Na ABDUL DUNIA, Pemba
BAADA ya kusubiri kwa miaka mitano sasa, Simba imetwaa taji lake kubwa la kwanza kufuatia kuifunga Azam FC bao 1-0 katika fainali ya Kombe la FA.
Simba ilivunja mwiko huo wa muda mrefu katika mtanange huo uliopigwa jana kuanzia saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Gombani, Pemba.
Bao la kujifunga la Yahya Zayd dakika ya 61 katika harakati za kuokoa faulo iliyopigwa na Neo Maema lilitosha kuipa ushindi Simba.
Dakika sita baadaye, kiungo nyota wa Azam FC, Feisal Salum maarufu Fei Toto, alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumshambulia kwa mikono Libasse Gueye wa Simba baada ya vuta nikuvute.
Baada ya kuonyeshwa kadi hiyo, Fei Toto na baadhi ya wachezaji na benchi la ufundi la Azam FC walionyeshwa kutofurahishwa na uamuzi huo kabla ya mchezaji huyo kuondoka uwanjani.
Licha ya kupata kadi nyekundu, Azam FC iliendelea na aina yake ya soka huku ikitengeneza baadhi ya nafasi ambazo ilishindwa kuzitumia kwa umakini.
Kabla ya jana, Wekundu hao wa Msimbazi mara ya mwisho kubeba taji kubwa (Ligi Kuu Bara au Kombe la FA) ilikuwa miaka mitano iliyopita, ikitwaa FA mwaka 2021 kwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Yanga.
Simba ilikuwa ya kwanza kuingia uwanjani kupasha misuli joto ikifanya hivyo saa 10:16 jioni na kutoka saa 10:41 wakati Azam FC ikiingia saa 10:17 na kutoka saa 10:41.
KOCHA WA SIMBA
Akizungumza baada ya mchezo huo, Steve Barker alisema anashukuru kushinda taji hilo na anawashukuru viongozi, wanachama na wachezaji kujituma na kupata ushindi huo.
MAGORI
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Crescentius Magori amesema mwaka huu walikutana na changamoto nyingi na wana imani mwanga wa mataji umeanza kurudi katika klabu yao.
AHMED ALLY
Ahmed Ally ambaye ni msemaji wa klabu ya SImba alisema ana furaha baada ya kukosa vikombe katika kipindi cha miaka minne mfululizo.
“Tumesubiri kwa muda mrefu, kama tungekosa hili kombe ingekuwa miaka mitano, tumejipata msimu huu tumechukua kombe hili, tunamshukuru Mungu,”alisema
Pia, alitangaza leo kuwepo paredi kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na watapita mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo mitaa ya Twiga na Jangwani ambapo alisema watakuwa na jambo lao nusu saa na kisha kufika fukwe za Coco Beach.
CLATOUS CHAMA
Clatous Chama alisema mchezo ulikuwa wa ushindani sana na iliwachukua muda kutwaa taji hilo.
“Mchezo ulikuwa mgumu, ukweli Azam ni timu nzuri na tumeshindana nao, tumeshinda tunashukuru Mungu,” alisema Chama.
KIBA DAKIKA NNE TU
Msanii nyota wa bongo fleva, Ali Kiba ametumia dakika nne kufanya onyesho la muziki kabla ya mchezo wa fainali ya Kombe la FA kati ya Simba na Azam FC.
Katika mtanange huo uliopigwa Uwanja wa Gombani, Pemba, Kiba ametumia dakika hizo kuimba nyimbo mbili pekee ambazo ni Utu na Finale.
Simba: Mamadou Kassali, David Duchu, Nickson Kibabage, Ismail Toure, Rushine De Reuck, Yusuph Kagoma, Libasse Gueye, Neo Maema, Elie Mpanzu, Clatous Chama na Anicet Oura.
Azam FC: Aishi Manula, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Lameck Lawi, Fuentes Mendoza, Himid Mao, Abdul Sopu, Yahya Zayd, Jephte Kitambala, Feisal Salum na Idd Selemani.




