Arusha
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa waepuke migogoro ambayo imekuwa chanzo kwa baadhi ya miradi kukwama.
Dk. Mwigulu alitoa wito huo alipofungua Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha.
“Twendeni tukatimize wajibu wetu, tuache migawanyiko kwa sababu hayo siyo matarajio ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Tuepuke migogoro, mameya, madiwani na wenyeviti, kuna baadhi ya maeneo tunachelewa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa sababu ya migogoro inayotengeneza migawanyiko.
“Ondoeni utaratibu wa kuchagua Makamu Mwenyekiti kila mwaka kwani jambo hili linaleta makovu. Nimeshamuagiza Waziri wa TAMISEMI amuandikie Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ni sheria ifutwe, kama ni kanuni ibadilishwe, lakini kama mkutano huu una mamlaka, utaratibu wa kuchagua Makamu Mwenyekiti kila mwaka ufutwe,” alisisitiza.
Alisema utaratibu wa sasa unawanyima fursa viongozi walioko madarakani kujielekeza katika masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi, badala yake wanajikuta katika harakati za kugawana vyeo.
“Wenyeviti wanajikuta wanaongoza watu waliogawanyika na hili halileti tija. Hivi sasa walioko madarakani bado wanajifunza kazi, tayari wengine wameshaanza kampeni kuwania nafasi zao,” alisisitiza.
Aliwataka viongozi watakaochaguliwa kesho wahakikishe wanakuwa chachu ya maendeleo na kusimamia maslahi ya wananchi kwa vitendo na kuongeza:
“Kwa viongozi mtakaochaguliwa, mhakikishe mnakwenda kusaidia jumuiya yetu na maslahi ya wananchi, muwe viongozi wanaopinga rushwa kwa vitendo. Mhakikishe mnakuwa daraja la kuleta maendeleo kwa wananchi na kuitafsiri Dira ya 2050,” alieleza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alisema sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa 2050, akiwataka viongozi wa halmashauri wawe wasimamizi na walezi wa mazingira rafiki ya uwekezaji.
“Katika DIRA 2050, sekta binafsi imepewa asilimia 70 za kutoa mchango. Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri mkawe walezi wa sekta binafsi. Mkitanguliza kulea sekta binafsi mtakuza mapato. Mkitanguliza mapato mtaua sekta binafsi. Sekta binafsi tunaitegemea sana katika kutengeneza ajira kwa kinamama na vijana,” alisisitiza.
Aliwataka viongozi hao kutojihisi dhaifu katika utekelezaji majukumu yao, akisisitiza kuwa serikali inatambua mchango wao mkubwa licha ya changamoto chache zinazojitokeza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwahakikishia wajumbe wa mkutano kuwa serikali inaendelea kulifanyia kazi suala la kuboresha maslahi ya madiwani kama ambavyo liliwasilishwa na Mwenyekiti wa ALAT anayemaliza muda wake, Murshid Ngeze.




