuimarisha upatikanaji mitaji na kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, aliyasema hayo katika hafla ya utiaji saini kati ya Benki ya CRDB, wachimbaji wadogo na Tume ya Madini, iliyofanyika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Mavunde aliipongeza CRDB kushirikiana na Tume ya Madini, akisema mpango huo ni hatua ya kihistoria itakayobadili mfumo wa upatikanaji mitaji katika sekta ya madini nchini.
Mavunde alisema katika hatua ya kihistoria, kikundi cha wachimbaji wadogo Songwe Gold Family kitakuwa cha kwanza kupata mkopo sh. bilioni 50 kwa wakati mmoja.
Pia, alisema serikali ipo katika hatua za mwisho kuanzisha Mfuko wa Dhamana kukopesha wachimbaji wadogo kupunguza vikwazo vya patikanaji mitaji na kuongeza kasi ya urasimishaji wa shughuli za uchimbaji.
Alisema sekta ya madini, imeendelea kukua kwa kasi, ikichangia asilimia 10 ya Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 56 ya mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya nje yanayozidi dola za Marekani bilioni tano kwa mwaka.
Alisema mafanikio hayo, yanatokana na mageuzi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha dhamira na utayari mkubwa wa kuikuza sekta ya madini.
Alisema katika miaka ya karibuni, yameshuhudiwa mabadiliko makubwa ya kiuwekezaji yatakayoongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.
“Tunachokishuhudia leo ni daraja linalounganisha maono ya serikali na nguvu ya mtaji kutoka sekta ya fedha.
“Ushirikiano huu, unaenda moja kwa moja kumgusa mchimbaji mdogo na kumwinua katika uchumi rasmi,” alisema.
Mavunde alisisitiza chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali imeendelea kutekeleza mageuzi ya kisera, kiusimamizi na kisheria, kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania wengi.
Alieleza azma ya serikali ni kuona uchimbaji hauishii kuuza madini ghafi pekee, isipokuwa kuongeza hadi uchakataji na uongezaji thamani ndani ya nchi kuongeza ajira, mapato ya taifa na ushindani wa Tanzania kimataifa.
Aidha, aliwataka wadau wa sekta hiyo, kuendelea kushirikiana kwa karibu kuongeza thamani ya madini nchini, kuongeza ajira na kukuza mapato ya taifa.
Alisisitiza mpango huo wa CRDB, unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wa dhamana zinazotokana moja kwa moja na shughuli za uchimbaji, ikiwa ni pamoja na leseni halali za uchimbaji, mikataba ya mauzo ya dhahabu na akiba iliyohifadhiwa katika viwanda vya kusafisha.
TUME YA MADINI
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, alisema wachimbaji wadogo wanachangia hadi asilimia 40 ya mapato yote ya sekta ya madini, hatua aliyoitaja kuwa ni mafanikio makubwa, ikilinganishwa na awali kabla ya kurasimishwa kwa mifumo ya masoko na vituo vya ununuzi wa madini, ilikuwa asilimia nne.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo, ushirikiano huo, utasaidia kuongeza manufaa kwa wadau wote wa mnyororo wa thamani wa madini, wakiwemo watoa huduma na wafanyabiashara, sambamba na kuchochea ajira na kuboresha viwango vya maisha kwa wananchi wanaotegemea shughuli za uchimbaji.
Alisisitiza kuwa, mpango huo utaimarisha uchimbaji salama na utunzaji mazingira kupitia matumizi sahihi ya teknolojia na mifumo rasmi, huku akiipongeza benki ya CRDB kwa hatua yake ya kuimarisha ushirikiano na Tume ya Madini katika kutatua changamoto za kifedha kwa wachimbaji wadogo.
VIONGOZI CRDB
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB, Dk. Donald Mmari, alisema benki hiyo, imejipanga kushiriki kikamilifu kuharakisha mageuzi ya sekta ya madini kwa kubuni huduma za kifedha zitakazokidhi mahitaji ya wadau wakubwa na wadogo wa sekta hiyo nchini.
Alisema pamoja na utajiri mkubwa wa rasilimali madini ambayo Tanzania imebarikiwa nayo, sekta hiyo ina mchango mkubwa zaidi, ikiwemo kuchochea ujenzi wa miundombinu muhimu kama barabara, reli, bandari na nishati ya umeme, hali inayochochea ukuaji wa uchumi kwa upana wake.
Makamu mwenyekiti huyo, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia, kuendelea kufanya mageuzi makubwa ya kisera na kisheria yaliyoongeza uwazi, kuimarisha uwekezaji na kusisitiza uongezaji thamani wa madini nchini, hatua alizosema zimeiweka sekta hiyo katika nafasi ya kimkakati ya kuleta mageuzi ya kiuchumi.
Aidha, alisema benki imeweka kipaumbele kuwawezesha wajasiriamali wadogo na kati wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini ili kuimarisha uchumi jumuishi, kupanua upatikanaji wa mitaji nafuu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia salama na bora.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema benki hiyo, imeweka mkakati maalumu wa kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyowakabili wachimbaji wadogo wa madini, ikiwa ni sehemu ya kuleta mapinduzi ya kweli katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.
Alieleza CRDB imeendelea kuwa benki bora kutokana na kuaminiwa na Watanzania, akaahidi kuimarisha zaidi huduma zake.
Alifafanua kuwa, sekta ya madini imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa kwa miaka mingi, lakini wachimbaji wadogo wameendelea kukosa mitaji rasmi, teknolojia sahihi na huduma za kifedha zinazoendana na mazingira yao ya kazi hivyo benki imeamua kuja na mpango wa kimkakati unaolenga kuwafikia na kuwawezesha.
“Leo tunaweka historia katika sekta ya madini nchini. Huu si mpango wa kawaida bali ni mkakati mahsusi wa kuleta mapinduzi kwa wachimbaji wadogo na kuwafanya wawe na tija zaidi,” alisema.
Alisema benki itatoa mikopo inayozingatia mahitaji halisi ya wachimbaji, ikiwemo mikopo ya mitaji, ununuzi wa mitambo na vifaa, pamoja na huduma za bima na ushauri wa kitaalamu wa biashara.
Aidha, kwa mara ya kwanza benki hiyo itakubali dhamana zinazotokana moja kwa moja na madini kama dhahabu ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo.
Aliongeza kuwa, lengo la benki siyo kupata faida pekee, isipokuwa kujenga taifa kwa kuwezesha makundi muhimu kiuchumi.
“Tunaamini uwezeshaji wa wachimbaji wadogo utaongeza ajira, kuboresha kipato cha familia na kuongeza mapato ya fedha za kigeni,” alisisitiza.
Hata hivyo, aliwataka wanufaika wa mpango huo, kuzingatia uadilifu na nidhamu ya kurejesha mikopo kwa wakati, akiahidi kuwa CRDB itaendelea kutoa huduma za haraka na zenye uelewa wa mahitaji ya wateja ili kuhakikisha sekta ya madini inakuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
FEMATA
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Rais wa Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, alisema mpango huo, umeleta matumaini mapya kwa wachimbaji wadogo waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukosa dhamana zinazokubalika na taasisi za fedha.
“Leo tunashuhudia mwanzo wa zama mpya. Wachimbaji wadogo tumepewa heshima ya kutambuliwa kama washirika halali wa maendeleo.
“Tunaishukuru sana Benki ya CRDB kwa kutuletea suluhisho hili, na tunaahidi tutaendelea kushirikiana nao pamoja na serikali kuhakikisha tunatumia fursa hii kwa uwajibikaji,” alisema.
Mkataba wa makubaliano uliosainiwa kati ya Benki CRDB na Tume ya Madini, unatarajiwa kuimarisha urasimishaji wa wachimbaji, kuongeza upatikanaji wa mitaji nafuu, kukuza ajira kwa vijana na wanawake katika maeneo ya migodi, pamoja na kuongeza mapato ya serikali kupitia uwazi wa miamala na ufuatiliaji wa kidijitali.




