Dodoma
NA SELINA MATHEW
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, ametoa wito kwa vijana kuilinda nchi yao kwa kuhakikisha matukio yaliyojitokeza Oktoba 29 mwaka huu wakati wa uchaguzi mkuu, hayajirudii.
Amesema matukio hayo yaliyochafua taswira ya Tanzania siyo utamaduni wa Taifa na hayaakisi maisha ya wananchi.
Balozi Dk. Migiro aliyasema hayo jijini hapa, alipofungua kongamano la Jukwaa la Wanawake 2025 lililoambatana na kauli mbiu isemayo “Mama ni Amani.”
Katika kongamano hilo lililowakutanisha washiriki zaidi ya 2000 kutoka maeneo mbalimbali nchini, Dk. Migiro alisema wanawake wana mchango wa kipekee kuhakikisha nchi hairudi katika changamoto zilizojitokeza Oktoba 29 mwaka huu.
“Sisi wanawake tuna mchango wa pekee na ili kuhakikisha kwamba haturudi tena katika changamoto ile, tutoe mawazo chanya ambayo yatatutoa hapa tulipo kuendelea mbele kuwezesha Taifa kuendelea kuwa salama.
Alisisitiza: “Siyo utamaduni wetu, siyo hulka wala maisha ambayo sisi Tanzania tumekuwa tukiishi yaliyotupatia sifa kubwa duniani kuwa nchi ya kisiwa cha amani na utulivu, tufanye kila tuwezalo kurejea tena katika nafasi yetu ambayo itaifanya nchi iendelee kuwa kiongozi katika amani, utulivu na maendeleo.”
“Tumeona changamoto zilizotokea, namna ambavyo serikali imesimama imara kuhakikisha kwamba utulivu unarejea katika nchi yetu, shughuli za usalishaji ambazo ziliathiriwa na changamoto hiyo zimeaanza tena,” alibainisha.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji falsafa ya 4R ambayo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiisisitiza kwa kubeba mambo manne likiwemo suala la ustahimilivu.
Alibainisha kuwa kupitia falsafa hiyo, Rais Dk. Samia alieleza nchi ipo tayari kujijenga upya, kuimarisha mazuri yaliyopo na ndiyo sababu jukwaa hilo limewaleta wanawake na vijana wenye mirengo mbalimbali.
“Kwa sababu inapokuja katika Tanzania ni yetu wote, sisi wote hatuna sehemu nyingine pa kwenda ila hapa. Kwa mantiki hiyo ujumuishi huu unadhihirisha umuhimu kwamba tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kwamba haturudi nyuma, haturudi katika changamoto zile,” alisisitiza.
Kuhusu tume iliyoundwa na Rais Dk. Samia kuchunguza kiini cha vurugu zilizojitokeza siku ya Uchaguzi Mkuu, Dk. Migiro alisema ni mwanzo mzuri kuelekea mchakato wa kuimarisha maridhiano.
KATE KAMBA
Kwa upande wake, mwanasiasa mashuhuri nchini, Kate Kamba aliwasilisha mada kuhusu nafasi ya mwanamke katika kulinda amani.
Mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, alisema uwekezaji kwa wanawake ni muhimu katika mustakabali wa taifa kwani ni wajenzi wa maadili na amani kuanzia ngazi ya familia.
“Watoto wafundishwe mila, desturi, utambulisho wa jamii ili kuzuia mmomonyoko wa maadili, tusiwaache wafanye vile jamii haitaki,”alisema Kate ambaye ndiye mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo miaka ya 1980.
SIFA SWAI
Akizungumzia athari za kukosekana amani kwa wanawake na jamii, Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mkoa wa Kilimanjaro, Sifa Swai, alisema kukosekana amani kunaathiri vipato, biashara na maendeleo ya kada mbalimbali.
“Tuhakikishe tunalinda amani kwa nguvu zote, lugha za chuki, matusi vinaweza kuwa chanzo cha mfarakano baina ya watu ndani ya jamii. Vijana wanatumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kusambaza jumbe mbaya ambazo zinasambaa haraka, waache, tutunze amani yetu,” alisema Swai ambaye aliwahi kuwa mweka hazina wa kwanza mwanamke ndani ya CCM.




