Na MWANDISHI WETU
VILIO, majonzi na simanzi vilitawala katika Hospitali ya Rufani Mwananyamala, Dar es Salaam jana, baada ya mamia ya waombolezaji, kuaga picha ya Slivia Kalinga (49), anayedaiwa kuuawa na mumewe, Julias Steven.
Tukio hilo la mauaji, linadaiwa kutokea Februari 20, mwaka huu, Mtaa wa Tanganyika, Salasala, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, baada ya wanandoa hao kuwa na ugomvi wa mara kwa mara.
Ilidaiwa Februari 23, mwaka huu, mwili wa Slivia ulikutwa chumbani kwake sakafuni, ukiwa katika hali mbaya, baada ya ndugu na majirani, kuamua kumtafuta kwa siku mbili.
MUME MBARONI
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Mtatiro Kitinkwi, alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema wanamshikilia Steven kwa upelelezi zaidi.
“Ni kweli tulipokea tukio hilo la mauaji ya Slivia Kalinga na mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa,” alisema.
MJUMBE ASIMULIA
Akizungumza juzi na gazeti hili, kuhusu tukio hilo, Mjumbe wa Mtaa wa Tanganyika, Kageshe Fideli, alisema Februari 20, mwaka huu, asubuhi alionana na Slivia na kumuuliza kuhusu kutopatikana katika simu, ambapo alimjibu mume wake ameichukua, hivyo hana mawasiliano.
“Nilishangaa ilivyofika Jumamosi mchana (Februari 21, mwaka huu), kinamama wakimtafuta Slivia kwa sababu hajaonekana katika kikoba.
“Taarifa za kutoonekana kwake, ziliendelea hadi Jumatatu (Februari 23, mwaka huu) asubuhi, ndiyo siku hiyo mwili wake ulionekana chumbani kwake,” alisema.
WANACHAMA WAMLILIA
Mwanachama wa Kikoba cha Upendo Group kilichopo Muungano Goba, ambacho Slivia alikuwa mwanachama, Radhia Said, alisema walipata taarifa kutoka kwa mmoja wa viongozi wa kikoba hicho kuwa mwanamama huyo, hajaonekana akitoka nyumbani kwake kwa siku mbili.
Alidai walifika nyumbani kwa Slivia ambako ukimya ulitawala, hivyo walizunguka nyuma ya nyumba yake, huku wakiita jina lake, bila mafanikio.
“Tulivyoona ukimya umezidi tuliamua kuchungulia madirishani hasa katika chumba chake kwa sababu tunakifahamu. Tulisimama mbele ya dirisha hilo kwa mbali, tulihisi harufu inatoka katika chumba hicho.
“Tuliogopa, tulipiga moyo konde na kuamua kulisukuma dirisha kupata upenyo kidogo, ndipo tukanusa harufu nzito. Tulilia kwa sababu tulijua hapa kutakuwa na kitu ambacho siyo kizuri kwa Slivia,” alidai.
MAJIRANI WASIMULIA
Kwa upande wake, Emakuta Edward anayeishi Mtaa wa Muungano, alidai alimwona jirani yake huyo, Februari 20, mwaka huu na kumweleza kuwa mume wake amemnyang’anya simu.
“Aliniambia amechoshwa na tabia za mume wake, mara amwibie mchele, mara fedha, nguo na hata wakati mwingine anachukua fedha za mchezo.
“Slivia alikuwa akinihadithia habari hizo, huku akilia kwa uchungu na kwa wakati mwingine alikuwa anajuta kuolewa na mwanaume huyo, ambaye kila siku anamjaza machungu ndani ya moyo wake,” alidai Emakuta.
Jirani mwingine wa Slivia, Upendo Kassimu, alidai alimwona mume wa marehemu akiwa na jeraha mkononi na alipomhoji alimjibu amekutwa na majanga.
Upendo alidai Slivia muda mwingi alikuwa akifanya shughuli za uzalishaji mali, huku akiwafundisha wanafunzi wa awali.
Alisema kujishughulisha kwake huko, kulimsaidia Slivia kuendesha maisha yake ya kila siku na hata kuwalipia ada ya shule watoto wake wawili wanaosoma sekondari.
“Mwenzetu alikuwa na maisha mazuri, siyo mwanamke wa kukaa bure alipenda kujishughulisha hadi tukampa jina ‘mwanamke shupavu’,” alisema.
Jirani mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alidai: “Nilimwona mume wa marehemu siku ya Jumatatu asubuhi amekaa barazani kwake anawarudisha wanafunzi wanaokuja kusoma na kuwambia mwalimu wao amesafiri.
“Nilishangaa kwanini anawaambia hivyo wanafunzi, wakati sisi tukimuuliza mke wake yupo wapi anatujibu hajui halipo. Mwanaume aliondoka pale kibarazani saa 2.30 asubuhi, huku akijua hakuna mwanafunzi mwingine atakayefika hapo shuleni,” alidai.
Jirani mwingine alidai alibahatika kuwasaidia polisi kuutoa mwili wa Slivia na kuupakia katika gari la polisi.
“Ilikuwa ni ngumu kwa jinsi nilivyomwona jirani alivyolala chini chumbani kwake, sikuamini niliona baadhi ya majeraha katika mwili wake, tulimbeba kwa vifaa maalumu na kumpakiza ndani ya gari la polisi,” alisema
MCHUNGAJI
Akizungumza katika ibada fupi ya kuuaga mwili wa Slivia iliyofanyika Hospitali ya Rufani Mwananyamala, Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Methodist Church (TMC), Young Byamungu alieleza kusikitishwa na msiba huo, huku akiwasihi waombolezaji wa msiba huo wanawake kuwapenda waume zao na wanaume kuwapenda wake zao.
“Hiki kilichofanywa kwa Slivia siyo mapenzi ya Mwenyezi Mungu, msijaribu kufanya vitu hivi, hakuna kitabu kilichoandikwa kuwa mwanamke ni wakunyanyasika.
“Ninajua kila mtu ana uchungu ndani ya moyo wake Mwenyezi Mungu awaondolee maumivu haya mliyonayo,”alisema.
Slivia alizikwa kijijini kwao Mafinga, Iringa, jana na ameacha watoto watatu.




