Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameizindua na kuipa maagizo matano Bodi ya Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kilichopo mkoani Morogoro.
Ametoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam Machi 6, 2026, ambapo ameelekeza bodi kuimarisha mifumo ya kitaifa ya Upimaji, Utoaji Taarifa na Uhakiki wa gesijoto (MRV), kuhakikisha taarifa za kaboni nchini zinakuwa sahihi, za kuaminika na zinazokubalika kimataifa.
Pia, ameitaka kuhakikisha Miradi yote ya kaboni inayotekelezwa nchini inasimamiwa kwa ufanisi, uwazi na kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa pamoja na maslahi mapana ya taifa.
Waziri Masauni amesema bodi hiyo inapaswa kuweka mazingira wezeshi yatakayovutia uwekezaji wa ndani wa kimataifa katika sekta ya kaboni, huku ikihakikisha uwekezaji huo unalinda rasilimali za taifa na kuleta manufaa ya kweli kwa wananchi, kuhakikisha kunakuwepo mfumo wa haki na uwazi wa mgawanyiko wa manufaa, jamii zinazohifadhi rasilimali za asili zinufaike moja kwa moja na miradi ya Kaboni inayotekelezwa katika maeneo yao.
“Kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika mifumo ya kimataifa ya biashara ya kaboni hususan chini ya Ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris, ikiwemo mifumo ya soko la kaboni kuongeza fursa za kiuchumi kwa taifa letu,” amesema Masauni.
Aidha, ameisisitiza bodi hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kituo kinaendeshwa kwa uwajibikaji, uadilifu na weledi wa hali ya juu kuhakikisha mifumo ya usimamizi wa sekta ya kaboni inalinda kikamilifu maslahi ya taifa.
“Ni matarajio ya serikali kuona kituo hiki kinakuwa kitovu cha ubora katika masuala ya ufuatiliaji wa kaboni, biadhara ya kaboni na tafiti za mabadiliko ya tabianchi katika ukanda wa Afrika. Haya ni matarajio makubwa kwa taifa letu na yanahitaji usimamizi madhubuti wa taasisi, mifumo imara ya ufuatiliaji pamoja na ushirikiano wa wadau wote,” alisema.
Aliongeza matarajio ya serikali yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na Mpango wa muda mrefu wa utekelezaji wake, sekta ya kaboni ina uwezo wa kuchangia takribani Dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk. Albina Chuwa alisema ushirikiano ndiyo jambo la msingi katika kufikisha lengo na ndoto za watanzania, hivyo watajitahidi kutafuta fursa kupata matokeo mazuri.
“Ushirikiano wa kutosha ndiyo naomba kutoka kwa kila mmoja wetu, kwani haya yote tunayoyazungumza tutakuwa tunafanya kazi nyepesi katika kuhakikisha kituo chetu cha kaboni kinafanya vizuri,” alisema Dk. Albina.
Alieleza biashara ya kaboni inaendelea kukua kwa kasi duniani, hivyo bodi hiyo ina jukumu muhimu la kuhakikisha rasilimali za kaboni za Tanzania zinasimamiwa kwa uwazi, weledi na kuzingatia mifumo na viwango vinavyokubalika kimataifa.
Wajumbe wanaounda Bodi ya Kituo cha Kaboni ni Khamis Hamza Khamis, Amne Sued Kagasheki, Farhat Mabrouk, Dk. Ladislaus Kyaruzi, Rishad Bade pamoja na Dk. Philipina Shayo.






