HAMISI SHIMYE Na FRED ALFRED, DODOMA
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa serikali kupunguza matumizi ya mafuta, kufuatia kupanda bei kwa bidhaa hiyo kutokana na vita ya Mashariki ya Kati.
Amesema ataanza kupunguza matumizi ya mafuta katika ofisi yake, ambapo kuanzia sasa, viongozi watatumia basi moja katika msafara wake, badala ya kila mmoja kutumia gari lake.
Rais Dk. Samia, alitoa maagizo hayo, alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni Ikulu, Chamwino, Dodoma.
Viongozi walioapishwa ni Profesa Palamagamba Kabudi, kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), akichukua nafasi ya marehemu William Lukuvi.
Viongozi wengine ni Reuben Kwagilwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Festo Dugange, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia elimu na Gerson Mdemu, Jaji wa Mahakama ya Rufani kuwa Mjumbe wa Turne ya Utumishi wa Mahakama.
“Ndani ya serikali tuna matumizi makubwa sana ya mafuta, magari ni mengi na safari ni nyingi, hivyo ni muhimu kuanza kupunguza matumizi ya mafuta.
“Nimeanza kwa upande wangu; kuanzia sasa, ninaposafiri, watendaji wa ofisi yangu nitakaoambatana nao, watatumia usafiri wa pamoja wa mabasi madogo ili kupunguza matumizi ya mafuta na gharama za uendeshaji katika kipindi hiki,” alisema Rais Dk. Samia.
Rais Dk. Samia, alisema vita inayoendelea Mashariki ya Kati, imeathiri nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, kutokana na kupanda kwa bei za mafuta na bidhaa.
Aliongeza kuwa, bei za mafuta zimefikia viwango vya juu katika baadhi ya nchi, hali iliyosababisha nchi hizo kupunguza shughuli za kiuchumi zinazotegemea matumizi ya nishati ya mafuta.
Alisema pamoja na kuwa Tanzania imekumbwa na athari hizo, bado ipo katika hali nafuu ya upatikanaji na hata bei za mafuta, ikilinganishwa na nchi nyingine.
Vilevile, alibainisha kuwa, serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya upatikanaji mafuta nchini na kuongeza kuwa, nchi ina akiba ya mafuta inayotosheleza matumizi ya takribani miezi mitatu.
Aliongeza: “Kiuhalisia hapa kwetu bei ziko chini kulinganisha na majirani wote wanaotuzunguka, licha ya kupunguza kodi katika nishati hiyo”.
Kwa upande wa Afrika, alisema baadhi ya nchi, zimetoa ruhusa kwa watumishi wa umma kufanya kazi nyumbani ili kupunguza matumizi ya magari kwenda ofisini kufuatia mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo duniani.
“Wananchi wajue upandaji wa bei ya mafuta mara zote unaenda na upandaji wa bei za bidhaa, wafanyabiashara ambao walinunua bidhaa muda mrefu, waangalie namna ya kuweka bei sawa,”alisema Rais Dk. Samia.
Aidha, Rais Dk. Samia, aliwataka wafanyabiashara nchini, kuwa waadilifu katika kupanga bei za bidhaa, hasa katika kipindi hiki cha kupanda bei ya mafuta duniani.
Rais Dk. Samia, alisema baadhi ya bidhaa zilizopo ghalani, zilinunuliwa kabla ya kupanda bei ya mafuta, hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuangalia namna ya kurekebisha bei bila kuwaumiza wananchi.
Pia, alionya dhidi ya matumizi mabaya ya hali ya soko ya kupandisha bei kupita kiasi, akisisitiza si bidhaa zote, zinapaswa kupanda kwa kiwango kikubwa.
Rais Dk. Samia, alisema kuna bidhaa zinazoingia nchini hivi sasa, ambazo zimeathiriwa moja kwa moja na kupanda bei ya mafuta, hivyo ni kawaida bei kuongezeka.
Alisema upandaji bei ya mafuta siyo tatizo la Tanzania pekee, bali ni changamoto ya dunia, ambapo aliwaomba wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki.
UTEUZI WA KABUDI
Akizungumzia uteuzi wa Profesa Kabudi, Rais Dk. Samia, alisema umetokana na uzoefu, maarifa na kuifahamu vyema historia ya nchi.
Alimtaka Profesa Kabudi kusimamia kwa karibu suala la uratibu wa shughuli za serikali na utekelezaji wa Dira ya ya Maendeleo ya Mwaka 2050.
“Baada ya Lukuvi kufariki, ilibidi kutafuta mtu kwa ajili ya kujaza nafasi yake, hivyo ilibidi kutafuta mtu mzima mzoefu na mwenye maarifa anayejua historia ya nchi. Hivyo tuliona Profesa Kabudi anafaa amefanya kazi nzuri ndani ya ofisi yangu.
Aliongeza: “Uwezo ulionao sina shaka kazi utaifanya kikamilifu ili kufikia malengo ambayo tunayatarajia. Nchi inaanza utekelezaji wa Dira ya 2050 hivyo inahitaji uratibu ndani ya serikali na sekta binafsi”.
Alisisitiza: “Tunahitaji sauti yenye ukomavu wa mambo, ndiyo maana umepewa jukumu hilo, hivyo kuelekea Dira ya 2050, tunaomba usaidie kuratibu serikali”.
KWAGILWA NA DUGANGE
Rais Dk.Samia alisema amemhamisha Kwagilwa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), ili akasimamie kikamilifu sekta ya mazingira.
Alisema hatua hiyo, imekuja baada ya kufuatilia ziara ya Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba na kuona Kwagilwa alivyofanya kazi vizuri.
Vilevile, alisema amemhamishia Dk. Dugange kwenda TAMISEMI ili akasimamie afya na elimu kutokana na uzoefu wake.
Hivi karibuni, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ilitangaza bei mpya ya mafuta ambapo petroli mkoani Dar es Salaam ilitoka sh. 2,864 hadi sh. 3,820 kwa lita.
Taarifa hiyo, ilieleza kupanda bei ya bidhaa hiyo, kunatokana na mabadiliko ya soko la kimataifa, ikiwemo ongezeko la bei ya mafuta ghafi na changamoto za usafirishaji kufuatia vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati kati ya Marekani, Israel dhidi ya Iran.




