Na NASRA KITANA
SIKU moja baada ya Serikali kupitia Baraza la Michezo Taifa (BMT), kuidhinisha marekebisho ya katiba ya Simba, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu amesema kuwa wamepokea maelekezo na hivi sasa wanahitaji muda kuyafanyia kazi.
Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Abel Ngilangwa alisema miongoni mwa maboresho yaliyoidhinishwa ni kuweka wazi nafasi ya Simba Sports Club Company Limited kama chombo kitakachosimamia masuala ya kibiashara na kiutendaji, huku umiliki wa hisa ukiendelea kuwa chini ya Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama.
Pia, serikali ilibainisha kuwa muundo mpya wa Baraza la Wadhamini utakuwa na wajumbe wasiopungua watano na wasiozidi saba, watakaosimamia mali za klabu kwa niaba ya wanachama, huku Mkutano Mkuu ukiendelea kuwa chombo chenye mamlaka ya mwisho.
Akizungumza mara baada ya kuidhindishwa kwa marekebisho hayo, Mangugu alisema watakwenda kufanyia kazi haraka kulingana na kile ambacho kimewasilishwa.
Alisema mchakato wa mabadiliko ndani ya klabu hiyo unagusa mamlaka zaidi ya moja za serikali, hivyo kuna mambo mengi ambayo yanahitaji muda zaidi.
“Niwaambie kuwa tunahitaji muda kwani kuna eneo linalosimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kuna eneo linalosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria, pia kuna eneo linalosimamiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, hivyo hatuwezi kufanya kwa haraha jambo hilo ila tutalifanyika kazi,” alisema Mangungu.
Hata hivyo wadau wa mchezo wa soka, walisema kuwa hilo ni jambo zuri kwa Simba na wana imani kuwa watafanikiwa katika machakato wao huo.
Akizungumzia hilo, Kenedy Mwaisabula alisema hivi sasa wanakwenda kuwa na Simba mpya, kwani mchakato ulikuwa wa muda mrefu, wanaelekea mwishoni, hivyo anaamini na klabu zingine zinatakiwa kuiga mfano huo.
Naye aliyekuwa kiongozi wa zamani wa Simba, Hassan Hasanoo alisema wamefurahia marekebisho hayo kutoka BMT ana imani Simba inakwenda kuwa bora zaidi.
“Timu yetu bado imara na nina amini mchakato wa mabadiliko ukimalizika tutakuwa na Simba bora zaidi ya hivi sasa,” alisema Hassanoo.




