SERIKALI imetoa tahadhari na kuwataka wananchi kuchukua hatua madhubuti ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko, yakiwemo mafua makali ya influenza, Uviko-19, homa ya dengue na kipindupindu.
Pia, imeziagiza hospitali za rufani za mikoa, taifa, wilaya na vituo vya afya kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa na mengineyo ya mlipuko.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, alitoa maagizo hayo jana mkoani Morogoro, alipozungumza na waganga wakuu wafawidhi na watendaji wa vituo vya afya kutoa huduma vinavyofanya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa.
“Tunaendelea kuviwezesha vituo vingi zaidi katika ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, hasa ukusanyaji wa sampuli mapema na kuziwasilisha Maabara ya Taifa, kazi hii ni ulinzi wa nchi dhidi ya magonjwa ya mlipuko na hakuna mbadala,” alisema.
Aidha, Dk. Grace, aliiasa jamii kuacha matumizi holela ya dawa za antibiotiki kudhibiti usugu wa vimelea dhidi ya dawa, jambo linalosababisha wengi kushindwa kupona baada ya kutumia baadhi ya dawa hizo.
“Mtu akijisikia mafua, kikohozi vimeambatana na homa, mwili kuchoka, kuumwa kichwa, anakimbilia duka la dawa kununua antibiotiki, hiyo siyo sawa, ukihisi unaumwa nenda kwenye kituo cha tiba wakwambie unaumwa nini baada ya kupimwa, badala ya kunywa dawa kiholela,” alisema.
Dk. Grace, alisema licha ya ugonjwa wa kipindupindu kuisha, alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na magonjwa hayo ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, matumizi sahihi ya vyoo na kutumia maji safi na salama.
Pia, alitumia nafasi hiyo, kuwashukuru wadau kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la PATH.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko kutoka wizarani, Dk. Vida Mmbaga, alisema Tanzania imejenga uwezo mkubwa wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Wakati huo huo, katika taarifa aliyoitoa kwa umma, jana, Dk. Grace alisema serikali imetoa tahadhari na kuwataka wananchi kuchukua hatua madhubuti ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko yakiwemo mafua makali ya influenza, Uviko-19, homa ya dengue na kipindupindu.
Alisema hatua hiyo inatokana na mwenendo wa maambukizi unaoendelea kufuatiliwa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wizara ya Afya imebaini ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya influenza na UVIKO-19 katika maeneo mbalimbali.
Ilieleza kuwa, magonjwa hayo huenezwa kupitia majimaji kutoka katika mfumo wa njia ya hewa ya mgonjwa mwenye maambukizi, yanayosambaa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza na kugusa mazingira yaliyochafuliwa na majimaji hayo.
Taarifa hiyo, ilisema dalili za mafua makali ya influenza na UVIKO-19 ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.
Kutokana na hali hiyo, iliwataka wananchi kufunika pua na mdomo wanapokohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Pia, waepuke misongamano isiyo ya lazima na kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili, kuwa karibu na mtu mwenye dalili au wanapokuwa katika maeneo yenye msongamano.
Aidha, iliwahimiza wananchi kuzingatia usafi binafsi, mazingira na kuwahi vituo vya kutolea huduma za afya kwa matibabu badala ya kujitibu au kutumia ‘antibiotiki’ bila ushauri wa wataalamu wa afya.
Taarifa hiyo ilisema homa ya dengue inaendelea kuwa tishio kiafya, ugonjwa huo, huenezwa na mbu aina ya Aedes, mweusi mwenye madoa meupe na hupendelea kuuma asubuhi, mchana na jioni.
“Dalili za dengue ni homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu sehemu za macho na uchovu, zinafanana na dalili za malaria.
“Wananchi wanatakiwa kutokomeza mazalia ya mbu katika maeneo yao kwa kuondoa makopo yaliyotupwa ovyo, matairi ya magari, vifuu na kufukia madimbwi kuzuia maji kutuama.
“Pia, wanatakiwa kujikinga dhidi ya mbu kwa kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha pamoja na kuwahi huduma za afya wanapoona dalili,” alisema.
Kuhusu kipindupindu, taarifa hiyo ilisema nchi imekuwa katika mlipuko uliogusa mikoa yote isipokuwa Kilimanjaro na Njombe, lakini kwa mwezi uliopita hakuna mgonjwa mpya aliyeripotiwa.
Iliwasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuchemsha maji ya kunywa au kuyatibu kwa dawa maalumu kama aquatab au waterguard, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni katika nyakati muhimu, kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula na kuepuka vyakula vilivyoandaliwa katika mazingira yasiyo safi.
Mbali na hilo, ilisisitiza umuhimu wa kujenga na kutumia vyoo bora, kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji na kutunza mazingira kwa kutotupa taka ovyo.
Taarifa hiyo ilisema serikali imejipanga kuendelea kufuatilia na kutoa huduma dhidi ya magonjwa ya mlipuko na itaendelea kutoa taarifa kwa umma kadri hali ya maambukizi itakavyobadilika au hatua zaidi zitakapohitajika kuchukuliwa.






