Na NASRA KITANA
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetangaza kuwepo kwa fedha sh. bilioni 50 kwa ajili ya kuwawezesha vijana wanaojihusisha na sekta ya ubunifu nchini.
Fedha hizo pia zimetengwa kwa ajili ya watengeneza maudhui mtandaoni (content creators), wasanii, wanamuziki, waigizaji, waandishi wa habari, watu wenye ushawishi mitandaoni na wabunifu wa kazi mbalimbali za sanaa.
Akizungumza jijini Arusha, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda alisema kuwa mfuko huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia sekta ya habari, sanaa na ubunifu.
“Awali Wizara ilikuwa imepangiwa kupewa sh. bilioni 20, lakini baada ya mazungumzo na Benki ya CRDB, kiwango hicho kimeongezwa na kufikia sh. bilioni 50 ili kupanua wigo wa vijana watakaonufaika na mfuko huo,” alisema Makonda.
Waziri Makonda alisema kuwa mfuko huo ni kwa ajili ya kuwainua vijana kutoka katika sehemu moja kwenda nyingine ili kuweza kunyanyuka kiuchumi na kurejesha tabasamu kwa Watanzania.
Alisema kuwa kwa hivi sasa kinachosubiriwa ni tarehe rasmi ya uzinduzi wa mfuko huo, ambapo baada ya uzinduzi fedha hizo zitaanza kutolewa kwa vijana waliopo katika sekta ya habari, sanaa na ubunifu ili kuwawezesha kukuza kazi zao na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.
Makonda alisema kuwa Wizara inapanga kuzindua rasmi mfuko huo katika hafla maalumu inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni, ambapo Rais Dk. Samia, anatarajiwa kuwa mgeni.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha vijana wanapata fursa za kiuchumi na kutumia vipaji vyao kama chachu ya maendeleo ya Tanzania.




