• ePaper
Sunday, April 5, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

LUKUVI KUAGWA MIKOA MITATU

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
March 27, 2026
in Habari, Kitaifa
0
LUKUVI KUAGWA MIKOA MITATU
0
SHARES
13
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Dodoma
Na Mwandishi Wetu

MWILI wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi, unatarajiwa kuagwa katika mikoa mitatu ya Dodoma, Dar es Salaam na Iringa.

Lukuvi alifariki dunia juzi, jijini Dodoma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.

Akizungumza jijini Dodoma, jana, nyumbani kwa marehemu, Ofisa Mwandamizi wa Bunge anayeshughulikia Habari, Mawasiliano, Elimu kwa Umma, Patson Sobha, alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwaongoza Watanzania katika mazishi ya Lukuvi yatakayofanyika Idodi, Iringa, Vijijini, Machi 31, mwaka huu.

Alisema mwili wa Lukuvi utaagwa katika mikoa mitatu ya Dodoma, Dar es Salaam na Iringa ambapo kwa Dodoma utaagwa leo katika viwanja vya Bunge na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ataongoza shughuli hiyo.

Pia, alisema baada ya kuagwa Dodoma mwili wa Lukuvi  utasafirishwa kwenda Dar es Salaam na Machi 28, mwaka huu,  utaagwa viwanja vya Karimjee ambapo Rais Dk. Samia atawaongoza Watanzania kutoa heshima za mwisho.

Alisema baada ya kuagwa mwili wa Lukuvi utapelekwa Iringa Mjini, jioni ambako utaagwa na wananchi wa Iringa Mjini, eneo la Gangilonga Machi 29.

Sobha alisema Machi 30, mwaka huu, mwili wa Lukuvi utasafirishwa kwenda kijijini Idodi, Iringa Vijijini kwa maziko yatakayofanyika Machi 31, mwaka huu, kijijini hapo na kuhudhuriwa na Rais Dk. Samia.

DK. MWIGULU NCHEMBA

Akizungumza na waombolezaji nyumbani kwa marehemu kwa niaba ya serikali, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu aliwaomba Watanzania waendelee kumwombea.

“Kwa niaba ya serikali natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa. Jambo hili zito, gumu kulielewa na gumu kulipokea.

“…Lakini ndiyo limeshatufika na sote hatukutarajia maana Mheshimiwa Waziri alikuwa kazini. Tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu na kuifariji familia. Mwenyezi Mungu awaimarishe kwa sababu yeyé ndiye mfariji mkuu,”alisema.

Alisema serikali iko bega kwa bega na familia katika kipindi chote cha majonzi, taifa limempoteza kiongozi mahiri na mwenye ujuzi mkubwa katika utendaji kazi wake.

WANANCHI ISIMANI

Katika hatua nyingine, wananchi wa Kijiji cha Idodi, Kata ya Idodi, wilayani Iringa Vijijini, walisema watahakikisha wanamuenzi Lukuvi kwa kuendeleza na kuitunza miradi ya maendeleo na maono aliyoyaacha kwa kuhakikisha jitihada zake alizozifanya miaka 30 ya ubunge jimboni humo zinaendelea kuzaa matunda kwa vizazi vijavyo.

Walisema wamempoteza shujaa wa maendeleo na kiongozi mwenye utu mkubwa.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Chahe, alisema kifo cha Lukuvi kimewaacha katika hali ya sintofahamu na huzuni, akieleza mchango wake kwa maendeleo ya kijiji ambao ulikuwa mkubwa na wa kipekee.

Mwenyekiti huyo alisema hali ya wananchi ni ya huzuni kutokana na tukio hilo na kwamba, wengi wao walikuwa  na ukaribu wa kipekee na marehemu enzi za uhai wake na walimtegemea katika kuhamasisha maendeleo.

Alisema Lukuvi alikuwa kiongozi anayeshirikiana kwa karibu na wananchi, akisikiliza changamoto na kushiriki shughuli za kila siku, jambo lililomfanya apendwe na kuheshimiwa na jamii.

Kuhusu sekta ya elimu, Mwenyekiti huyo alisema wananchi watakumbuka jinsi alivyosaidia kujenga na kuboresha miundombinu ya shule, hali iliyowezesha watoto wengi kupata elimu katika mazingira bora.

“Sekta ya afya nayo ilinufaika kwa kiasi kikubwa, ambapo vituo vya huduma viliboreshwa na kusogezwa karibu na wananchi, hivyo kupunguza umbali wa kufuata matibabu na kuokoa maisha ya watu wengi,”alisema.

Aidha, jitihada zake katika kuanzisha miradi ya skimu za umwagiliaji zilitajwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima na ziliwasaidia kuachana na utegemezi wa mvua na kuongeza uzalishaji na kipato cha familia nyingi.

Mwenyekiti huyo alisema mchango wake katika michezo uliwezesha vijana kupata fursa ya kukuza vipaji vyao kupitia mazingira aliyoyawezesha, jambo lililowapa matumaini na mwelekeo mpya wa maisha.

Naye, mkazi wa kijiji hicho, Juliana Mwekule, alimtaja Lukuvi kuwa kiongozi shupavu, mpenda watu na aliyejitoa kwa dhati kutetea maslahi ya wananchi pamoja na maendeleo ya taifa.

Alisema wameondokewa na kiongozi aliyekuwa karibu nao katika nyakati zote, aliyekuwa tayari kusikiliza changamoto zao na kushiriki kwa vitendo katika jitihada za kujiletea maendeleo katika kijiji hicho na maeneo jirani.

VYAMA VYA SIASA

Wanasiasa kutoka vyama mbalimbali mkoani Iringa ambao waliwahi kufanya kazi na Lukuvi, walielezea masikitiko yao kufuatia kifo chake wakimtaja kuwa kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

DAUDI MASASI

Kamishna wa ADC Kanda ya Iringa, Daudi Masasi, alisema Lukuvi atakumbukwa kwa mchango wake katika siasa za mageuzi pamoja na uwezo wake wa kushirikiana na watu wenye itikadi tofauti kwa lengo la kuleta maendeleo.

PETER MSIGWA

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Msigwa, alisema kifo cha Lukuvi ni pigo kubwa si tu kwa wananchi wa Iringa bali kwa taifa kwa ujumla.

Alieleza kuwa, Lukuvi alikuwa kiongozi jasiri, mwenye msimamo thabiti na aliyejitolea kuwatumikia wananchi wake kwa dhati.

ISRAEL CHOTAMASEGE

Katibu wa Mbunge, Israel Chotamasege, alisema kuwa kifo cha Lukuvi ni pigo kubwa kwa wananchi wa Isimani na aliwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi chote cha maombolezo.

Mawaziri, wabunge wazidi kumlilia

Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Twaha Mwakioja, alimwelezea Lukuvi alikuwa ni kiongozi shupavu, mnyenyekevu na mzalendo aliyetoa maisha yake yote kulitumikia taifa kwa uadilifu katika nyadhifa alizoshika serikalini na ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Taifa limepoteza nguzo muhimu ya uongozi. Lukuvi alikuwa kielelezo cha utendaji kazi usio na kuchoka, mwanadiplomasia wa masuala ya kijamii na mtatuzi wa kero za wananchi aliyeacha alama isiyofutika nchini,” alisema.

BALOZI  LIBERATA  MULAMULA

Waziri mstaafu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya Wanawake Amani na Usalama (AU), Balozi Liberata Mulamula, alisema Lukuvi ndiye aliyekuwa ‘Chief Whip’ bungeni alikuwa anawaongoza na kuwaelekeza wabunge.

“Siwezi kusema nilifanya naye kazi maana alikuwa ni kiongozi wetu mwandamizi. Binafsi nilijifunza mengi kisiasa kutoka kwake hususan nikiwa bungeni alikuwa kama mwalimu kwangu.

“Kwa kweli kifo chake ni pigo kubwa kitaifa. Ameacha pengo kubwa Serikalini na Bungeni,”alisema.

Alisema kiongozi huyo alihudumu miongo kadhaa, huku akitoa salamu za pole kwa Rais Dk. Samia na Spika wa Bunge, Musa Hassan Zungu, kwa msiba huo kwa nchi.

“Tutamkubuka daima Mhe. Lukuvi kwa utanashati wake, uzoefu wake mkubwa, busara zake na ucheshi,”alisema.

PROFESA KABUDI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Paramagamba Kabudi, alisema Lukuvi atakumbukwa kwa kufanya kazi kwa kujituma, bila kuchoka na kwa umoja.

HAMAD CHANDE

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, alisema Lukuvi alikuwa ni mtu wa aina yake, mpole na mwenye moyo wa kusaidia wengine.

Alifafanua kuwa, Lukuvi alikuwa mzoefu bungeni na alipokea wabunge wengi na kuwafundisha kazi, wengi waliopita katika mikono yake wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Lukuvi alikuwa muumini wa kupenda watu wote na kujali watu wote bila kujali wanatoka mkoa gani na kutuunganisha kwa pamoja. Hata alipokuwa Waziri wa Ardhi alikuwa muumuni wa kusikiliza watu,”alisema.

KHAMIS MBETO

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis, alisema CCM Zanzibar ilimtaja Lukuvi alikuwa ni kiungo na kiraka kilichoziba katika nyakati zote ngumu za kisiasa, kiutendaji na kiutawala.

Mbeto alisema Tanzania imepoteza kiongozi madhubuti, jasiri, mzalendo na mshauri muhimu wa vipindi vyote katika maisha yake.

Alisema kuna mambo muhimu yatakayofanya Lukuvi azidi kukumbukwa na jamii katika utumishi wake kwa kuwa kioo kilichoakisi tija na utatuzi wa changamoto katika siasa, utumishi na utawala.

Previous Post

RUFANI YA SENEGAL KUSIKILIZWA

Next Post

WASIRA AWATOLEA UVIVU WALIOANZA MBIO ZA URAIS

Next Post
WASIRA AWATOLEA UVIVU WALIOANZA MBIO ZA URAIS

WASIRA AWATOLEA UVIVU WALIOANZA MBIO ZA URAIS

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

ARAJIGA, KAYOKO HAOO CAFCL

ARAJIGA, KAYOKO HAOO CAFCL

7 months ago
‘BIRTHDAY’ YA MAZINGIRA

‘BIRTHDAY’ YA MAZINGIRA

2 months ago

Popular News

  • RAIS DK. SAMIA SULUHU MWANADEMOKRASIA WA KISIASA

    RAIS DK. SAMIA SULUHU MWANADEMOKRASIA WA KISIASA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • CHAMUDATA YAZUNGUMZIA AMANI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MCHENGERWA ASHUSHA MAAGIZO KWA WAGANGA WAKUU WA MIKOA, WILAYA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. MWINYI AELEZA FAIDA YA KULINDA TUNU YA AMANI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • UTEUZI WA PROFESA KABUDI GUMZO NCHINI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?