Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima amekemea uzushi unaenezwa na baadhi ya watu wenye nia ya kupotosha jamii, kuwa mwanaume akishikwa bega hupoteza sehemu zake za siri.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani yaliyofanyika wilyani Ubungo, yaliyolenga kuhamasisha ulinzi, malezi na ustawi wa watoto.
Dk. Gwajima aliamsha ari ya wanaume waliokuwepo kuonesha kwa vitendo kuwa uvumi wa kupotea nyeti, baada ya kushikwa bega ni uongo na utapeli kupitia wao kwa wao kushikana mabega wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando.
Katika maadhimisho hayo, wanaume hao walithibitisha taarifa hizo ni za uongo, kwa kuwa hakuna aliyepotelewa nyeti.
Dk. Gwajima aliwataka wananchi kupuuza taarifa za aina hiyo na kujikita katika shughuli za maendeleo, huku akihimiza umuhimu wa jamii kuwa na uelewa sahihi wa kupambanua taarifa za kweli na za upotoshaji.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Zanzibar linawashikilia watuhumiwa 40 kutokana na kuenea kwa uvumi unaodai baadhi ya watu wamekuwa wakisababisha wenzao kupoteza sehemu zao za siri kwa njia za kishirikina.
Imeelezwa taarifa hizo zisizo na ukweli zimezua hofu kubwa katika jamii na kusababisha madhara mbalimbali, ikiwemo majeruhi na kifo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo, jumla ya matukio 29 yaliripotiwa katika mikoa minne ya Zanzibar.
“Mkoa wa Mjini Magharibi unaongoza kwa matukio 22, ukifuatiwa na Kusini Unguja tukio moja, huku Kusini Pemba na Kaskazini Pemba kila mmoja ukiripoti matukio matatu,” ilieleza taarifa hiyo.
Jeshi hilo lilieleza hali hiyo imechangiwa na imani potofu na upotoshaji wa taarifa miongoni mwa wananchi.
Katika matukio hayo, lililoripotiwa Kaskazini Pemba lilisababisha kifo cha Hamad Othman Mwalimu (35), mkazi wa kijiji cha Jojo.
Taarifa hiyo ilisema watuhumiwa wa tukio hilo wanashikiliwa na hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa.
Ilieleza watu wote waliodai kupoteza sehemu zao za siri walifikishwa hospitali kwa uchunguzi wa kitabibu, ambapo madaktari walithibitisha hawakuwa na tatizo lolote kiafya.
“Hali hii inaonesha wazi kuwa madai hayo hayana ukweli wowote na ni uvumi unaochochea taharuki isiyo ya lazima katika jamii,” ilieleza taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi lilitoa wito kwa wananchi kupuuza uvumi huo na kuacha kusambaza taarifa zisizothibitishwa na kuonya mtu atakayebainika kusambaza taarifa za uongo kwa makusudi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, liliwahimiza wananchi kutoa taarifa sahihi kwa vyombo vya dola na kuepuka kujichukulia sheria mkononi, kudumisha amani na utulivu uliopo.




