• ePaper
Thursday, April 16, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

WALIOTAJWA UBADHIRIFU RIPOTI YA CAG KIKAANGONI

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
April 2, 2026
in Habari, Kitaifa
0
WALIOTAJWA UBADHIRIFU RIPOTI YA CAG KIKAANGONI
0
SHARES
12
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

SELINA MATHEW Na HAMIS SHIMYE, Dodoma

SERIKALI imesisitiza kuwachukulia hatua waliotajwa au kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2025/2026.

Pia, imedhamiria kukuza uchumi wa nchi na wananchi kwa kuibua fursa za ajira na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuhakikisha inatekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 20250 kwa weledi.

Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba aliyasema hayo bungeni, jijini Dodoma, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

“Navielekeza vyombo vya dola na mamlaka za nidhamu kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki za kisheria, kinidhamu na kiutumishi kwa watakaobainika kuhusika na wizi wa fedha na mali za umma au hujuma,” alisema.

Dk. Mwigulu alisema amepokea hoja na mapendekezo yaliyowasilishwa na CAG, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), kwa ajili ya kuzifanyia kazi.

Aidha, Dk. Mwigulu alilihakikishia Bunge kwamba, serikali itafanyia kazi hoja zote kuleta ufanisi katika utendaji wa serikali.

Aliwaelekeza maofisa masuuli wa taasisi zote za umma zenye hoja kujibu hoja hizo na kufanyia kazi mapendekezo kwa mujibu wa sheria.

Alisema ili kuhakikisha uadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma, serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya ukaguzi na usimamizi.

Alifafanua kuwa, hatua zilizochukuliwa ni kuziwezesha taasisi za udhibiti, ukaguzi na uchunguzi kwa kufanya mabadiliko ya sheria mbalimbali ili kuziongezea nguvu, bajeti, rasilimaliwatu na vitendea kazi.

Alisema hatua hizo zimeziwezesha taasisi za udhibiti kutekeleza kikamilifu majukumu yao na kuwasilisha taarifa kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Machi 30, mwaka huu.

“Ukaguzi uliofanyika umewezesha kubaini upungufu katika usimamizi wa matumizi ya rasilimali za serikali na kujua thamani ya fedha katika miradi ya maendeleo,” alisema.

Vilevile, zimewezesha kuimarisha taasisi, uwajibikaji na uwazi katika matumizi, ufuatiliaji na kuchukua hatua stahiki.

ATAJA UIMARA WA RAIS

Waziri Mkuu alisema Rais Dk. Samia ni imara kwa uongozi mahiri na juhudi zake za kuwatumikia wananchi kwa mapenzi ya dhati.

Alisema kila mmoja ni shahidi wa kazi kubwa anayoifanya Rais Samia kuleta maendeleo na kuonesha dira, mwelekeo wa taifa hususani katika utekelezaji wa falsafa ya “Kazi na Utu – Tunasonga Mbele.

“Nitumie fursa hii kuwaomba wabunge wenzangu na wananchi wote kumwomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa Rais wetu nguvu, ulinzi, afya njema na kila lililo la heri katika kuwatumikia Watanzania,” alisema.

Aliongeza; “Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020; Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025; Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2021/2022 hadi 2025/2026; na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

AHADI ZA UCHAGUZI KUTEKELEZWA

Alisema Rais Dk. Samia alitoa ahadi mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo na kukuza ustawi wa wananchi zikiwemo alizoahidi kuzitekeleza ndani ya siku 100 ambazo zimetekelezwa baada kuchaguliwa tena kuongoza nchi.

“Ahadi hizo zililenga kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya, elimu, miundombinu na maji; kurasimisha sekta isiyo rasmi; na kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa biashara ndogo na za kati na uendeshaji wa kampuni changa ambapo sasa mambo yamekuwa mazuri,” alisema.

HALI YA UCHUMI

Alisema taarifa za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), uchumi wa dunia ulikua kwa wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2025, kiwango sawa na mwaka 2024.

“Mwenendo huu unatokana na kuongezeka kwa uwekezaji katika teknolojia mpya, hususani teknolojia ya akili unde, na juhudi za nchi mbalimbali kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea shughuli za uzalishaji katika uchumi wao.

 “Tanzania uchumi umeendelea kukua kwa kasi ambapo katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2025, pato halisi  la taifa limekua  kwa asilimia sita ikilinganishwa na asilimia 5.5 kipindi kama hicho mwaka 2024.

“Ukuaji huo umechangiwa na uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ikiwemo nishati, mawasiliano, usafiri na usafirishaji, huduma za kijamii na kuimarika kwa shughuli za uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi,” alisema.

Mfumuko wa Bei alisema nchi imeendelea kuwa na utulivu wa bei uliotokana na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha, kuimarika kwa bei ya mafuta na bidhaa katika soko la dunia na utulivu wa thamani ya sh. dhidi ya dola ya Marekani.

“Utulivu huo ulichangia kupunguza kasi ya ongezeko la bei ya bidhaa na huduma. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2025, wastani wa mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.5. Kiwango hicho kipo ndani ya lengo la nchi la asilimia tatu hadi tani,” alisema.

MAUZO NJE YA NCHI, AKIBA FEDHA ZA KIGENI

Alisema mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 16.3 Januari, 2025 hadi dola za Marekani bilioni 18.7 Januari, 2026 sawa na ongezeko la asilimia 12.7.

“Ongezeko hilo lilichangiwa na mauzo ya bidhaa mbalimbali ikiwemo dhahabu, tumbaku, kahawa, bidhaa za viwandani, utalii na huduma za usafirishaji.” Alisema.

Aidha, alisema Januari mwa huu, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 6.3 kiasi ambacho kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi 4.8 ikiwa juu ya kiwango kinachokubalika kimataifa.

Alisema mikopo iliyotolewa na benki kwa sekta binafsi imeongezeka kutoka asilimia 12.8 Januari, 2025 hadi asilimia 23.5 Januari, 2026  na imesaidia kuchochea shughuli za uwekezaji pamoja na uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo madini, biashara, kilimo, viwanda, usafirishaji na ujenzi.

MWENENDO MAPATO

Alisema serikali imeendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza makusanyo ikiwemo kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini; kupanua wigo wa kodi; na kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji wa mapato.

Kutokana na jitihada hizo, alisema sh. trilioni 26.63 zilikusanywa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari, 2026 kati ya lengo la kukusanya sh. trilioni 25.68, sawa na ufanisi wa asilimia 103.7 na ukuaji wa asilimia 19.27 ikilinganishwa na mapato ya sh. trilioni 22.32 yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/2025.

“Mapato hayo ya sh. trilioni 22.09 ni mapato yaliyotokana na kodi, sh. trilioni 3.78 ni mapato yasiyo ya kodi na sh. bilioni 754.26 ni misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo,” alisema.

Aidha, alisema kati ya fedha zilizokusanywa, sh. trilioni 12.28 zilitumika kutekeleza miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR); Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato; ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya na elimu; miradi ya maji; miundombinu ya nishati, usafiri na usafirishaji; na skimu za umwagiliaji.

Alisema serikali imeendelea kutekeleza mkakati wa taifa dhidi ya rushwa kwa kuweka mkazo wa kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi ambapo kupitia uchunguzi takribani sh. bilioni 60.231 ziliokolewa.

WAFANYAKAZI

Dk. Mwigulu alisema mwenendo wa malipo ya mishahara unaonesha kuwa lipo kundi la watumishi 7,447 ambao hadi Machi 26, mwa huu, walikuwa wamelipwa mishahara binafsi kwa gharama ya sh. bilioni 14.34.

Kutokana na hilo, alisema serikali itachukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhuisha sheria ya utumishi wa umma, sura 298 na kanuni zake kuhusu idhini ya utoaji wa kibali cha mshahara binafsi na kuhuisha waraka unaohusu watumishi watakaobadilishwa kazi kuendana na mahitaji.

Alisema watumishi hao walilipwa mishahara binafsi isiyoendana na majukumu wanayofanya.

Hatua nyingine aliyoitaja ni kuainisha mishahara ya watumishi wa umma na kupunguza tofauti kubwa ya viwango vya mishahara katika utumishi wa umma na sekta binafsi na kufanya mapitio ya waraka kuhusu utaratibu wa kushughulikia maombi ya mishahara binafsi kwa watumishi wa umma.

Alisema serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya kazi kwa kukamilisha na kutangaza amri ya kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kilichoongezeka kwa viwango tofauti kwa kuzingatia sekta, utekelezaji huo ulioanza rasmi Januari, 2026.

Alieleza kuwa watumishi wa umma ni nguzo ya msingi katika utekelezaji wa sera, dira, mipango na mikakati ya serikali.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa watumishi wa umma, Serikali ya Awamu ya Sita baada ya kuingia madarakani hadi Machi, mwaka huu imewapandisha vyeo na madaraja jumla ya watumishi 662,707 kati ya 678,115 waliopo katika orodha ya walipwa mishahara.

Kadhalika, katika kipindi hicho, serikali imebadilisha kada na miundo watumishi 42,515 kwa gharama ya sh. bilioni 3.52.

Vilevile, imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 148,137 yenye jumla ya sh. bilioni 248.52 na imeajiri watumishi wapya 155,008.

Aidha, alisema serikali itaendelea kuajiri, kupandisha vyeo na madaraja, kuongeza mishahara na kuwaendeleza watumishi ndani ya utumishi wa umma kadiri hali ya uchumi itakavyoruhusu.

Alisisitiza katika mwaka 2026/2027, serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kazi kwa wafanyakazi na waajiri kwa kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa majadiliano baina ya serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri na kuandaa mwongozo wa usajili, usimamizi na uratibu wa vyama vya wafanyakazi, vyama vya waajiri na mashirikisho.

Pia, alisema serikali imeendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na dawa za kulevya kupitia mikakati mbalimbali.

“Mikakati hiyo inalenga kupunguza upatikanaji, uhitaji, madhara na matumizi ya dawa za kulevya na imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kukabiliana na dawa za kulevya,” alieleza.

DIRA 2050

Waziri Mkuu Mwigulu alisema kwa miaka 25 iliyopita Tanzania iliongozwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo ilitafsiriwa katika mipango mitatu ya maendeleo ya taifa ya miaka mitano.

Alisema Julai 2025 Rais Dk. Samia alizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo itaongoza mipango ya maendeleo katika miaka 25 ijayo na kujenga taifa jumuishi, lenye ustawi kwa wote, haki na linalojitegemea.

“Mpango na bajeti itakayopitishwa na Bunge ni hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa nne wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano (2026/2027 – 2030/2031) na Dira 2050. Utekelezaji wa dira hiyo utaliwezesha taifa kuwa na uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja na wastani wa pato la mtu mmoja mmoja kuwa dola za Marekani 7,000 kwa mwaka ifikapo 2050,” alisema.

Alisema Dira ya 2050 ndiyo mwelekeo wa taifa letu ambapo kwa kuzingatia hilo kipaumbele cha serikali kitawekwa katika utekelezaji wa malengo kama yalivyobainishwa na dira hiyo.

“Suala hilo litawezekana ikiwa wadau wote watakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu vipaumbele vilivyoainishwa katika Dira 2050. Nitoe rai kwa viongozi wa serikali, dini, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wa Maendeleo kuhakikisha mipango yao inawiana na vipaumbele vya Dira 2050 na kuiunga mkono katika utekelezaji wake,” alibainisha.

UWEKEZAJI NA UENDELEZAJI SEKTA BINAFSI

Alisema serikali inaendelea kujenga uchumi unaoongozwa na uwekezaji kutoka sekta binafsi kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.

“Ili kuonesha dhamira ya dhati ya kutekeleza malengo hayo, katika mwaka 2025/2026, miradi 927 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 11.08 ilisajiliwa. Hatua hiyo, inaonesha kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji nchini na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” alisema.

Alisema serikali imeendeleza maeneo maalumu ya uwekezaji kuimarisha ukuaji uchumi wa viwanda na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi. Hatua zilizochukuliwa ni kutenga maeneo maalumu ya kiuchumi 34 na kuendelea na utekelezaji wa miradi 25 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 280.8.

“Miradi hiyo inatarajiwa kuzalisha mauzo ya nje yenye thamani ya dola za Marekani milioni 672.63. Mikakati mingine ni kupunguza tozo 245; kurekebisha sheria 28 na kuimarisha utoaji wa huduma kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania,” alieleza.

Akieleza kuhusu kilimo alisema serikali imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa chakula ambapo tani 23,783,128 zilizalishwa katika msimu wa mwaka 2024/2025 ikilinganishwa na mahitaji ya tani 18,279,054 kwa mwaka 2025/2026 na hivyo kuihakikishia nchi usalama kwa asilimia 130.

Pia, alisema serikali imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko mkoa Lindi kwa gharama ya sh. bilioni 280.58 ambazo ni fedha za ndani.

“Hadi Februari 2026, ujenzi umefikia asilimia 95. Kukamilika kwa bandari hiyo kutaimarisha utoaji wa huduma kwa wavuvi wakubwa na wadogo wa ndani na nje ya nchi, kuzalisha ajira 30,000 na kuboresha miundombinu ya uvuvi ili kupunguza kiwango cha umaskini,” alisema.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa uvuvi katika bahari kuu, serikali imenunua meli maalumu ya uvuvi kwa njia ya mishipi yenye urefu wa mita 22 iliyowasili nchini Februari mwaka huu.

“Meli hiyo itawezesha uvuvi katika Ukanda Maalumu wa Uchumi wa Bahari Kuu (EEZ) na kuongeza kiwango cha uvuvi, kukuza ajira na ujuzi hususani kwa vijana na kuongeza pato la wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema.

MALIASILI, UTALII, MADINI

Alisema sekta ya maliasili na utalii imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, ajira na pato la taifa likiwemo ongezeko la idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za taifa kwa asilimia 10.73 kutoka watalii 5,360,247 mwaka 2024 hadi 5,935,561 mwaka 2025.

“Mapato yatokanayo na utalii kutoka dola za Marekani bilioni 3.9 mwaka 2024 hadi dola za Marekani bilioni 4.4 Desemba 2025 sawa na ongezeko la asimilia 12.82,” alisema.

Alisema serikali imeendelea kuimarisha sekta ya madini kwa kutekeleza mikakati mbalimbali inayoongeza mapato ya serikali na fursa za ajira kwa wananchi.

Kuhusu sekta ya nishati ya umeme alisema ni injini ya kuharakisha na kurahisisha maendeleo ya kisasa inapotumika katika shughuli za uendeshaji wa viwanda, teknolojia na matumizi ya nyumbani.

Alisema serikali kwa kutambua hilo, imeendelea kutekeleza mikakati mahsusi ya kuhakikisha nishati ya umeme inayozalishwa nchini, inakidhi mahitaji yatokanayo na kasi kubwa ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.

MAFUTA, GESI, ARDHI

Alisema serikali imeendelea kusimamia na kusisitiza matumizi ya gesi asilia ambapo kuanzia Julai 2025 hadi Februari 2026, serikali imeongeza mtandao wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika viwanda, taasisi na nyumbani hadi kilomita 243.6 ikilinganishwa na kilomita 184.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2024/2025.

Aidha, alisema sekta ya ardhi ni muhimu kuwezesha uzalishaji na maendeleo ya sekta nyingine.

Hata hivyo, sekta hiyo imekumbwa na changamoto na migogoro mbalimbali yakiwamo maeneo mengi kutopimwa, ucheleweshaji wa hati, umilikishaji wa eneo moja kwa zaidi ya mtu mmoja na baadhi ya watendaji kutokuwa waaminifu.

“Serikali imeendelea kutatua migogoro iliyopo kupitia kliniki za ardhi, kamati za wataalamu, mabaraza ya ardhi na ziara za viongozi. Hadi Januari, 2026 migogoro 5,333 imetatuliwa, maombi ya umiliki 10,113 yalipokelewa na hatimiliki 7,182 ziliandaliwa pamoja na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 191,”alisema.

VIWANDA, BIASHARA

Alisema sekta ya viwanda na biashara inaendelea kuwa nguzo muhimu kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini kutokana na sekta hiyo kuwa kichocheo katika ukuaji wa pato la taifa, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Kwa upande wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji alisema ni msingi wa uchumi wa taifa na inachangia kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii lengo likiwa kuhakikisha huduma hiyo inakuwa bora.

“Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, vivuko na majengo ya serikali na kuwajengea uwezo wakandarasi wa ndani,” alisema.

Pia, alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya usafiri na usafirishaji, serikali imeendelea kuwekeza miundombinu ya kimkakati ya reli, anga, barabara na maji kwa kasi kubwa, kwa mafanikio.

Vile vile, alisema serikali katika kuendeleza sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari, imeanza kutekeleza ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika.

SEKTAZINGINE

Alisema serikali imeendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 (Toleo la 2023), mitaala iliyoboreshwa, mipango na mikakati mbalimbali.

“Lengo letu ni kuzalisha rasilimaliwatu wenye ujuzi na maarifa stahiki yatakayowezesha kumudu ushindani wa ajira na uwezo wa kujiajiri ndani na nje ya nchi,” alisema.

Alisema tathmini inaonesha wanafunzi 3,021,177 wanatarajiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2028 ambapo jumla  ya  gharama  zinazohitajika ni sh. trilioni 1.77.

Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 23,226; matundu ya vyoo 46,632; maabara 9,366; ajira mpya za walimu 40,192; ruzuku ya vitabu na uendeshaji pamoja na ruzuku ya mitihani na upimaji.

Kwa upande wa afya, lisema serikali imeendelea kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa utoaji wa huduma za afya nchini kwa kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma zinazotolewa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi taifa.

Kwa upande wa maji alisema ni muhimu kwa uhai wa viumbe na kwamba serikali imeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji na kuimarisha usimamizi wa rasilimali hiyo katika maeneo mbalimbali.

Alifafanua kwa upande wa vijijini, serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati yenye gharama ya sh. bilioni 349.59.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo, umefikia kati ya asilimia tano hadi 75 na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kutahudumia vijiji 225. 177.

“Kwa mwaka 2026/2027, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati itakayounganishwa kwenye gridi ya taifa ya maji inayohusisha kutoa maji maeneo yenye vyanzo vya uhakika kupeleka maeneo yenye uhaba.

“Vilevile, itaandaa mpango kabambe kwa lengo la kutoa mwelekeo wa muda mrefu wa kimkakati wa kitaifa kusimamia, kuendeleza na kutumia rasilimali za maji kwa njia endelevu,” alisema.

MABADILIKO TABIANCHI

Alisema serikali imeendelea kusimamia mikakati na mipango ya kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hatua hizo zinajumuisha kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuhamasisha upandaji miti, kuendeleza uwekezaji katika biashara ya kaboni na kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, alieleza kuwa, serikali imeendelea kuchukua hatua kuimarisha uratibu wa biashara ya kaboni kama nyenzo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha taifa na wananchi wananufaika na fursa zitokanazo na biashara hiyo.

Previous Post

TRA YANG’ARA ROBO YA TATU:MAKUSANYO YAVUKA MALENGO KWA KASI YA AJABU

Next Post

DK. MWIGULU AFUNGUKA MAANDALIZI AFCON 2027

Next Post
DK. MWIGULU AFUNGUKA MAANDALIZI AFCON 2027

DK. MWIGULU AFUNGUKA MAANDALIZI AFCON 2027

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

SINGIDA BS YAIPANIA SIMBA

SINGIDA BS YAIPANIA SIMBA

1 month ago
AL AHLY, YANGA UBORA UTAONGEA

AL AHLY, YANGA UBORA UTAONGEA

3 months ago

Popular News

  • MAFANIKIO YA KISHINDO SGR

    MAFANIKIO YA KISHINDO SGR

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • NYAMBUI AFUNGUKAAMANI KATIKA MICHEZO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • YANGA, MBEYA CITY KAZI IPO LEO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. MWINYI AFICHUA KUWA NA KIPAJI CHA SOKA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?