Na MWANDISHI WETU
BAADHI ya wadau wa michezo nchini, wamempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio ya Taifa Stars katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), kuwa yametokana na juhudi zake za kuiwezesha na kuiletea nchi heshima kubwa.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, wamesema kitendo cha Rais kuweka nguvu ndani ya timu hiyo, kimetoa hamasa kwa wachezaji kufanikiwa kutinga 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Neema Msitha amesema siku 100 za Rais Dk. Samia kuwa madarakani kumepatikana mafanikio makubwa.
“Siku 100 za Rais Dk. Samia kukaa madarakani zimeleta mafanikio mengi, angalia timu ya Taifa Stars imefanya vizuri kule Morocco, miundombinu ya viwanja inaendelea kujengwa,”amesema.
Amefafanua kuwa, shule 56 za vipaji ambazo zitajengwa kwa kukuza vipaji na kuviendeleza.
Ametoa wito kwa vijana kumuunga mkono Rais Dk. Samia kwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na kuiletea heshima nchi.
“Vijana nawaomba watumie michezo kama ajira, kwani miundombinu Rais Dk. Samia ameiwezesha, kazi kwao vijana kufanya vitu vyao ndani ya viwanja,”amesema.
Kwa upande wa Rais wa Sanaa na Maonesho, Dk. Cynthia Henjewele, amesema Rais Dk. Samia ndani ya siku 100, amefanya kazi kubwa kuwezesha kuwepo mfuko wa sanaa na utamaduni ambao ni chachu ya mafanikio kwa wasanii kufanya vizuri
“Kujengwa kwa shule za sanaa na utamaduni 40, saba zimeanza kujengwa, nina imani kutaongeza hali ya wasanii wengi kujitokeza kwenda kusoma na itainua vipaji vya vijana kupata ajira kupitia sanaa ,” amesema Dk. Cynthia Henjewele.
Kiongozi huyo, alisema kuwepo kwa mirabaha ya wasanii kumeongeza nguvu ya wanamuziki kutunga nyimbo zenye maadili ya nchi.
Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa alisema Rais Dk. Samia ni mdau mkub wa wa soka tangu akiwa Makamu wa Rais amekuwa anatoa hamasa kubwa ya michezo nchini.
Kauli hizo, zimekuja baada ya Rais Dk. Samia kusema mafanikio ya Taifa Stars katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), yameiletea nchi heshima kubwa na ushahidi tosha kwa Dunia kuwa soka la Tanzania linaendelea kukua na kupanda viwango barani Afrika.
Alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam, Januari 10, mwaka huu katika sherehe maalumu ya kuwapongeza vijana hao, baada ya kufikia hatua ya 16 bora ya fainali hizo zilizofanyika nchini Morocco.
“Hongereni sana, mmefanya kazi nzuri sana. Tunajua kilichotokea na sababu zake, kwa kuwa walikuwa wenyeji, taifa lenye rasilimali na lenye ushawishi katika uandaaji.
“Hata hivyo, dunia imeona wazi kuwa Tanzania ina wapambanaji, na mmepambana kwa nguvu zenu zote. Nawapongeza sana,” alisema Rais Dk. Samia.
Hivi karibuni, mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) yalifanyika nchini Morocco, ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi shiriki na kuonesha ushindani wa hali ya juu.
Taifa Stars ilipangwa kundi C na timu za Nigeria, Uganda na Tunisia na kufanikiwa kutinga hadi hatua ya timu 16 bora.
Mafanikio hayo, yametokana na juhudi kubwa za Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ambazo zilihakikisha maandalizi mazuri.
Timu hiyo, ilikuwa kambini nchini Misri pamoja na kupata mechi za kirafiki zilizosaidia kuimarisha uwezo wa kikosi hicho.
Ikumbukwe kuwa, Tanzania imeshiriki mashindano ya AFCON kwa mara ya nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957, ikiwa ni baada ya kushiriki miaka ya 1980, 2019 na 2023.
Ushindi wa Taifa Stars katika mashindano hayo, ulishuhudiwa na Watanzania wengi, ambapo kwa upande wa wizara, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda aliambatana na timu hiyo katika mashindano hayo.
Akiwa katika kambi ya timu, Waziri Makonda alizungumza na wachezaji, benchi la ufundi na kuwasisitiza kupambana kwa kutanguliza uzalendo wanapovaa jezi ya Taifa.
“Taifa zima lina imani kubwa nanyi. Chezeni kwa moyo, kwa umoja na kwa kujituma, mkijua mna mamilioni ya Watanzania wanao waombea na kuwaunga mkono,” alisema Makonda.
Kauli hiyo iliongeza hamasa kubwa timu ya Taifa Stars, ambao walipambana kwa hali ya juu na hatimaye kufuzu hadi hatua ya timu 16 bora.
Mafanikio hayo yaliiongezea Tanzania heshima katika tasnia ya soka na kuiwezesha kupanda hadi nafasi ya 110 katika viwango vya ubora wa soka duniani.
Kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. Samia, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limempa zawadi ya Tuzo ya Heshima, kufuatia kutambua mchango mkubwa wa kukuza mchezo huo nchini na Afrika kwa ujumla.
CAF ilitoa tuzo hiyo Novemba 19, mwaka jana mjini Rabat nchini Morocco
ikiwa na lengo la kutambua mchango wa Rais Dk. Samia, katika maendeleo ya soka nchini na Afrika kwa ujumla.
Tuzo hiyo, imetolewa ndani ya siku 100 za uongozi wa awamu ya sita baada ya CAF kufurahishwa na utendaji kazi wa Rais Dk. Samia kwa kukuza sekta ya mpira wa miguu.
Mafanikio hayo, yamepatikana kupitia tuzo maalumu aliyopokea Rais Dk. Samia kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Katika hafla hiyo, tuzo ya kwanza kwa Rais Dk. Samia ambayo ilitolewa na Rais wa CAF, Dk. Patrice Motsepe kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya soka nchini.
Pia, Motsepe alitoa tuzo nyingine kwa Rais Yoweri Museven wa Uganda na Rais wa Kenya, William Ruto.
Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Dk. Samia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema serikali ya Tanzania inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa CAF na FIFA kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua.
Tuzo nyingine ilikwenda kwa nyota wa Yanga, Clement Mzize ambaye alishinda tuzo ya ‘Goli Bora la Mwaka’.
Mchezaji huyo alifunga bao hilo katika mchezo kati ya Yanga na TP Mazembe mechi ya CAF.
Mchezo huo, ulipigwa Januari 4, mwaka huu ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.





