ARUSHA
Na Lilian Joel
KIKAO cha Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kimezidi kufungua fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara nchini, huku kikionyesha namna uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ukiwa imara katika kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa Tanzania.
Hayo yameelezwa na wafanyabiashara na wananchi mkoani Arusha wakati wakijiandaa kupokea ugeni mzito wa viongozi wa jumuiya ya EAC wanaotarajiwa kuwasili nchini kuanzia leo kwa ajili ya kikao kinachotarajia kufanyika kesho jijini hapa.
Kikao hicho ni mkutano wa 25 wa kawaida wa wakuu wa nchi wa EAC, utakaobeba maamuzi muhimu yatakayoendeleza mustakabali wa mtangamano wa kikanda wa jumuiya hiyo.
Pia, katika kikao hicho wakuu hao wanatarajiwa kumteua Katibu Mkuu mpya wa EAC, kuteua Majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki, kuongeza muda wa uteuzi wa Manaibu Katibu Wakuu, kuteua Makamishna wa Mamlaka ya Ushindani ya EAC na kuridhia miswada iliyopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki.
Joseph Ole Naiputuka alisema kikao cha viongozi wakuu wa EAC kimekuwa na fursa kubwa kwa wakazi wa Arusha, ambapo maeneo mengi ya kibiashara yamekuwa na watu wengi na mzunguko wa fedha umekuwa mzuri.
“Tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa juhudi kubwa ya kuifungua nchi. Mkoa wa Arusha umekuwa na shughuli nyingi zinafanyika kutokana na uongozi bora unaotoa majawabu mazuri,” alisema.
Naye, mfanyabiashara wa magari ya kukodisha mkoani Arusha, Onesmo Mushi alisema kikao cha EAC kimekuwa fursa kubwa kutokana na watu wengi kufanikiwa kufanya biashara ikiwemo za malazi, magari na vyakula.
“Mkutano umekuwa na fursa, wiki nzima imekuwa na neema kwetu. Tunampongeza sana Rais Dk. Samia kwa juhudi zake za kuboresha uhusiano wa Tanzania kimataifa na huu ni mwendo mzuri wa kukuza uchumi wa watu wa Arusha,” alisema.
KATIBU MKUU EAC AZUNGUMZA
Akizungumza jana Katika makao makuu ya EAC Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, alisema mkutano huo ni jukwaa muhimu la uongozi wa jumuiya kukutana na kutoa maamuzi ya kimkakati.
Alisema mkutano huo utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Kuimarisha Mtangamano kwa Ajili ya Kuboresha Maisha ya Wananchi wa EAC,” ikiwa ni uthibitisho wa dhamira ya nchi wanachama kuendeleza ushirikiano wa kikanda na kukuza maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki.”
Kwa mujibu wa Veronica, mkutano huo utawakutanisha wakuu wa nchi nane ambao ni Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia, Uganda na Sudan Kusini.
Nchi hizo ni wanachama wa EAC ambapo watapata fursa ya kujadili utekelezaji wa programu za kikanda, kupokea ripoti ya Baraza la Mawaziri kwa kipindi cha Novemba 30, 2024 hadi Desemba 31, 2025, sanjari na masuala ya kimkakati yanayolenga kuimarisha mtangamano na ustawi wa wananchi.
UZINDUZI WA DHAMANA YA FORODHA YA EAC
Alisema katika mkutano huo pia kutafanyika uzinduzi rasmi wa Dhamana ya Forodha ya EAC, mfumo wa dhamana moja ya kikanda utakaorahisisha usafirishaji wa bidhaa katika nchi wanachama.
“Kupitia utaratibu huo mpya, wafanyabiashara na mawakala wa forodha watapata dhamana moja tu itakayotambulika katika nchi zote wanachama badala ya kuwa na dhamana tofauti kwa kila nchi wanayopitia,” alisema.
“Mfumo huo utaunganisha mamlaka za forodha, kampuni za bima na taasisi za kifedha chini ya mfumo mmoja wa kikanda, hivyo kupunguza gharama za uendeshaji, kupunguza ucheleweshaji mipakani, kulinda mapato ya serikali na kuharakisha usafirishaji wa bidhaa ndani ya Jumuiya,” alisema.
Kuzinduliwa kwa Mkakati wa saba wa Maendeleo Mkutano huo pia utashuhudia uzinduzi wa Mkakati wa saba wa Maendeleo wa EAC (2026/27–2030/31), unaoweka mwelekeo wa kuharakisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mkakati huo unaendana na Dira ya EAC 2050, Ajenda 2063 ya Umoja wa Africa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), unaolenga kuongeza ushindani wa kikanda sanjari na uimara wa uchumi wa nchi wanachama.
“Kuandaliwa kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi jijini Arusha kunatoa fursa kwa viongozi wetu kufanya maamuzi yatakayoongeza ushirikiano, kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa pamoja kwa wananchi wa Afrika Mashariki,” alisema.
Aliongeza kuwa uzinduzi wa Dhamana ya Forodha na Mkakati wa saba wa maendeleo unaashiria mwelekeo wa Jumuiya katika kutekeleza suluhisho za vitendo zinazoongeza ushindani na uimara wa uchumi wa kikanda.
Aidha, alisema mkutano huo umetanguliwa na kikao maalumu cha Baraza la Mawaziri wa EAC kilichoanza Machi 2 hadi 5, mwaka katika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha.
Matokeo ya mkutano huo yanatarajiwa kuimarisha ulinganifu wa sera miongoni mwa nchi wanachama na kuharakisha utekelezaji wa programu muhimu za kikanda kwa lengo la kukuza uchumi shirikishi na mtangamano wa kina zaidi wa Afrika Mashariki.
KUKUA KWA SHUGHULI ZA KIBIASHARA EAC
Alisema takwimu zinaonesha kuwa biashara ya ndani ya ukanda imeongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 28.2 katika robo ya pili ya mwaka 2024 hadi dola bilioni 39 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Veronica, mafanikio hayo yameonekana wazi katika utekelezaji wa Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, maandalizi ya Umoja wa Fedha na mchakato wa kuelekea Shirikisho la Kisiasa.
Huduma za mipaka zarasimishwa Kuhusu huduma za mpakani kurasimishwa Veonica alisema kupitia mfumo wa One Stop Border Posts (OSBPs), muda wa kuvuka mipaka umepungua kwa takribani asilimia 70, huku ukileta uokoaji wa zaidi ya dola milioni 63 kila mwaka.
“Usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Mombasa kwenda Kampala umepungua kutoka wastani wa siku 18 mwaka 2007 hadi siku 4–5 mwaka 2020”.
Alisema Mfumo wa Electronic Single Window (ESW) nao umerahisisha nyaraka za forodha kwa njia ya kidijitali, kupunguza urasimu na ucheleweshaji bandarini na mipakani.
Uhuru wa Watu na Ajira Katibu mkuu huyo alisema raia wa nchi wanachama sasa wanasafiri bila viza ndani ya ndani ya nchi wanachama na kwasasa wanatumia hati za kusafiria ya kielektroniki ya EAC iliyoanzishwa mwaka 2016.
“Uhuru huu wa watu na ajira pia umetoa fusa kwa wataalamu kama wahasibu na wahandisi kufanya kazi katika nchi yoyote mwanachama kupitia mikataba ya kutambua taaluma (MRAs)”.
Alisema utaratibu huo umeimarisha soko la ajira la kikanda na kuongeza fursa kwa vijana na wataalamu.
Soko la Watu Milioni 300 Kwa upande wa masoko, Veronica alisema kwa sasa EAC ni soko la zaidi ya watu milioni 300 lenye pato la zaidi ya dola bilioni 300 za Marekani na limevutia uwekezaji mkubwa wa ndani na nje, kukuza viwanda vya kuongeza thamani na kupanua ajira.
Umoja wa Fedha Kuhusu fedha alisema Jumuiya imepanga kufikia Umoja wa Fedha ifikapo mwaka 2031 na tayari mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS) umeanzishwa ili kuruhusu miamala ya fedha kwa kutumia sarafu za nchi husika.
“Kwa sasa tunaendelea kuunda taasisi muhimu imiwemo ya Taasisi ya Fedha ya Afrika Mashariki,Tume ya Usimamizi na Uzingatiaji ili kuweka msingi imara wa sarafu ya pamoja” alisema
Amani na Mwelekeo wa Shirikisho la Kisiasa Mbali na uchumi, alisema EAC imeendelea kushirikiana katika masuala ya amani na usalama, ikiwemo juhudi za kidiplomasia na mchakato wa amani wa Nairobi, mashauriano ya kitaifa yanaendelea katika baadhi ya nchi wanachama kuhusu rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la EAC.
Aidha, wataalamu wanasema Umoja wa Fedha utapunguza gharama za miamala, kuondoa changamoto za ubadilishaji wa sarafu na kuongeza imani kwa wawekezaji katika nchi za EAC.
“Hii ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa jumuiya yetu kwa sababu utapunguza gharama mbalimbali ikiwemo miamala ya fedha na hii itasaidia sana wafanyabishara kufanya malipo ya bidhaa mbalimbali tofauti na hivi sasa”Alisema Walter Maeda
Mafanikio ya miaka 25 ya EAC yanaashiria dhamira thabiti ya nchi wanachama kujenga ukanda wenye uchumi imara, mipaka iliyorahisishwa na mshikamano wa kisiasa. Safari bado inaendelea, lakini msingi uliowekwa unaonyesha mustakabali wa matumaini kwa Afrika Mashariki.




