Na AMINA KASHEBA
SERIKALI imesema pambano la ngumi za kulipwa la ‘Knockout ya Mama’ litakuwa chachu ya kufungua milango ya mabondia wakubwa kutoka mataifa mbalimbali duniani, kuja nchini.
Pamoja na hilo, pambano hilo litasaidia kukuza tasnia ya ndondi na kuongeza fursa kwa mabondia hapa nchini
Hayo yalisemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, wakati wa ukaguzi wa maandalizi ya pambano la kimataifa kati ya Ibrahim Mafia na +Alvin Camique kutoka Ufilipino.
Mafia na Camique watadundana katika pambano la marudiano la raundi 10, litakalofanyika Ukumbi wa EACLC uliopo Ubungo, Dar es Salaam.
Katika pambano la awali lililofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 10, mwaka jana, Mafia alipoteza kwa TKO raundi ya nne.
Makonda alisema pambano hilo litaitangaza Tanzania kimataifa na kuwavutia mabondia wenye majina makubwa kuja nchini kupambana na mabondia wetu.
Waziri huyo alisema ujio wa mabondia kutoka Uingereza, Urusi, Marekani, Ujerumani na Falme za Kiarabu utasaidia kukuza tasnia ya ndondi pamoja na kuongeza fursa kwa mabondia hapa nchini.
“Pambano hili linapaswa kufungua milango kwa mabondia wakubwa kuja nchini, si tu kushiriki mashindano bali kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia mambo mazuri yaliyopo,” alisema Makonda.
Aidha, Waziri huyo alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo na kuwaunga mkono mabondia wa ndani watakaopanda ulingoni kupeperusha bendera ya nchi.
Akizungumzia maandalizi ya pambano lake, Mafia alisema hatakubali kupoteza pambano baada ya kufanya mazoezi makali chini ya kocha Kanda Kabongo.
“Nimejifua vikali kwa lengo la kulipa kisasi, kocha ameniongoza kufanya mazoezi makali ambayo naamini yatanisaidia kumtwanga mpinzani wangu,” alitamba Mafia.
Mwanamasumbwi huyo alisema amenolewa na makocha wawili ambao wamempa mbinu tofauti za kumchapa Camique.
Kocha wa bondia huyo, Kabongo, alisema katika pambano la marudiano, mashabiki wa ndondi wajiandae kushangilia ushindi wa bondia wake ambaye amepikwa kikamilifu.
Kabongo aliwaomba Watanzania na wadau wa masumbwi kujitokeza kwa wingi kumshangilia Mafia.




