Na MWANDISHI WETU
JOTO limezidi kufukuta katika klabu ya Simba baada ya viongozi wake wa juu kutofautiana kuhusu kutangazwa Baraza jipya la Wadhamini la miamba hiyo ya soka nchini.
Simba kupitia Mwenyekiti wake, Murtaza Mangungu, juzi ilitangaza baraza jipya la wadhamini lililoundwa na wajumbe saba ambao ni Salim Abdallah ‘Try Again’, Dk. Bill Kiwia, Alhaj Ismail Mohamed, Amos Makalla, Adam Mgoi, Hamad Abdallah na Hassan Hasanoo.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Makalla alitangaza kutokubaliana na uteuzi huo akidai haukufuata katiba ya klabu ya Simba.
Baada ya Mangungu kutangaza baraza hilo, Simba kupitia mitandao ya kijamii, ilichapisha taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori, ambaye alidai kuwa kikao kilichotangaza baraza hilo siyo kikao rasmi cha Mkutano Maalumu wa klabu hiyo.
Magori kupitia taarifa hiyo, alidai kuwa maamuzi yote yaliyotangazwa katika kikao hicho ni batili na kinyume cha katiba ya Simba.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Simba ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho 2026, ibara ya 23, Mkutano Maalumu utaandaliwa na Mwenyekiti wa klabu kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi,” ilieleza taarifa ya Magori.
Pia, Magori aliweka wazi kuwa, jana kulitarajiwa kuwa na kikao cha Bodi ya klabu hiyo kujadili ajenda ya Mkutano Mkuu Maalumu wa wanachama wa miamba hiyo.
Kufuatia kauli ya Magori, jana Mangungu aliweka wazi kuwa, alitangaza baraza hilo jipya baada ya kushauriana na Rais wa Simba, Mohamed Dewji.
“Mohamed ndiye aliyempendekeza, kuhusu kumshauri au hakumshauri hilo sio jukumu langu ,lakini hata hivyo anayo haki ya kukubali au kukataa kwa sababu bado hajapewa barua ya uteuzi,”
Mangungu alikiambia kituo kimoja cha redio, jijini Dar es Salaam.
Alifafanua kuwa, Mo alichangia majina manne na majina mengine matatu yametoka upande wa wanachama ambao unaongozwa na Mangungu.
SIMBA INAONGOZWA NA BODI-MAGORI
Akizungumza kwa njia ya simu na kituo cha redio, Magori alisisitiza kuwa, Simba inaongozwa na bodi na siyo kitu kingine.
“Hayo majina yametolewa kwa uhalali wa nani? au kwenye bodi ipi?, anajua kikao kinafanyika Jumatatu saa 9 mchana (jana) juu ya jambo hilo,” alisema.
Aliongeza kuwa, ameshangaa baada ya baraza jipya kutokuwa na Athuman Kapuya na Ramesh Patel.
“Hili jambo halivumiliki hata kidogo, katika hili, tutalifanyia kazi na tunajua wapo watu wanawatumia hawa.
“Watuoneshe katiba inavyosema, hili la ajenda hizo linajadiliwa Jumatatu (jana), kikao kimeitishwa tangu Ijumaa, leo unakuja kuondoa watu bila ya idhini ya bodi, hili halivumiliki,”alisisitiza Magori.
UHURU ilipomtafuta Mo Dewji kuthibitisha kama anaungana na Mangungu au Magori, simu yake iliita bila majibu.




