Na ATHNATH MKIRAMWENI
MAKAMU wa Rais, Dk. Deogratius Ndejembi, ameipa Wizara ya Viwanda na Biashara miezi sita (sawa na siku 180), kukamilisha maandalizi ya sera maalumu ya biashara changa za kibunifu.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuvutia mitaji, kukuza ajira na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Ameeleza kuwa, sera hiyo, itatoa mwongozo kwa taasisi za fedha, wawekezaji na wadau wengine kuweka mazingira yatakayowezesha biashara hizo kupata mitaji na kukua kwa kasi, badala ya kuendelea kuzichukulia kama biashara ndogo na kati (SMEs), ambazo zina mahitaji na malengo tofauti.
Alitoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam, katika ufunguzi wa Kongamano la Wiki ya Biashara Changa Tanzania, lililojadili nafasi ya taasisi za fedha katika kuwawezesha vijana.
Alisema biashara changa za kibunifu, zina uwezo mkubwa wa kubadilisha uchumi na kusaidia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alieleza kuwa, tofauti na biashara za kawaida zinazoweza kuendelea kwa ukubwa uleule kwa muda mrefu, biashara changa za kibunifu, zina uwezo wa kukua kwa kasi kubwa, kupanua shughuli zake na kuvutia uwekezaji mkubwa kutokana na ubunifu na suluhisho zinazotolewa kwa changamoto za jamii.
Alitolea mfano kijana aliyemtambulisha kwa jina la Alvin, anayekusanya nywele zinazotupwa baada ya watu kunyolewa na kuzitumia kutengeneza bidhaa.
Alisema biashara hiyo siyo tu inatengeneza kipato kwa mwanzilishi wake, inasaidia kutatua changamoto ya utupaji wa nywele na kutoa ajira kwa vijana.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Alvin, biashara hiyo imeajiri vijana 100, jambo linaloonesha namna mawazo ya kibunifu yanavyoweza kugeuka kuwa fursa za ajira na kipato.
Alisema serikali itaendelea kuunga mkono vijana wenye mawazo na miradi yenye tija.
“Nitoe maelekezo kwamba, twende tukaunde sera, tukatengeneze sera ya ‘startups.’ Tusishikilie SMEs kama nilivyokuwa nimeeleza, kuna utofauti mkubwa. Tutengeneze sera ambayo siyo rahisi baadaye kurudi tena kuihuisha,” alisema Ndejembi.
Alisema nchi kadhaa zikiwemo Kenya, Tunisia, Nigeria, Ghana na Afrika Kusini, zimechukua hatua ya kuwa na sera za biashara changa za kibunifu.
Alisisitiza Tanzania inapaswa kujifunza kutoka katika nchi hizo kwa kuweka mwelekeo unaotambulika na kuvutia wawekezaji katika soko la biashara changa.
Alibainisha kuwa, upatikanaji wa mitaji ni miongoni mwa changamoto zinazokabili biashara hizo, akieleza kuwa siyo kila ‘startup’ inahitaji mkopo wa benki, bali nyingine zinahitaji mitaji ya uwekezaji itakayozisaidia kukua na kuvutia wawekezaji wengine.
Aliendelea kusema serikali inaelewa changamoto zinazozikabili taasisi za fedha katika kutoa mikopo kwa biashara, ambazo bado hazijathibitisha uwezo wake wa kurejesha fedha.
Alisema kuna umuhimu wa kuweka mifumo itakayopunguza hatari za uwekezaji na kuvutia mitaji kuelekezwa kwenye sekta hiyo.
Alieleza kuwa, serikali imeanza kutafuta namna ya kushirikiana na wadau wa maendeleo, ukiwemo Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, kusaidia kupunguza hatari za utoaji mitaji kwa vijana na biashara changa za kibunifu, hatua itakayochochea taasisi za fedha kuongeza uwezeshaji.
Ndejembi alipendekeza kuanzishwa kituo maalumu kitakachotumika kama sehemu ya kukutanisha vijana wabunifu, taasisi za fedha, wawekezaji na kampuni kubwa, kwani mazingira hayo yatasaidia kubadilishana mawazo, kutafuta mitaji na kujenga ushirikiano wa kibiashara.
Alisema serikali inaweza kuanza kwa kutafuta jengo lisilotumika, hususan maeneo ambayo baadhi ya ofisi zilihama baada ya shughuli za serikali kuhamishiwa Dodoma, kisha kuliboresha na kuweka miundombinu ya kuwasaidia vijana kufanya kazi na kuendeleza mawazo yao.
Aliongeza kuwa, kituo hicho kinaweza kuwa na huduma za intaneti, maeneo ya mikutano na huduma nyingine zitakazowezesha vijana kufanya kazi pamoja, huku kikiunganisha biashara changa na kampuni kubwa ziweze kushiriki katika minyororo ya thamani.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha vijana wanapata fursa katika uwezeshaji kiuchumi na manunuzi ya serikali kwa sababu mazingira bora ya biashara yanaweza kusaidia mawazo ya vijana kukua na baadaye kuajiri watu wengine.
“Miezi sita tuwe tumekamilisha hili, na mimi nitalisimamia hilo kwa niaba ya Rais wetu kuhakikisha kwamba linafanikiwa,” alisema Ndejembi.
Alisema kuimarishwa kwa biashara changa za kibunifu ni muhimu kwa sababu zinaweza kusaidia kurahisisha maisha ya wananchi kupitia teknolojia na ubunifu katika sekta mbalimbali, zikiwemo kilimo, afya, nishati na biashara.
Ndejembi aliitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kushirikiana na wadau kuhakikisha sera hiyo inakamilika kwa wakati na kuwa msingi wa ukuaji wa biashara hizo nchini.
WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Judith Kapinga, alisema biashara bunifu zina nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na kufungua fursa zaidi ajira kwa wananchi, huku zikichangia kuongezeka kwa thamani ya bidhaa na huduma.
Alisema serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa biashara na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi na kukuza uchumi.
Judith alisema katika mwaka huu, serikali imeweka mkazo katika kuimarisha na kukuza biashara bunifu, hatua inayolenga kuendeleza biashara hizo na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.
TSA
Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Umoja wa Makampuni Changa Tanzania(TSA), Paul Makanza, alisema sekta ya teknolojia nchini imechangia kuimarisha uchumi kwa kuzalisha ajira takribani 174,000 zisizo za moja kwa moja.
Alisema biashara zinazotumia teknolojia zimeendelea kuleta manufaa ya kiuchumi hivyo ni muhimu kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji na ubunifu.
Alisema serikali imekuwa ikitoa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo alikaribisha juhudi za Wizara inayosimamia TEHAMA katika kuendeleza sera na mipango ya kukuza ubunifu.
Hata hivyo alisema programu ya mwaka huu imejikita katika maeneo ya udhibiti, uwekezaji na upatikanaji wa fedha, masoko na ushirikiano hivyo aliwasihi wadau kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta ya teknolojia.




