Na MWANDISHI WETU
WATAALAMU wamehimizwa kuandaa mapendezo na msimamo mahsusi wa Tanzania katika mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 31), kuwezesha upatikanaji wa sh. trilioni 7.3 za miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam Oktoba 27, 2026 na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Richard Muyungi kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Mazingira, Kemilembe Mutasa, wakati wa ufunguzi wa kikao kilichojadili maandalizi ya Tanzania kuelekea mkutano wa COP 31 utakaofanyika nchini Uturuki Novemba 9 hadi 20, mwaka huu.
Dk. Muyungi amesema mkutano huo ni jukwaa maalumu la kuiwezesha Tanzania kupata fedha za miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi hususan katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Programu ya mageuzi ya usimamizi wa mazingira kuelekea dira 2050 imeanisha mahitaji ya shilingi trilioni 7.3…kuelekea katika mkutano huo ni wajibu wetu tutahakikisha fedha hizi zinapatikana kupitia majadiliano katika mkutano huo.”
Katibu huyo amesema katika mkutano wa COP 30 uliofanyika nchini Brazil, Tanzania ilikuwa Mwenyekiti wa Kundi la Afrika la Majadiliano kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, ambapo iliratibu msimamo wa pamoja wa Afrika ikiwemo upatikanaji fedha za tabianchi na utekelezaji makubaliano ya kimataifa.
Ametaja baadhi ya mafanikio iliyopata Tanzania katika mkutano COP 30 ni pamoja na uanzishwaji wa kituo cha mafunzo ya majadiliano ya tabianchi kwa vijana, ambapo hivi karibuni Ofisi ya Makamu wa Rais iliratibu mafunzo ya kwanza yaliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi huu.
Amefafanua mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuandaliwa na kuzinduliwa kitabu cha kumbukumbu cha Miaka 30 ya AGN ambacho kimeweka kumbukumbu ya historia, mafanikio, changamoto na mchango wake katika majadiliano na uamuzi wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Dk. Muyungi amesema mkutano huo pia uliwezesha kuanzishwa ofisi ya kikanda ya mtandao wa Santiago ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji msaada wa kiufundi kwa nchi za Afrika.
Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Bahari kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar, Dk. Makame Omar Makame, amesema Zanzibar ni moja ya maeneo yaliyo hatarini kukabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kupitia sekta za uzalishaji mali ikiwemo kilimo na uvuvi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatarajia kushiriki katika Mkutano wa COP 31 kuunganisha nguvu za pamoja na kuweka mkazo na msisitizo katika upatikanaji wa fedha za miradi ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Mwakilishi kutoka Shirika la Shirika la Kimataifa la Uhifadhi Mazingira na Maendeleo Endelevu (IUCN), Ghaamid Abdulbasat, alisema shirika hilo limeendelea kuimarisha ushirikiano na serikali ya Tanzania katika utekelezaji ahadi za mikataba ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi.




