Na NASRA KITANA
KOCHA Mkuu wa Young Africans, Pedro Goncalves, ametamba kuwa wamelenga kupata ushindi dhidi ya Prisons licha ya kukabiliwa na majeruhi kwa baadhi ya wachezaji akiwemo Clement Mzize.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri, Pedro alisema kikosi chake kimejiandaa vizuri huku akili zao zikilenga kufanya vizuri na kufikia malengo ya klabu.
“Tutakuwa na mazoezi ya mwisho kujiandaa na mechi dhidi ya Tanzania Prisons. Tunajua tunakwenda kucheza na timu ngumu ambayo imetoka kupoteza mechi dhidi ya Simba na baadaye kupata sare na Azam FC.
“ Tuna uhakika mchezo utakuwa mgumu, lakini tupo hapa kwa ajili ya alama tatu na tunaamini tutazipata,” alitamba kocha huyo.
Kipa wa Yanga, Hussein Masalanga alisema wachezaji wote wamejiandaa vizuri na wanafahamu umuhimu wa kushinda mchezo huo.
“Sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri na tunajua umuhimu wa mchezo huu. Tunajua tunakwenda kucheza na timu ngumu yenye wachezaji wazuri, lakini tutawaheshimu na kupambana kwa sababu lengo letu ni pointi tatu,” alisema Masalanga.
Juzi, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Ajabu Kifukwe, alisema kuwa kikosi chao chote kipo fiti kuivaa Yanga.
Aliongeza kuwa maandalizi ya timu yamekamilika na wachezaji wako katika hali nzuri ya kiufundi kuelekea mchezo huo muhimu.
Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na poin ti 32 baada ya kushuka dimbani mara 12 katika ligi hiyo huku Prisons ikiwa na alama 13 baada ya kucheza mechi 15 za ligi hiyo.
Lakini kauli ya kocha wa Yanga, Pedro Goncalves imekuja baada ya hivi karibuni, Clement Mzize kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini ambapo atakuwa nje ya uwanja hadi mwishoni mwa msimu.
Mzize anatarajiwa kurudi dimbani msimu ujao wa 2026/2027.
Wakati huo huo, beki wa Yanga, Dickson Job amefanyiwa upasuaji wa goti, jana, baada ya kuumia katika mchezo wa ‘dabi’ dhidi ya Simba.
Job alipata majeraha hayo kipindi cha kwanza katika mechi ya ‘Kariakoo Dabi’ dhidi ya Simba iliyochezwa Machi Mosi, mwaka huu viwani Zanzibar.
Katika mchezo huo, Job alipata majeraha hayo baada ya kugongwa na kiungo wa Simba, Inno Loemba wakati wakiwania mpira na kushindwa kuendelea kucheza mechi hiyo iliyomalizika kwa matokeo ya suluhu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa nahodha huyo msaidizi amefanyiwa operesheni asubuhi ya leo(kesho) kwa mujibu wa madaktari hali yake inaendelea vizuri.
“Nahodha wetu Dickson Job amefanyiwa operesheni asubuhi ya leo(jana) nchini Afrika Kusini na ‘Alhamdulillah’ jambo limekwenda vizuri kabisa,” alisema.
Kamwe alisema taarifa ya awali kutoka Afrika Kusini, imeeleza kuwa beki huyo atakaa nje ya dimba kwa kipindi cha miezi mitatu akiuguza jeraha hilo.
Ofisa habari huyo aliwaomba mashabiki na wapenzi wa soka nchini kumuombea mchezaji huyo ili apone kwa haraka.
Hayo ni majeraha ya kwanza makubwa kwa Job, tangu asajiliwe na timu hiyo aliyojiunga nayo Januari 11, mwaka 2021 akitokea timu ya Mtibwa Sugar ya Turiani mkoani Morogoro.




