Na MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya DP World imesema imepata mafanikio makubwa tangu ilipowekeza katika Bandari ya Dar es Salaam mwaka 2024.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano wa Nje wa DP World, Elitunu Mallamia, alisema mafanikio yao yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na kampuni hiyo.
Amesema uwekezaji wa awali wa dola milioni 125 kati ya dola milioni 250 zilizowekezwa na DP World, umechangia mafanikio hayo.
Amesema dola milioni 125 zilizowekezwa na DP World tangu Aprili 7, 2024 ilipoanza kazi, zimechochea ukuaji uchumi wa nchi kupitia bidhaa mbalimbali zinazoletwa nchini.
Mallamia amesema DP World imemudu soko la dunia kwa kuwa bandari inapokea meli nyingi na kubwa zinazoleta mizigo.
Pa, amesema DP World imeboresha mifumo ya TEHAMA ambayo imekuwa na manufaa, ambapo mifumo na taasisi zingine ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inasomana.
“Tunafanya kazi nzuri na TRA, timu inayofanya kazi na bandari inatupa ushirikiano mzuri. Mtaona TRA imekuwa ikivuka malengo ya ukusanyaji mapato, hii inatokana na mchango wa bandari, kwa sababu takribani asilimia 30 ya mapato yao yanatoka hapa bandarini,”amesema Mallamia.
Meneja huyo amesema kitendo cha mifumo ya kitaasisi kusomana, kumeongeza kasi ya utoaji makontena katika bandari hiyo.
Amesema mwaka 2025 walitoa makontena 323,837 ikiwa ni ongezeko la asilimia 96, kulinganisha na mwaka 2023 walipotoa makontena 165,545.
“Mzigo wa bidhaa mbalimbali kwa mwaka 2023, terminal ilifanya tani milioni moja, laki mbili na ishirini. Mwaka 2025 tulifanya tani milioni mbili, laki mbili na thelathini ambayo ni sawa na asilimia 81 zaidi
“Kwa mazao ya kichele hapa nazungumzia ngano, mchele, chumvi, mbolea na nafasi mbalimbali mwaka 2023 terminal ilifanya tani milioni tatu, laki tano na thelathini. Mwaka 2025 tulifanya tani milioni tatu, laki nane na tisini ikiwa ni ongezeko la asilimia 10,”alisema Mallamia.
Malamia alisema katika robo ya mwaka huu, DP World ilihudumia makontena 110,199 kulinganisha na robo mwaka ya mwaka jana walipohudumia makontena 57,401.
Aidha, alisema DP World imeajiri zaidi ya wafanyakazi 480, ambapo raia wa kigeni 15, awali kulikuwa na watumishi 250 kabla ya kubinafsishwa.
Mallamia alisema uwekezaji uliofanywa na DP World ikiwemo kuajiri wazawa, umeleta ufanisi ambapo meli za mizigo zinakaa kati ya siku saba hadi 11, kulinganisha na awali ambapo meli zilichukua muda mrefu.
“Hivi sasa mtaona kumekuwa na idadi kubwa ya bandari kavu, ni kwasababu hivi saa mzigo haukai bandarini, meli ikifika mzigo unapakuliwa, inakaa muda mfupi na mizigo inakwenda katika sehemu husika,”alisema Mallamia.
Pia, alisema ndani ya miaka miwili hadi mitatu, mkakati wa DP World ni kuboresha yadi za bandari ili kupokea mzigo mkubwa zaidi.
Vilevile, kujenga idadi kubwa ya maghala ya kuhifadhi mizigo kwa kiwango kikubwa likiwemo eneo la Kwala mkoani Pwani.
Alisema mkakati mwingine ni kuweka mashine bora za kisasa ambazo zitakuwa na kazi ya kupakua mizigo lengo ni kuweka udhibiti wa bidhaa.
Mallamia alisema wataongeza kasi ya kuimarisha ulinzi kwa kuweka miundombinu madhubuti, pia kuboresha matumizi ya TEHAMA.



