Emmanuel Mohamed
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimefanya mabadiliko ya sekretarieti ngazi taifa, kwa kumteua Aggrey Mwanri kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, akichukua nafasi ya John Mongella, huku Abdi Mohamed Abdi akiwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, akimrithi Dk. Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa mikutano Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Unguja, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, alisema katika mabadiliko hayo, Paul Chacha amekuwa Katibu wa NEC Oganaizesheni akimrithi Issa Haji Ussi ‘Gavu,’ na Jamal Kassim amekuwa Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, akichukua nafasi ya Joshua Mirumbe.
Katika nafasi moja ya Mjumbe wa Kamati Kuu, Rahma Kassim Ali ameteuliwa kujaza nafasi ya Leila Ngozi, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’.
PONGEZI KWA MARAIS SAMIA, MWINYI
Katika hatua nyingine, Kihongosi alisema CCM imempongeza Mwenyekiti wake, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi imara, madhubuti, unaojali maendeleo ya Watanzania na kusisitiza: “Chama kinajionea kasi ya maendeleo ndani ya Jamhuri ya Tanzania.
“Kazi inafanyika kwa weledi, sekta zote zikiwemo afya, miundombinu ya barabara, sekta ya maji, elimu na nishati, hivyo CCM inampongeza mwenyekiti kwa kuonyesha uongozi imara ambao una matokeo chanya.”
Alifafanua, “CCM inampongeza Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya Zanzibar, leo tumeona mabadiliko makubwa, barabara zinajengwa kwa kasi, Chama kinazipongeza serikali zake zote mbili,” alisema.
Alisema serikali zinafanya vizuri katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030, kwa kuhakikisha mambo yaliyoahidiwa yanatekelezwa.
UCHAGUZI WA KIDEMOKRASIA
Kihongosi alisema katika kikao cha Halmashauri Kuu, wajumbe walijadili maandalizi ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake, ambao unatarajiwa kufanyika mwakani, baada ya kikao hicho kupitisha ratiba na miongozo ya uchaguzi huo.
“Tunataka uchaguzi wa kidemokrasia, uchaguzi huru na wa heshima kama ambavyo CCM imekuwa ikijitanabaisha kuwa na uwezo mkubwa wa kusimamia uchaguzi wake wa ndani, katika hali ya utulivu na amani, ”alifafanua.
REKODI
Mwanri aliwahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi wa CCM, nafasi ambayo aliteuliwa mwaka 2006, wakati sekretarieti mpya ya CCM ilipoundwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama wakati huo, Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Chacha, hadi uteuzi wake unafanyika jana, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Abdi alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Zanzibar huku Jamal akiwahi kushika nafasi ya Waziri wa Fedha Zanzibar.




