Na AMINA KASHEBA
BAADA ya ushindi wa mabao 3-0, Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge amesema amefurahishwa na kiwango kizuri walichokionesha wachezaji wake katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji.
Azam ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Akizungumza baada ya kumaliza mchezo huo, kocha huyo alisema kufuatia kupata sare michezo miwili alikaa na kuzungumza na wachezaji na kuwahamasisha kupambana kuhakikisha timu inafanya vizuri.
Alisema katika mchezo huo, kila mchezaji alipambana na kutimiza majukumu yake uwanjani ndiyo maada waliibuka na ushindi.
“Ninafurahi kwa sababu wachezaji wangu wamecheza vizuri baada ya kutoka sare michezo miwili, niliongea nao jinsi ya kupambana ili kupata ushindi na kuondoka na pointi tatu muhimu katika mchezo wetu.
“Ninashukuru kuona wachezaji walipambana na kupata pointi tatu ikiwemo kuonesha kiwango kizuri tofauti na mechi zingine ambazo tulicheza,pia ninataka kushinda haijalishi iwe nyumbani au ugenini,” alisema Ibenge.
Kocha huyo alisema mbali ya kupata ushindi wa mabao 3-0, lakini mchezo haukuwa rahisi tofauti na tulivyotarajia.
“Licha ya kupata ushindi, lakini mchezo ulikuwa mgumu ninashukuru wachezaji walipambana hadi kupata matokeo ambayo yametupa pointi tatu, muhimu, hivi sasa tunakwenda kujipanga na michezo mingine ijayo,” alisema Ibenge.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam imefikisha pointi 27 ikiwa nafasi ya tatu baada baada ya kucheza mechi 13 hadi hivi sasa.




