Na ABDUL DUNIA
UKUTA wa timu za Yanga na Azam FC zimeonesha kuwa kinara wa kutoruhusu mabao mengi hadi sasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu huu.
Kabla ya ligi kusimama kwa lengo la kupisha michuano ya Kombe la Muungano, inayoendelea Zanzibar, tayari timu hizo zilikuwa zimecheza mechi 19.
Katika mechi hizo, Yanga inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 47 wakati Simba inafuatia baada ya kukusanya alama 42, Azam FC yenye pointi 37 inashika nafasi ya tatu huku Singida Black Stars ikiwa nafasi ya nne kwa alama 29.
Pamoja na msimamo huo, Yanga na Azam FC zimeonesha kuwa timu zenye safu bora ya ulinzi hadi sasa, ambapo Yanga iliruhusu mabao matatu huku Azam FC ikifungwa mabao matano.
Kwa mujibu wa msimamo, wababe hao wanafuatiwa na Simba iliyoruhusu mabao saba, Mashujaa mabao 17, TRA United na Pamba Jiji kila moja ikifungwa mabao 18.
Singida Black Stars na JKT Tanzania kila moja imeruhusu mabao 20, Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar kila moja imefungwa mabao 21 wakati Coastal Union na Namungo kila moja ikiruhusu mabao 22.
Tanzania Prisons imeruhusu mabao 23, Fountain Gate imefungwa mabao 26 huku KMC na Mbeya City kila moja ikiruhusu mabao 30.




