AMINA KASHEBA Na NASRA KITANA
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kutwaa ubingwa wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Idhaa za Kiswahili iliyofanyika jijini Arusha, Makonda amesema Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda ina kila sababu ya kuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Amesema kipindi cha mashindano hayo itakuwa dirisha muhimu la kuitangaza Tanzania Bara na Zanzibar huku matumizi ya lugha ya Kiswahili katika matangazo na mawasiliano ya mashindano hayo yatasaidia kukuza hadhi na ushawishi wa Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
“Mwakani mashindano ya AFCON, Zanzibar wamejipanga kikamilifu, Dar es Salaam wamejipanga na Arusha hivyo hivyo, miji yetu hii mikubwa mitatu ni ndoto yetu ichukue asilimia 60 ya mashindano ya Afcon 2027.
“Mashindano haya yanakwenda kuitangaza nchi yetu kufanya alama ya amani, mshikamano na utulivu, pia kuonyesha fursa za uchumi wa Tanzania, ” alisema Makonda.
Waziri huyo amesema kuwa ushiriki wa Tanzania katika michuano hiyo unatoa nafasi ya kipekee ya kulitangaza taifa kimataifa.
KOCHA GAMONDI
Kocha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Miguel Gamondi, amesema kikosi chake kipo fiti kuhakikisha kinapata ushindi katika mechi mbili za kirafiki za mashindano ya FIFA Series 2026.
Taifa Stars ambayo jana ilikwenda Rwanda kushiriki michuano hiyo, itavaana na Liechtenstein na kama itaibuka na ushindi itacheza na bingwa kati ya Aruba na Macau.
Akizungumza kabla ya kuondoka nchini, Gamondi amekiri mechi hizo zitakuwa ngumu lakini hana wasiwasi na kikosi chake kwani anaamini kitafanya vyema.
Gamondi raia wa Argentina, alisema kila mchezaji wake anafahamu umuhimu wa mechi hizo hivyo watahakikisha wanaonyesha kiwango bora kupata ushindi.
“Tumejipanga vizuri kwa mashindano hayo muhimu, lengo letu ni kuhakikisha tunashinda katika kila mchezo ili tufanye vizuri na kurejea nyumbani na ushindi,” alisema Gamondi.
Naye beki wa timu hiyo, Bakari Mwanyeto alisema kila mchezaji yupo tayari kuipambaniua bendera ya Tanzania na anaamini michuano hiyo itawapa uzoefu mkubwa kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani.
“Tunakwenda katika mashindano haya tukiwa tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapambana ili kuonyesha uwezo tuliokuwa nao, pia yatatusaidia katika maandalizi ya AFCON,” alisema.
Kiungo Novatus Dismas, alisema: “Kila mchezaji yupo vizuri kwa michezo ya FIFA Series, pia mwalimu ametuandaa vyema kiakili tufanye vizuri zaidi,”.
Naye kipa wa timu hiyo, Aishi Manula alisema amefurahi kurejea tena katika timu ya taifa na aliwakahikikishia Watanzania kuonyesha kiwango bora.




