Na ZIANA BAKARI
WADAU wakiwemo wasomi wa uchumi nchini, wamesema kuna uhusiano mkubwa kati ya uwekezaji na amani ambayo huvutia wawekezaji wa kigeni popote duniani.
Pia, wamewasihi Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi ambayo ni tunu ya taifa inayopaswa kupewa kipaumbele, huku wakishauriwa kutokubali kushawishiwa na mtu yeyote kuvuruga amani iliyopo.
Wakizungumza UHURU, baadhi ya wadau hao walisema wawekezaji wengi huvutiwa kuwekeza katika nchi yenye amani.
PROFESA WANGWE
Mtaalamu wa uchumi, Profesa Samuel Wangwe, alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya uwekezaji na masuala ya amani, kwa sababu asilimia kubwa huvutiwa kuweka mitaji yao katika sehemu zilizo salama.
Alisema siku zote wawekezaji wanapenda sehemu yenye amani na hawawezi kwenda mahali penye vurugu.
“Wawekezaji wanapenda nchi yenye amani, kama kuna vurugu watakwenda nchi nyingine ambayo ina amani, hivyo kuna uhusiano mkubwa kati ya uwekezaji na amani ndani ya nchi,”alisema Profesa Wangwe.
Alifafanua nchi yoyote haiwezi kupata maendeleo bila kuwepo amani inayoambatana na utawala bora ambazo ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanafanikiwa na kuleta tija kwa taifa.
Kwa mujibu wa Profesa Wangwe, uwekezaji unahitaji mazingira ya utulivu kuweza kunufaisha taifa.
“Uwekezaji ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi, lakini uwekezaji uweze kuvutia na kukua, lazima kuwa na amani, siku zote machafuko, migogoro au kutokuwepo usalama kunaweza kuzuia wawekezaji kutoka nje na hata kukwamisha wazawa kufanya biashara zao kwa uhuru,” aliongeza.
Alieleza mtu anapotaka kuwekeza hatopenda uwekezaji wake uingie katika dosari sababu ya vurugu, hivyo lazima atakwenda sehemu yenye amani.
Akitaja athari za kutokuwepo amani, Profesa Wangwe alisema ni kupungua uwekezaji nchini, maendeleo yatapungua na hata wananchi watakwama kuendelea na shughuli za kujipatia kipato.
“Amani inapokosekana ndani ya nchi hata ukuaji wa uchumi utashuka na maendeleo yoyote hayawezi kupatikana bila ya uwepo wa amani na tujue tu tutaweza kukosa wawekezaji kwa sababu nchi itakuwa haina amani.
“Tunapaswa kufahamu amani ni jambo muhimu sana ndani ya nchi kwa sababu, maendeleo yote yanahitaji uwepo wa amani kuvutia wawekezaji nchini,” alisema.
NINI CHA KUFANYA
Profesa Wangwe aliwashauri Watanzania kuendelea kudumisha amani, kwani ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo.
“Amani ni moja ya hazina kubwa tuliyonayo, tuendelee kudumisha amani na umoja wetu na mshikamano, hii itasaidia maendeleo kuzidi kuonekana.
“Siku zote uwepo wa amani ni jambo ambalo linavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini na linachochea maendeleo ya kiuchumi, hivyo niwaombe sana kulinda tunu yetu ya amani na serikali isichoke kuendelea kusikiliza changamoto za wananchi,” alisema Profesa Wangwe.
MHADHIRI WA OUT
Katika hatua nyingine, Mhadhiri wa Uchumi Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Timothy Lyanga, alisema mwekezaji siku zote anapotaka kuwekeza sehemu anachoangalia ni utulivu na amani katika nchi.
Alisema mwekezaji hawezi kuwekeza sehemu ambayo haina amani kwa sababu anachoangalia ni uhakika wa usalama wa mali zake, wafanyakazi na mazingira ya biashara.
Katika mazingira ya amani, Dk. Lyanga alisema hakuna mwekezaji aliye tayari kuweka mtaji wake katika mazingira ya wasiwasi sababu ya migogoro.
Alibainisha athari za kutokuwepo amani ni chanzo cha shughuli za kiuchumi na kijamii kushindwa kufanyika vizuri.
“Niwashauri Watanzania wenzangu tuendelee kuitunza amani yetu, kwani maendeleo yoyote yanahitaji amani, tuthamini nchi yetu na kuipenda,”alisema Dk. Lyanga.
AMANI, UWEKEZAJI
Akizungumzia uhusiano uliopo baina ya uwekezaji na amani, Mhandiri Mwandamizi wa OUT, Dk. Mohammed Maguo, alisema kuna uhusiano mkubwa baina ya vitu hivyo viwili.
Alisema kama hakuna amani hata uwekezaji hauwezi kufanyika ndani ya nchi, hivyo aliwahimiza Watanzania kutunza amani kuvutia wawekezaji zaidi.
TUSIDANGANYIKE KABISA
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi na Uongozi kutoka Chuo cha Mwalimu Nyerere, Dk. Philip Daninga, alisema wawekezaji huvutiwa zaidi kuwekeza sehemu yenye utulivu na uongozi mzuri.
“Tuendelee kudumisha amani yetu na tusidanganyike na mtu yeyote kuvuruga amani iliyopo, tusichoke kufundisha vizazi vyetu umuhimu wa amani ndani ya nchi,”alisisitiza Dk. Daninga.
WANANCHI WAHIMIZWA
Naye, Mhadhiri wa Idara ya Hisabati wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Sylvester Rugeihyamu, alisema hakuna mwekezaji atakayekubali kuwekeza sehemu isiyokuwa na amani hivyo, aliwahimiza wananchi kulinda amani kwani, tatizo dogo likitokea linaweza kuharibu kitu kikubwa.
“Tujifunze yaliyotokea kipindi cha nyuma, tuwe tayari kubadilika na kuilinda nchi yetu ibaki kuwa ya amani izidi kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza,” alisisitiza Dk. Rugeihyamu.




