Na AMINA KASHEBA
KOCHA mpya wa Simba, Steve Barker ameshauriwa kuanza na usajili wa wachezaji katika eneo la kipa, kiungo mshambuliaji na straika kuwa na kikosi bora ili kufanya vyema msimu huu.
Maoni hayo yalitolewa na wadau mbalimbali wa soka ambapo wanaamini kama kocha huyo kutoka Afrika Kusini atasajili jumla ya wachezaji watatu katika maeneo hayo, timu yake itakuwa bora.
Barker alitangazwa kocha mpya wa Simba wiki iliyopita akichukua mikoba ya Meneja Mkuu, Dimitar Pantev aliyeachana na miamba hiyo kutokana na matokeo yasiyoridhisha.
Katika kikosi hicho, Barker ambaye anatarajiwa kuwasili nchini hivi karibuni kuiongoza timu hiyo, atakuwa na kibarua kizito kuhakikisha Wekundu hao wa Msimbazi wanarejesha makali katika Ligi Kuu Tanzania Bara na kufufua matumaini ya kuwania kucheza robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau wa soka wamesema kwamba kocha huyo anapaswa kufanya usajili katika maeneo hayo kwa kuwanasa nyota mahiri ambao wataongeza ubora kikosini.
Nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella, amesema uongozi wa Simba unapaswa kumpa nguvu ya kusajili wachezaji kocha huyo na nafasi ambazo anaamini Simba ina uhitaji nazo ni kipa bora mfano wa Mousa Camara na Yakoub Mohamed ambao wanauguza majeraha.
Pia, Mogella amesema nafasi nyingine ni kiungo mshambuliaji atakayepika vyema mabaop pamoja na straika bora atakayekuwa tishio katika lango la wapinzani.
“Sio kama Simba haina wachezaji wazuri, lakini eneo la umaliziaji wa kupata mabao ndiyo inakuwa tatizo hapo wanatakiwa kupambana na kutumia fedha nyingi kupata mshambuliaji ambaye atawaletea ushindi baada ya kupata kocha mpya.
“Pia, kitu kingine wanatakiwa kupata mchezaji eneo la kati ambaye ana mipango mizuri ya kumiliki mpira na kutoa pasi zenye kuleta manufaa katika timu, mara nyingi Simba imekuwa inakosa utulivu sehemu hiyo,” amesema.
Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema Simba ina wachezaji wazuri hivyo maboresho yanayohitajika ni madogo kuwa na kikosi bora zaidi kitakachofanya vyema.
“Simba inapaswa kuwa na kipa zaidi ya wawili au watatu ambao wana ubora mzuri, kama itatokea moja wao amepata majeraha kunakuwa na wengine ambao watasimama katika mechi, pia wanapaswa kuangalia eneo la ushambuliaji ambao mara nyingi limekuwa haliwapi matokeo,” amesema.
Kocha wa soka la vijana, Maalim Salehe alisema hivi sasa Simba inachohitaji kukifanya ni kuangalia makosa yao na kusajili baadhi ya wachezaji ambao wanaamini wataongeza ubora kikosini.
Katika Ligi Kuu Bara, Wekundu hao wa Msimbazi wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 12 baada ya kushuka dimbani mara tano, wakishinda mechi nne na kutoka sare moja.
Pia, miamba hiyo haijapata ushindi wala sare katika mechi zote mbili za kwanza za kundi D katika CAFCL, ikikubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Petro de Luanda ya Angola nyumbani na 2-1 dhidi ya Stade Malien ya Mali ugenini.
Kundi hilo linaundwa na Simba, Stade Malien, Petro de Luanda na Esperance de Tunis ya Tunisia.
Simba imebakiwa na mechi nne katika kundi hilo ambapo ili itinge robo fainali inapaswa kushinda angalau mechi tatu na kutoka sare moja.




