Na ZIANA BAKARI
JAMII imehimizwa kuzingatia utaratibu wa kunywa maji ya kutosha kila siku kujikinga na athari za kiafya yakiwemo, maumivu ya kichwa, kupata choo kigumu au kukosa kabisa.
Pia, imeshauriwa kiafya mtu kunywa lita mbili hadi tatu za maji kwa siku, kwani husaidia kupunguza maumivu ya kichwa, mgongo, mafua na maumivu ya tumbo.
Ushauri huo ulitolewa na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mongo la Ndege iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Nuru Kanungila, alipozungumza na UHURU kusisitiza jamii kutumia muda mwingi kunywa maji.
“Naiomba jamii isisahau utaratibu wa kunywa maji ya kutosha kila siku, jitahidini kunywa angalau glasi nane, kila moja ikiwa na ujazo wa mililita 300, sawa na lita mbili au tatu kwa siku, pia asubuhi mtu anywe angalau glasi moja ya maji kabla ya kuanza shughuli zake.
“Tusipokunywa maji ya kutosha kuna uwezekano mkubwa wa kupata athari za kiafya yakiwemo, maumivu ya kichwa, kupata choo kigumu au kukosa kabisa, ngozi kukauka na chakula kutosagwa vizuri hivyo, mtu anapaswa kufahamu umuhimu wa maji mwilini,”alisema.
Akizungumzia baadhi ya mitazamo ya watu wanaodhani kuwa, hisia ya njaa daima humaanisha hitaji la chakula, Dk. Nuru, alisema siyo kweli, bali muda mwingine ni dalili ya mwili kuhitaji maji.
Dk. Nuru alisema jamii inapaswa kuwa na uangalifu wa kunywa maji ya kutosha katika kipindi hiki cha baridi, kwani baadhi ya watu wamepunguza unywaji wa maji kutokana na kuhisi hali ya ubaridi.
Akitaja faida za kunywa maji, Dk. Nuru alisema husaidia chakula kumeng’enywa vizuri, kulainisha ngozi na kuboresha uwezo wa kuona.
Pia, alisema maji huboresha afya ya ngozi kwa sababu seli zake huhitaji maji kulinda ngozi na kuisaidia kupambana na magonjwa na wakati mwingine husaidia kuifanya ngozi kuwa katika ubora wake.
Alieleza kuwa, maji husaidia katika utendaji kazi wa ubongo, kuondoa sumu na taka mwilini na kusaidia moyo kusukuma damu kwa ufanisi.
“Kitu kikubwa ni kuhakikisha mtu anaweka utaratibu wa kunywa maji kulingana na kiasi kinachotakiwa, bila kusahau kufanya mazoezi ambayo husababisha mtu kutoa jasho, hivyo kuongeza uhitaji wa maji mwilini,”alisema.
Aliongeza kuwa, watoto hawana kipimo maalumu cha kunywa maji, bali wanapaswa kupewa maji kadri wanavyohitaji na ulaji wa vyakula vyenye maji kwa wingi kama matunda unatakiwa kuzingatiwa.
Naye, Daktari wa Hospitali ya Kilosa mkoani Morogoro, Stamily Ally, alisema seli za mwili zinapokuwa zimeishiwa maji yapo madhara yakiwemo viungo vya mwili kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Alitaja viungo hivyo ni moyo, figo, ubongo na madhara mengine yanayoweza kupatikana ni kuathiri msukumo wa damu mwilini.
Pia, aliishauri jamii kila mmoja kuweka utaratibu wa kunywa maji mara kwa mara kwa siku kwa kiwango kinachotakiwa kiafya.
Maoni ya wananchi
Mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam, Julieth Jackson, aliishauri jamii kuweka utaratibu wa kunywa maji kwa siku, kwa sababu yanasaidia kukupa nguvu hususani wakati wa jua kali.
“Nimejiwekea utaratibu wangu ninapokuwa natoka nyumbani kwangu nahakikisha nabeba chupa yangu ya maji na hata watoto wangu nawasisitiza kunywa maji kwa kuwa najua umuhimu mkubwa wa maji katika mwili,”alisema.
Naye, Juma Khamis, mkazi wa Ilala, alisema jambo la muhimu hivi sasa ni kuweka utaratibu wa kupima afya mara kwa mara kwa kuwa, itasaidia ugonjwa kujulikana mapema na kuweza kuutibu.




