Na NASRA KITANA
TIMU za Azam FC na Singida Black Stars leo zinatarajiwa kupambana ambapo utamu utakuwa katika takwimu.
Mchezo huo Ligi Kuu Tanzania Bara, umepangwa kutakaofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi, Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 usiku ambapo Singida BS ina pointi saba huku Azam ikiwa na alama tano katika msimamo wa michuano hiyo.
Singida BS ipo nafasi ya 11, Azam ikiwa nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi hiyo, baada ya timu zote mbili kushuka dimbani mara tatu tangu ligi hiyo ilipoanza.
Azam imeshinda mechi moja wakati Singida BS wao wameshinda mechi mbili katika ligi hiyo.
Lakini Azam imefunga mabao manne katika michuano hiyo huku Singida BS ikiwa imepachika mabao matatu.
Hata hivyo, timu zote mbili hazijafungwa mchezo wowote katika michuano hiyo ya msimu wa 2025/26.
Vita nyingine katika pambano la leo ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anaendelea kuwania kiatu cha ufungaji bora baada ya kupachika mabao mawili hadi sasa.
Kinara wa kufunga mabao hadi sasa katika ligi hiyo ni Salehe Karabaka wa timu ya JKT Tanzania ambaye amefunga mabao manne katika ligi hiyo ambapo macho ya mashabiki watataka kuona kama Feisal ataongeza idadi hiyo ya kufunga mabao.
Akizungumza kuelekea katika mchezo huo, Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge alisema wanakwenda katika mchezo mgumu, lakini watapambana kupata ushindi.
“Utakuwa mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa, tunakwenda kupambana na timu bora ambayo ina wachezaji wenye kiwango bora,” alisema Ibenge.
Ibenge alisema kuwa amerekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mechi zilizopita ili kufanya vizuri katika michezo inayofuata ikianza na Singida Black Stars.
Mchezaji wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda alisema wachezaji wote wamejipanga vizuri kupambana kupata ushindi.
“Tunajua wapinzani wetu wana wachezaji wazuri, lakini tumejipanga kucheza kwa ushirikiano mkubwa kuhakikisha tunaibuka na ushindi,” alisema.
Naye Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi alisema kuwa wanakwenda kukutana na timu nzuri hivyo wamejipanga kupambana nayo.
“Azam ni timu bora na ina wachezaji wazuri, nimewaona jinsi walivyokuwa wanacheza, hivyo nitaingia uwanjani kuhakikisha tunatumia mbinu mbadala ya kupata ushindi na tutafanya mashambulizi mwanzo hadi mwisho wa mchezo,” Gamondi.
Mchezaji wa Singida BS, Kennedy Juma, alisema kuwa mchezo huo ni muhimu kwao na wapo tayari kupamabana kwa dakika zote 90 kuhakikisha wanapata pointi tatu.
“Tunaingia katika mchezo mgumu, sisi kama wachezaji hatutakubali kuona tunapoteza tutapambana mwanzo mwisho ili kupata matokeo mazuri,” alisema Kennedy.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Singida BS ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi saba huku Azam ikishika nafasi ya 15 ikiwa na pointi tano ambapo timu zote zimeshuka dimba mara tatu.




