• ePaper
Wednesday, April 29, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

RAIS DK. SAMIA AFUNGUA UCHUMI WA BAHARI

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
April 26, 2026
in Habari, Kitaifa
0
RAIS DK. SAMIA AFUNGUA UCHUMI WA BAHARI
0
SHARES
4
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na ATHNATH MKIRAMWENI

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza mikakati mikubwa ya kunufaika na uchumi wa bahari ukiwemo kununua meli, kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na kuunganisha teknolojia ya kisasa.

Rais Dk. Samia aliainisha mikakati hiyo jijini Dar es Salaam, katika hafla ya uzinduzi wa meli ya kwanza ya uvuvi katika bahari kuu, uliofayika katika viwanja vya Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni na kusema lengo ni kuimarisha sekta ya uvuvi kufanya vizuri katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

BANDARI ZA UVUVI

Kuhusu bandari za uvuvi, alisema serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu muhimu zikiwemo bandari hizo za uvuvi na kubainisha kuwa, ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa umefikia hatua ya juu ya ukamilishaji.

Rais Dk. Samia alieleza kuwa, pamoja na mradi huo wa Kilwa, serikali ina mpango wa kujenga bandari nyingine ya uvuvi katika eneo la Bagamoyo, hatua itakayopanua uwezo wa nchi katika shughuli za uvuvi wa bahari kuu.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa bandari hiyo utaenda pamoja na kuanzishwa kwa eneo huru la kiuchumi litakalohusisha shughuli za uvuvi na kuimarisha viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi.

Rais Dk. Samia alisema hatua hizo, zinalenga kuongeza uzalishaji, kufungua fursa za ajira kwa wananchi na kuimarisha usalama wa chakula kupitia upatikanaji wa mazao ya baharini.

UNUNUZI MELI NNE

Aidha, alibainisha kuwa serikali inaendelea na mpango wa kununua meli nyingine nne za uvuvi, meli ya mafunzo na utafiti, kwa lengo la kujenga uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu.

Alisisitiza kuwa, uwekezaji huo utaenda pamoja na kuimarisha mafunzo, utafiti wa kitaalamu na mifumo ya usimamizi wa sekta kuhakikisha rasilimali za bahari na maziwa zinasimamiwa kwa ufanisi kwa kuzingatia misingi endelevu.

“Hatua zinaendelea za ununuzi wa meli nyingine nne za uvuvi na meli ya mafunzo ya utafiti kama waziri alivyosema hapa, tutafanya hivi kujenga uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu,” alisema.

KUFUFUA TAFICO

Rais Dk. Samia alisema serikali imedhamiria kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari kuu na kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa taifa.

“Hatua hii inalenga kurejesha uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu, ambao kwa muda mrefu umefanywa na kampuni za nje, hali iliyopunguza manufaa kwa wananchi na mapato ya serikali,” alisema.

Alisema kufufuliwa kwa TAFICO kutaendana na uwekezaji wa vifaa na teknolojia za kisasa, kuongeza ufanisi na ushindani wa shirika hilo katika shughuli za uvuvi wa kimataifa.

Rais Dk. Samia alisema kupitia mkakati huo, nchi itadhibiti vyema rasilimali zake za bahari na kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya Watanzania, huku ajira zaidi zikitarajiwa kufunguliwa kwa vijana.

Mkuu wa nchi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za serikali katika kuhakikisha shirika hilo linaendeshwa kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

Pia, alisema serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu na mifumo ya usimamizi kuhakikisha TAFICO inakuwa imara na endelevu, huku mafanikio yake yakitegemea nidhamu na matumizi sahihi ya rasilimali.

Aliongeza kuwa, hatua hiyo ni ya kimkakati katika kulinda rasilimali za taifa na kukuza uchumi wa buluu, huku ukitarajiwa kuongeza tija na mchango wa sekta ya uvuvi katika maendeleo ya nchi.

Rais alieleza kuwa kwa muda mrefu uvuvi wa bahari kuu, umekuwa ukifanywa na meli na kampuni kutoka nje ya nchi, hali iliyopunguza mapato ya taifa na manufaa kwa wananchi.

MAELEKEZO MATANO

Pia, Rais Dk. Samia alitoa maelekezo matano kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, yanayotarajiwa kuimarisha sekta ya uvuvi na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

Mosi, Rais Dk. Samia alisisitiza kuwa, watendaji wa wizara wanapaswa kushikamana na kwenda kwa kasi katika utekelezaji wa majukumu yao, kufanikisha malengo ya mageuzi ya sekta hiyo.

Alieleza kuwa, dhamira ya serikali ni kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinawanufaisha wananchi na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi.

Pili, alielekeza umuhimu wa kutunza na kuendesha kwa ufanisi vyombo vinavyonunuliwa kwa shughuli za uvuvi, vidumu na kuleta manufaa ya muda mrefu.

Alionya kuwa, bila usimamizi mzuri wa rasilimali hizo, juhudi za serikali katika kuwekeza katika sekta hiyo zitakosa tija.

Tatu, Rais Dk. Samia alitambua changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo na kuagiza wizara kuendelea kuzishughulikia kwa kuwapatia mitaji, teknolojia na masoko.

Alisema hatua hiyo itawawezesha wavuvi kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.

Nne, alisisitiza utoaji wa elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha kwa wavuvi wanufaike zaidi na shughuli zao, akieleza elimu hiyo itasaidia kuongeza thamani ya kazi mazao na kuboresha maisha yao.

Tano, Rais Dk. Samia alielekeza kuimarishwa kwa mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Alisisitiza kuwa, uvuvi endelevu ni muhimu kwa kulinda rasilimali za maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Rais Dk. Samia alieleza kuwa, hatua hiyo ni mwanzo wa mageuzi makubwa katika sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla.

WAZIRI BASHIRU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dk. Bashiru Ally, alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya uvuvi, umeanza kuzaa matunda hususan kupitia maendeleo ya miundombinu ya bandari ya uvuvi ya Kilwa na masoko ambayo yamefikia asilimia 97 ya ukamilishaji, huku hatua iliyobaki ikiwa ni upimaji wa mitambo kabla ya uzinduzi rasmi.

Dk. Bashiru alisema hatua ya kuanza kufikia dhamira ya nchi kunufaika na rasilimali za uvuvi wa bahari kuu ni kubwa, baada ya jitihada za muda mrefu hivyo uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa samaki kwa soko la nje na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Pia, serikali inaendelea na uwekezaji mkubwa kupitia mradi wa kuendeleza usimamizi wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji wenye thamani ya dola milioni 117, utakaotekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kwa miaka mitano,

Balozi Dk. Bashiru alisema mradi huo umelenga kujenga miundombinu, kuimarisha tafiti na mafunzo na kuwezesha upatikanaji wa wataalamu kuifanya Tanzania kushiriki kikamilifu katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.

Previous Post

TUUNGANE KUJENGA NCHI – BALOZI NYALANDU

Next Post

BALOZI NCHIMBI ATAKA RAIA KUILINDA AMANI

Next Post
BALOZI NCHIMBI ATAKA RAIA KUILINDA AMANI

BALOZI NCHIMBI ATAKA RAIA KUILINDA AMANI

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

BALOZI DK.  NCHIMBI ATAJA MISINGI YA CCM

BALOZI DK.  NCHIMBI ATAJA MISINGI YA CCM

8 months ago
MIGOGORO ARDHI MFUPA MGUMU

MIGOGORO ARDHI MFUPA MGUMU

2 months ago

Popular News

  • TANZANIA YAJINADI KIMATAIFA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

    TANZANIA YAJINADI KIMATAIFA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • VYALENGA KUIJENGA JAMII KIUCHUMI NA KIROHO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • KUVUMILIANA MUHIMU

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • WAZIRI SANGU ABAINISHA HIFADHI SKIMU INAVYOENDA KUBADILI MAISHA YA WATANZANIA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TUCTA: WAAJILI WATEKELEZE NYONGEZA YA KIMA CHA MISHAHARA SEKTA BINAFSI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?