Na NASRA KITANA
NI mchezo wa kusaka heshima na rekodi, wakati Simba na Azam FC zitakapopambana leo katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba iliyopo nafasi ya pili na alama 15 katika msimamo, itakuwa ugenini kuikabili Azam FC inayoshika nafasi ya tatu na pointi 14, katika mechi itakayochezwa dimba la Azam Complex, Dar es Salaam.
Mara ya mwisho timu hizo zilichuana katika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), Julai 4, mwaka huu, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, na kutwaa kombe.
Mechi hiyo maarufu kama ‘Mzizima Derby’ inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na rekodi za ushindani za vigogo hivyo.
Tangu kuanza kwa ligi msimu huu, Azam haijapoteza mechi yoyote, imepata ushindi katika michezo minne na kutoka sare mara mbili.
Ilianza ligi kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania kisha ilishinda mabao 2-1 ilipoumna na TRA United kabla ya kuifunga Pamba Jiji mabao 2-1, ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Geita Gold, kabla ya kushinda mabao 2-0 ilipopepetana na Kagera Sugar na kuifunga Namungo FC mabao 2-0.
Simba ilianza ligi kwa nguvu baada ya kushinda mechi zote za awali, ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na ikaifunga Pamba Jiji mabao 2-1.
Wekundu hao wa Msimbazi walipata ushindi mwingine wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars kisha iliichapa Coastal Union bao 1-0 Coastal Union kabla ya kuifunga Geita Gold mabao 2-0.
Akizungumzia maandalizi ya pambano hilo, Kocha wa Simba, Steve Barker, alisema anajua mchezo utakuwa mgumu lakini atakipanga kikosi chke kupata ushindi.
Barker alisema pamoja na kutarajia ushindani, Simba ipo tayari kupambana kupata matokeo mazuri ugenini.
“Tunaenda katika mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa, naamini wachezaji wangu watapambana na kuvuna alama tatu muhimu na kuendelea kuweka rekodi ya matokeo mazuri msimu huu,” alisema Barker.
Kocha huyo alisema Azam siyo timu ya kuibeza kwani ina kikosi chenye ushindani na kinaweza kufanya lolote katika dimba la nyumbani kama Simba haitaizuia.
Nyota wa Simba, Nathaniel Chilambo, alisema wanajua umuhimu wa mchezo dhidi ya Azam na wamejipanga kupata matokeo mazuri.
Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, alisema utakuwa mchezo wenye ushindani, Simba imetoka kushinda idadi kubwa ya mabao, katika michuano ya kimataifa, lakini hana hofu na uwezo wa wapinzani, ataiongoza timu yake kutoa upinzani na kubakiza alama tatu nyumbani.
“Tunaenda kucheza na Simba ambayo imeanza ligi kwa kufanya vizuri, tunahitaji pointi tatu, nimewakumbusha wachezaji umuhimu wa kushinda mechi hiyo,” alisema Ibenge.
Mlindamlango wa timu hiyo, Aishi Manula, alisema kikosi chao kitaumana na timu yenye ubora, hata hivyo anajua uwezo wa Azam ambayo imekuwa ikitoa upinzani mkali kwa Simba.
Mwaka huu, Simba na Azam zimekutana mara tatu katika mashindano yote, ambapo Januari 8, mwaka huu, Azam ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.
Julai 4, mwaka huu, Azam ilifungwa bao 1-0 na Simba, katika mechi ya michuano ya FA.
Hadi sasa, timu hizo zimekutana mara 35 katika mashindano yote makubwa, tangu Azam FC ilipopanda Ligi Kuu mwaka 2008.
Katika mechi hizo, Simba imeshinda mechi 15 huku Azam ikishinda michezo tisa na kutoka sare mara 11.




